Samia awajibu wanaokosoa miradi ya Serikali

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewashukia wanaodai miradi yote iliyoanzishwa na Serikali haiwezi kuendelezwa.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewashukia wanaodai miradi yote iliyoanzishwa na Serikali haiwezi kuendelezwa.

Amesema Serikali itaendelea na miradi yake ya kimkakati ikiwemo kukamilisha na kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani.

Ameyasema hayo leo Jumanne Desemba 28, 2021 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368, kitakachogharimu dola za Marekani bilioni 1.908 sawa na Sh4.41 trilioni kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Yapi Merkez kutoka Uturuki.

“Niliahidi kuendeleza mema yaliyopita, yaliyopo na kuanzisha mema mapya. Ujenzi na utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na inayoendelea…, tutaendelea kuisimamia na kuhakikisha inakamilika. Sasa kuna wale ambao walipenda kuona  miradi hii haiendelezwi na wanathubutu kusema kwamba miradi hii imeshindikana, haiendelezwi.

“Pamesemwa hapa makandarasi hawadai hata senti moja ila Serikali inadai kazi, hivyo hivyo kwa miradi mikubwa mingine. ujenzi wa bwawa tunakwenda nao vizuri hatudaiwi na miradi mingine yote iliyoachwa tunakwenda nayo vizuri.

“Na mkipita pita huko hakuna mradi uliosimama, miradi yote inaendelea. Nataka kuwaambia Watanzania tutasimamia miradi iendelee…, kwa hiyo kama walidhani kutakuwa na kusimamishwa miradi ili wapate la kusema halipo. Tutaendelea na ujenzi wa miradi, kuna jitihada za kutuvunja moyo katika mikopo, hata hizo nchi zilizoendelea zina mikopo mikubwa kuzidi ya kwetu…,tutakopa tumalize miradi ya maendeleo,” amesisitiza.