Matumaini ndege aina ya airbus za ATCL kuendelea kutoa huduma

Dar es Salaam. Ikiwa zimepita wiki mbili tangu Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lisitishe baadhi ya safari kutokana na matatizo ya injini kwa baadhi ya ndege zake, dalili za matumaini ya kurejea kwa ndege hizo kwenye ratiba ya kawaida zimeibuka.

Gazeti hili limegundua kuwa ATCL ipo mbioni kuzikarabati injini za ndege zake aina ya Airbus220-300, zilizokuwa zimepata hitilafu na kusababisha ratiba ya safari za shirika hilo kubadilika.

Kama ilivyo kwa mashirika mengine ya ndege duniani, baada ya ndege za ATCL kukumbwa na tatizo hilo, ililazimika kusitisha safari za ndege zake tatu kati ya nne za aina hiyo.

Hii ilisababisha kupunguza baadhi ya safari kupisha matengenezo ya injini.

Katika mahojiano maalumu juzi na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema ndege hizo zitafanyiwa ukarabati na kampuni ya Airbus (watengenezaji wa ndege hizo), ambao wamesema watatoa injini moja ya ziada.

“Leo (Jumatatu) tulikuwa na mkutano na wasimamizi wa Airbus, wametuahidi kutoa injini moja ya ziada kabla ya kuisha kwa mwezi huu,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa sasa wanafanya maandalizi ya kuona namna nzuri ya kuifikisha injini hiyo hapa nchini.

Kuletwa kwa injini hiyo kutaikwamua ndege moja kati ya tatu zilizoharibika.

Kuhusu ndege nyingine mbili zilizosimama kufanya kazi kutokana na hitilafu mbalimbali, Matindi alisema mwezi ujao injini zake zitapelekwa Frunkfurt nchini Ujerumani kwa matengenezo.

“Hizi ndege nyingine mbili kama mambo yatabaki sawa, mwezi ujao injini zake tutazipeleka kwenye kituo cha matengenezo kilichopo Frankfurt, Ujerumani,” alisema.

ATCL, yenye jumla ya ndege 11, inamiliki ndege nne aina ya Airbus A220-300, huku A220 moja pekee ikiruka hadi sasa na nyingine zikiwa na hitilafu.

Mwananchi limefanya uchunguzi na kubaini kuna ndege 250 aina za A220-300 duniani, huku nyingi zikisemekana kuacha kufanya safari zake kutokana na hitilafu kwenye injini.

Matindi aliliambia gazeti hili kuwa katika mkutano wake na Airbus, uliofanyika Jumatatu, kampuni hiyo ilikuwa ikichukua hatua kadhaa kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya huduma kutoka kwa mashirika ya ndege.

“Wanachofanya sasa ni kukabiliana na uhaba wa injini kwa kutengeneza injini za ziada,” alisema.

“Airbus itaongeza karakana kutoka tatu za sasa hadi sita,” aliongeza Matindi, akielezea juhudi za Airbus kwenye kufanya matengezo ya ndege zake.

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA CCC), jana limetoa wito kwa mashirika ya ndege yenye uhaba wa ndege kutokana na matatizo ya kiufundi au kiuendeshaji kuzingatia ukodishaji wa ndege ili kufanya shughuli zao kama kawaida.

“Tunashauri mashirika ya ndege kutafuta njia mbadala, ikiwa ni pamoja na kukodisha, ili waweze kuendelea kutoa huduma katika soko la anga ambalo limekuwa likikua kwa kasi nchini,” TCAA CCC ilisema katika tangazo lililochapishwa kwenye vyombo vya habari vya ndani jana.


Si kosa la mashirika ya ndege

Historia ya usafiri wa anga duniani kupitia tovuti kongwe ya habari hizo (Aviation Source) inasema tatizo hilo lilianza kujitokeza mwaka 2014 kwa ndege aina ya A220 ambazo ziliitwa ‘C-Series’.

Kwa mujibu wa Chanzo cha Usafiri wa Anga, wakati huo Bombardier ilikuwa mmiliki wa C-Series ambayo ilikuwa bado katika hatua ya awali ya kuzinduliwa.

Lakini pia, Oktoba 16, 2019, Shirika la ndege la SWISS International Airlines ambalo linamilikiwa na Shirika la ndege la Lufthansa la Ujerumani, lilisimamisha safari za ndege zake zote za aina ya Airbus A220 kutokana na matatizo ya injini zake.

Injini zote za ndege hizo zililazimika kukaguliwa ili kuhakiki usalama wake. Ndege hizo hutumia injini aina ya PW 1500G zilizotengenezwa na kampuni ya Pratt & Whitney ya Canada.

Shirika hilo lilisema lipo katika mazungumzo na mamlaka za usimamizi wa usafiri wa anga na pia mtengenezaji wa ndege hizo ambaye ni kampuni ya Airbus.

Mamlaka ya usafiri wa anga ya Marekani, FAA ilitoa mwongozo kwamba injini zote za A220 ambazo ni Pratt & Whitney zinatakiwa kufanyiwa ukaguzi zaidi wa kiusalama.

A220 si ndege pekee yenye matatizo kwa sasa, ila inaongeza idadi katika orodha ya ndege zenye matatizo. Nyingine ni Boeing 737 MAX na Boeing 787 Dreamliner ambayo pia ina matatizo katika injini zake aina ya Rolls Royce Trent 1000.