Mmoja auawa, wafuasi wa Chadema, ACT wakamatwa
Muktasari:
Wanachama zaidi ya 100 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na matukio mbalimbali hasa vurugu katika Uchaguzi Mkuu huku mmoja akiuawa mkoani Mara.
Mikoani/Zanzibar. Wanachama zaidi ya 100 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na matukio mbalimbali hasa vurugu katika Uchaguzi Mkuu huku mmoja akiuawa mkoani Mara.
Aliyeuawa ni Nyatega Wenje ambaye ni mdogo wa mbunge wa zamani wa Chadema Jimbo la Nyamagana, Ezekia Wenje anayedaiwa kufariki dunia katika vurugu za kisiasa.
Wanachama na wafuasi wengine wa ACT na Chadema wanashikiliwa na polisi katika mikoa ya Mara wilaya za Tarime/Rorya, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera na kisiwani Zanzibar.
Wilaya za Michire na Rorya inadaiwa vurugu kubwa zilitokea kusababisha kifo hicho cha Nyatega huku baadhi ya watu wakirejuruhiwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, William Mkondya hakupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokewa.
Mkuu wa wilaya hiyo, Simon Odunga alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo akisema polisi wanaendelea kuimarisha ulinzi na usalama.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Odunga alimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Nyatega ambaye ni kaka wa aliyekuwa mgombea ubunge Rorya Chadema Wenje ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria.
Odunga alisema vurugu hizo zilitokea Oktoba 30 na kusababisha majeruhi ambao idadi yao haijajulikana.
Alisema vurugu hizo ziliwahusisha wakazi wa Kijiji cha Michire ambao ni watu wa jamii na ukoo mmoja waliogawanyika katika imani na itikadi za kisiasa.
“Awali, watu wa jamii hiyo walikuwa wafuasi wa Chadema kabla ya kugawanyika katika uchaguzi wa mwaka huu; baada ya matokeo kutangazwa, kuliibuka ugomvi kati yao na hatimaye kusababisha kifo,” alisema Odunga.
Bila kufafanua mazingira wala chanzo cha vurugu hizo, mkuu huyo wa wilaya alisema Nyatega alifariki dunia akiwa njiani kukimbizwa hospitali baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Mabomu ya machozi nyumbani kwa Wenje
Akizungumzia tukio la polisi kufyatua mabomu ya machozi nyumbani kwa Wenje, mkuu wa wilaya, Odunga alisema hatua hiyo ilitokana na taarifa za kuwepo kwa kikao kilichokuwa kikipanga kufanya vurugu ili kupinga matokeo na aliamuru kuagiza polisi kutawanya.
Hata hivyo, madai ya kuwepo kikao cha kupanga vurugu zilikanushwa na katibu wa Chadema wilayani Rorya, Jopasy Sanya kwamba Wenje pamoja na viongozi wa chama hicho na timu ya kampeni walikuwa kwenye kikao cha tathmini ya uchaguzi.
Kutokana tishio la usalama wa mali na maisha ya baadhi ya viongozi na makada wa CCM wilayani Rorya, Odunga alisema polisi imeimarisha ulinzi nyumbani na kwenye eneo la biashara ya kituo cha kuuza mafuta cha mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Charles Ochele ambaye pia ni diwani mteule wa Mkoma kulitokea vurugu.
Wanachama, viongozi wakamatwa
Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami na mwenzake wa Kanda ya Victoria, Zakaria Obadia walisema hadi jana viongozi, makada na wanachama wa chama hicho zaidi ya 40 walikuwa wakishikiliwa na polisi katika mikoa sita inayounda kanda hizo.
Mnyawami alisema wanaoshikiliwa Kanda ya Serengeti ni makada 29 katika wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, Shinyanga na Simiyu huku Obadia akisema wengine 20 wa Geita na Kagera wanashikiliwa kwa madai ya kushiriki vurugu za uchaguzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba alisema hadi jana alikuwa akiwashikilia watu watano akiwamo aliyekuwa mgombea ubunge wa Shinyanga Mjini, Salome Makamba wote wakituhumiwa katika jaribio la kuchoma nyumba ya mbunge mteule wa jimbo hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alisema jeshi hilo linawashikilia watu 50 wanaodaiwa kufanya vurugu katika uchaguzi licha ya kuwa wengine walianza kuwekewa dhamana.
Kyando alisema baadhi walifanya fujo kwa kupinga matokeo na wengine walichoma matairi barabarani walipokuwa wakishangilia ushindi.
Wakati hayo yakijiri katika mikoa hiyo, Arusha zaidi ya watu 20 wanashikiliwa na polisi katika majimbo ya Arusha, Arumeru, Ngorongoro na Moduli kwa tuhuma za kujihusisha na vurugu mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu.
Kamanda wa polisi wa mkoa, Salum Hamduni alithibitisha kushikiliwa kwa watu hao akisema ni “kutokana na kufanya vurugu katika uchaguzi”.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Reginald Masawe alisema chama hicho kinaendelea kukusanya takwimu na hadi jana mchana wanachama takribani 30 walikuwa wakishikiliwa.
Chama cha ACT-Wazalendo, kimesema hali ya mjumbe wa kamati kuu ya chama ya hicho, Ismail Jussa inaendelea vizuri.
Jussa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Al Rahma.
Zanzibar
Kati ya watu waliokamatwa na polisi katika Uchaguzi Mkuu, yumo naibu katibu mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui ambaye kwa siku tatu mfululizo viongozi wenzake walikuwa wakimtafuta baada ya kudaiwa kuchukuliwa katika mazingira ya kutatanisha.
Jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohammed Haji Hassan alikiri polisi kumshikilia Mazrui na wenzake 32 aliosema walikamatwa Oktoba 28 saa sita usiku wakiwa na vifaa vinavyoashiria kuingilia mfumo wa matokeo ya uchaguzi.
Kamanda wa Mkoa wa Pemba Kaskazini, Juma Sadi Hamisi alisema katika mkoa wake kuna watu ambao wamewakamata na wanakamilisha upelelezi ili kesho wawapeleke mahakamani.
Kamanda wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Makarani alisema Oktoba 27 na 28 waliwakamata watu kadhaa ambao wameendelea kuwahoji na wengi wameachiwa.
Imeandikwa na Bakari Kiango (Dar), Anthony Mayunga (Mara), Peter Saramba (Mwanza), Habel Chidawali (Dodoma) na Kalunde Jamal (Zanzibar)