Mawaziri wapya hawa hapa...

#LIVE-Mawaziri wapya hawa hapa...

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri huku akiteua mawaziri wapya watano.

Akitangaza mabadiliko hayo leo Jumamosi Januari 8, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga amesema Rais amefanya mabadiliko ya muundo katika wizara tatu.

Mawaziri wapya watano walioteuliwa ni; Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Hamad Masauni (Mambo ya Ndani), Dk Pindi Chana (Sera Bunge na Uratibu), Anjelina Mabula (Ardhi) na Husein Bashe (Kilimo).

Pia Rais Samia ameteua manaibu waziri wapya katika wizara tano.

Manaibu waziri hao wapya walioteuliwa ni pamoja na; Anthony Mavunde (Kilimo), Jumanne Sagini (Mambo ya Ndani) Dk Lemomo Kiruswa (Madini), Ridhiwani Kikwete (Ardhi) na Atupele Mwakibete (Ujenzi na Uchukuzi).

Pia, Rais Samia amewabadilisha na kuwahamisha mawaziri katika wizara tisa.

Mawaziri hao waliohamishwa wizara za awali wafuatao na wizara wanazohamishiwa katika mabano; Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ummy Mwalimu (Afya), George Simbachawene (Katiba na Sheria), Profesa Joyce Ndalichako (Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Innocent Bashungwa (Tamisemi).

Mawaziri wengine waliohamishwa ni; Profesa Adolf Mkenda (Elimu), Dk Doroth Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu), Mohamed Mchengerwa (Utamaduni, Sanaa na Michezo), Dk Ashatu Kijaji (Uwekezaji, Viwanda na Biashara).

Manaibu waziri waliohamishiwa wizara ni pamoja na; Khamis Khamis (Muungano na Mazingira), Hamad Chande (Fedha na Mipango) na Mwanaid Khamis (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu).

Rais Samia pia amefanya mabadiliko ya wizara tatu na kuunda wizara mpya ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Wizara ya Afya na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Waliokuwa mawaziri na hawakuchaguliwa mabadiliko hayo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji Geoffrey Mwambe na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi Mwita Waitara.

Balozi Kattanga amesema mawaziri wapya na manaibu waziri wapya wataapishwa Jumatatu Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Rais Samia amefanya mabadiliko hayo ikiwa anatimiza ahadi yake ya kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Jumanne Januari 4, 2022 Rais Samia wakati akipokea taarifa ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, Rais Samia alidokeza mpango wa kulifumua baraza lake la Mawaziri.