Mkufunzi wa sensa akutwa amefariki dunia nyumba ya kulala wageni

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao

Muktasari:

Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022. Kwa sasa semina na mafunzo yanaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali.

Tabora. Bahati Msengi ambaye ni mkufunzi wa sensa amekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni, Kata ya Kanyenye mkoani Tabora.

 Mkufunzi huyo ambaye pia alikuwa afisa elimu kata ya Milambo, wilayani Kaliua mkoani humo, alihudhuria mafunzo ya siku 21 yaliyomalizika juzi Jumanne na kufungwa na mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian, katika Chuo Cha Ualimu Tabora.

Msengi alikutwa amefariki jana Jumatano Julai 27, 2022 saa nane mchana katika nyumba ya kulala wageni ya Wema.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema tukio hilo ni kifo cha kawaida kama vifo vingine vinavyotokea hospitalini.

Naye Jirani wa nyumba hiyo ya wageni, zaidi Ahmed amesema mkufunzi huyo hakuwa ametoka ndani tangu alipoingia kulala juzi na ndipo walipofika baadhi ya jamaa na ndugu walioangalia kupitia dirishani na kumuona amelala kifudifudi.

Amesema walimuita kwa muda mrefu bila mafanikio na kuamua kuuvunja mlango wa chumba na kumkuta akiwa amekwisha kufariki dunia.

Mmoja wa wageni waliolala katika nyumbani hiyo na kuomba hifadhi ya jina lake alisema mkufunzi huyo aliingia chumbani na kulala baada ya kusalimiana naye mna alionekana kuwa mwenye afya njema.