Rais Samia kufumua Baraza la Mawaziri

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amesema baada ya kukaa kwenye nafasi hiyo miezi nane, anategemea kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema baada ya kukaa kwenye nafasi hiyo miezi nane, anategemea kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni.

Rais Samia amedokeza hayo leo Jumanne Januari 4, 2022 Ikulu ya Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.

Amesema kuwa baada ya kuwasoma kwa muda, sasa anatarajia kutoa orodha mpya ya wateule ambao anaona watamsaidia kuwaletea wananchi maendeleo.

“Nimeweka watu ninaoamini mtanisaidia kazi, wakuu wa mikoa nimekuwekeni nikiamini kule nilikowakasimia madaraka mtakwenda kusimamia kazi nawengine wote makatibu wakuu na mawaziri” amesema

“Nimekaa nadhani huu ni mwezi wangu wa nane sijui, nilisema nilikuwa nawasoma nanyi mnanisoma, na siku niliyofanya mageuzi ya mawaziri kidogo nikasema hapa nimeweka koma, kazi inaendelea”

Nataka niwaambie nitatoa listi mpya hivi karibuni, wale wote ninaohisi wanaweza kwenda na mimi nitakwenda nao” amedokeza mkuu huyo wa nchi


Kelele za mkopo wa Sh1.3 trilioni

Akizungumzia watu anaosema wanapiga kelele kuhusu mkopo wa Sh1.3 trilioni, Rais Samia amesema kuwa kelele hizo zinaletwa na joto a uchaguzi 2025.

Amesema mkopo huo ambao Serikali iliupata kwaajili ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 ni mzuri na haijawahi kutokea kama huo tangu nchi ipate uhuru.

Amesema “Huwezi kuamini mtu mzima na akili yako unaenda una-argue tozo na mkopo wa 1.3 trilioni kama vile ndio kwanza umetokea Tanzania wakati toka tumepata uhuru ni mikopo kwenda mbele na katika mikopo yote huu ni mkopo mzuri ever”

“Mtu na akili yake anakwenda kusimama ana-argue, ni uhuru wake kusema chochote lakini ni mtu tunayemtegemea, mtu ambaye mna matumaini naye mtashirikiana naye kwenye safari ya maendeleo hutegemei atasema hicho, unategemea labda atakuwa na uelewa hasa kwa sababu ma bajeti yote, mamikopo yote na taarifa zote za kiuchumi ndani ya nyumba yake ndio zinapita, lakini ni 2025 fever, wasameheni” amesema Mkuu huyo wa nchi bila kutaja aliotaka wasamehewe

“Wasameheni, ninalotaka kuwaambia nitajitahidi kila fursa nitakayoiona ninayoweza kutumia kuleta maendeleo Tanzania nitaitumia, wala sifanyi hivi kwaajili ya uchaguzi 2025” amesema

Utabiri watimia?

Rais Samia amesema baada ya kuapishwa kuiongoza nchi, kuna mtu alimuambia kuwa anayeweza kumsumbua katika uongozi wake sio kutoka upinzani.

“Hapa inanikumbusha hadithi moja, kuna mtu mmoja nilipotwishwa huu mzigo akanitafuta alivyonipata akaniambia; mama nimekuja kukupa hongera lakini pole, nikamwambia napokea” amesema Rais Samia na kuendelea;

“Akanipa mawaidha mengiii akaniambia; lakini nataka nikuambie atakayekusumbua katika kazi yako na uongozi wako ni shati la kijani mwenzio wala sio mpinzani, huyo ndiye atakayekusumbua” amesimulia

“Shati la kijani mwenzio anayetizama mbele mwaka 2025-2030 huyu ndiye atakayekusumbua” anasimulia Rais akisema yameshatokea

“Nataka niwaambie ndicho kinachotokea, kwa sababu huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika muhimili aende akaseimame aseme yale,   ni stress ya 2025” amesema


Sababu ya kukopa badala ya tozo

Rais Samia amesema lazima nchi ikope kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa madarasa kwa kuwa fedha za tozo haziwezi kutosheleza mahitaji ya miradi hiyo.

Amesema kuna mahitaji wa madarasa mengi katika sekta ya elimu ambayo kwa kutegemea fedha ya tozo itachukua muda mrefu kukamilisha mahitaji hayo.

"Lakini ndugu zangu tulichopata hapa leo zaidi ya fedha hizo za Uviko-19, kuna fedha ya tozo ambayo na yenyewe ilipoanza ilipigiwa kelele eee, tukasema ngoja tupunguze tukapunguza, baada ya kupunguza kelele zimeshuka” amesema Rais nakuongeza

“Lakini wapigaji kelele hao wa sasa hivi waliuliza kuna fedha ya tozo kwa nini tunakwenda kukopa”

Amesema mpaka sasa fedha zilizopatikana kwenye tozo zimejenga madarasa 500 lakini uhitaji wa ni zaidi ya madarasa 10,000 kwa shule za msingi pekee.

"Takwimu zilizotolewa na mawaziri hapa zinatosheleza kwamba pamoja na kwamba tuna fedha za tozo mahitaji ya madarasa shule za msingi ni 10,000 mpaka sasa hivi, tumeweza madarasa 500 kwa fedha za tozo, tunafika lini? Amehoji Rais Samia na kusisitiza

“Lazima tukope tuweke miundombinu”

Amesema kuna uhitaji mkubwa wa madarasa kwa siku zijazo hivyo kutegemea fedha ya tozo itachelewesha kufikia malengo kwa wakati

“Tuna madarasa mbele yanahitajika, tunayajenga kwa fedha za tozo kweli?, ambayo mpaka sasa imetusaidia madarasa 500, hatuwezi kwenda na fedha ya tozo”

"Kwa hiyo inashangaza kuona mtu mwenye uelewa anasema kuna fedha ya tozo lakini kaenda kukopa ya nini au kwa nini tunaendelea kutoza tozo wakati fedha ya mkopo ipo” amesisitiza