Ndugai: Kuna siku nchi itapigwa mnada

Muktasari:

  • Wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai akihoji wanaofurahia nchi kukopa na kwamba deni limefika Sh70 trilioni, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni lazima serikali ikope ili kumaliza miradi ya maendeleo.


Dodoma. Wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai akihoji wanaofurahia nchi kukopa na kwamba deni limefika Sh70 trilioni, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni lazima serikali ikope ili kumaliza miradi ya maendeleo.

Akizungumza jana Desemba 28 katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma, Ndugai alitetea uamuzi wa Bunge kuanzisha tozo za miamala ya simu, kuliko kuendelea kukopa.

“Juzi mama ameenda kukopa 1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alisema Spika Ndugai.

“Tutembeze bakuli ndio heshima, tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku,’ amesema Ndugai huku akitetea tozo kwamba; “Tukasema pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.

 “Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya ku-run nchi (kuongoza nchi) hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” alihoji Ndugai kwenye mkutano huo wa kimila wa kabila la Wagogo.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, Rais Samia akizungumza leo Desemba 28 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa SGR uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, amesema Serikali itaendelea kukopa ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo.

Mkataba huo ulilenga kukamilisha kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368, kitakachogharimu dola za kimarekani dola 1.908 bilioni sawa Sh4.41 trilioni kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Yapi Merkez kutoka Uturuki.

"Kama nilivyosema uwekezaji mpaka sasa ni Sh14.7 trilioni hivyo tusipoendeleza ujenzi huu tukakamilisha, fedha tulizolaza pale chini zitakuwa hazina maana. Kwahiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote tutakopa… tutaangalia njia rahisi, zitakazotufaa za kukopa

 “Kwani fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala kwenye kodi tunazokusanya ndani ni lazima tutakopa ili kukamilisha mradi huu. Ni lazima tukope twende tumalize huu mrad,” amesema Rais Samia.

Amsema Mradi wa SGR ulianza kutekelezwa kwa mujibu wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ulianza mwaka 2017 na umegawanyika katika vipande vitano ukipita katika mikoa tisa.

Amesema kwasasa ujenzi huo unaendelea katika vipande vitatu cha Dar es Salaam- Morogoro (asilimia 95), Morogoro- Makutupora (asilimia 77) na Mwanza-Isaka (asilimia 4) ambapo ni jumla ya kilometa 1063 za njia kuu za reli pamoja na njia za kupishana.

“Hii ni kazi kubwa yenye kuhitaji uthubutu mkubwa wa serikali na wananchi wake. Hii inafanya uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati ya vitano vinavyoendelea kufikia kiasi cha sh 14.7 trilioni ukijumlisha na kodi,” amesema.