Moto wa korosho wawaka upya bungeni
Dodoma. Sakata la korosho limewasha moto kwa mara nyingine bungeni huku wabunge watatu wakiikalia kooni Serikali na kuitaka kutoa majibu yatakayowaridhisha juu ya mchakato mzima wa uuzwaji wa zao hilo nchini.
Wabunge hao walisema hayo jana wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha 2019/2020.
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alianza kwa kuchangia hoja juu ya zao hilo akiwataka waliohusika kulihujumu wawajibike wenyewe na wasipofanya hivyo, atapeleka bungeni kusudio la kuwataja mmojammoja.
Nape alisema Rais John Magufuli alikuwa na nia njema lakini waliokwenda kutekeleza mchakato mzima wa ununuzi walikwenda kuua zao hilo. “Bahati mbaya zoezi lilikuwa na dhuluma, lilikuwa na rushwa lilikumbwa na ubabaishaji mwingi na uongo mwingi sana,” alisema waziri huyo wa zamani wa habari.
Alisema wapo wakulima ambao korosho zao zilichukuliwa, lakini hadi jana walikuwa hawajalipwa fedha zao na akaitaka Serikali kupeleka bungeni Sheria ya Korosho ili waipitie upya.
Katibu huyo wa zamani wa itikadi na uenezi wa CCM, pia alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akague na kupeleka ripoti bungeni jinsi kazi hiyo ilivyofanyika huku akidai iligubikwa na rushwa.
“Kama nilivyosema, Rais alikuwa na nia njema, lakini wengi wamemdanganya. Sasa ni vizuri wawajibike na mheshimiwa Spika ni vizuri tukawa specific. Si sahihi kuiingiza Serikali katika mambo yaliyofanyika ovyo,” alisisitiza Nape.
Nape hakuwa pekee yake katika mchango huo wa korosho ambao umekuwa ukijadiliwa bungeni karibu kila mara katika miezi ya karibuni.
John Mnyika (Chadema-Kibamba), alimwomba Rais kuvunja Baraza la Mawaziri kwa kile alichodai wamemshauri vibaya kwenye sakata hilo la korosho.
“Baraza la Mawaziri linatakiwa kuwajibishwa kwa kumshauri vibaya Rais Magufuli katika suala la korosho, kwa sasa korosho inaoza kutokana na kukosekana kwa wanunuzi,” alisema Mnyika.
Wakati Mnyika akisema hivyo, Joseph Selasini (Rombo-Chadema) alisema Spika Job Ndugai atakumbukwa kwa kuunda kamati iliyochunguza fujo zilizotokana na gesi mikoa ya Kusini na kamati iliyochunguza Tanzanite na Almasi.
“Nimeitazama picha ya Rais akiwa ameshika paji la uso anaonyesha kutafakari sana. Picha inamuonyesha kuzeeka kuliko alipoapishwa.
“Inaonekana Rais ana mawazo mengi. Kazi ya Bunge hili ni kuishauri Serikali. Kazi ya Bunge hili ni kuisimamia Serikali tunafanya makosa makubwa sana kufanya siasa ndani ya Bunge hili,” alisema Selasini.
Alisema yeye ni msafirishaji wa korosho kwa miaka mingi na kwamba, korosho inaoza kama vitunguu na iwapo majimaji yake yakigusa korosho nyingine nayo inaoza.
“Nimetangulia kukusifu Mheshimiwa Spika kama kuna ubishi wa korosho zimeoza ama hazijaoza, tengeneza kamati ya watu wachache waende wakague kwenye maghala. Nataka nikwambie kuwa korosho imeoza kwa asilimia 30,” alisema Selasini.
Alitoa mfano wa viongozi walivyojiuzulu wakati wa sakata la Richmond (kampuni ya kufua umeme) baada ya kuonekana kampuni hiyo haina uwezo wa kuzalisha umeme.
“Hoja ya Mheshimiwa Mnyika hakuna sababu ya taarifa ya mwongozo, tuna haja ya kuangalia tulipokosea. Sakata la korosho litadumu kizazi hadi kizazi, maghala yamejaa, karibu msimu unaanza, wakulima wanadai. Kwa hiyo kutakuwa na mfululizo wa hasara,” alisema.
Alisema hoja hiyo itakwenda kuwa kashfa kama Epa, Escrow na Richmond na kwamba, anaungana na wanaotaka CAG aende kukagua.