Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Mswahili’ ni nani? Wasikilize Wataalam

Katibu Mkuu wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (Chalufakita), Athumani Salum (wa kwanza kushoto) akizungumzia tafsiri ya neno Mswahili. Picha na Saada Amir

Muktasari:

Novemba, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu , Sayansi na Utamaduni (Unesco) lilitangaza rasmi Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani na kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.

Mwanza. Mswahili ni nani? Hili ni swali linaloulizwa mara kwa mara katika mazungumzo au mijadala mbalimbali, lengo likiwa ni kupata maana au tafsiri sahihi ya neno hilo.

Wapo wanaosema ‘Mswahili’ ni mtu anayeishi maeneo ya mwambao wa pwani. Wengine wanasema Mswahili ni mtu anayezungumza lugha ya Kiswahili.

Kwa baadhi ya watu, Mswahili ni mtu anayetenda kinyume cha makubaliano; yaani mtu asiyetunza ahadi.

Lakini kwa wataalam wa lugha ya Kiswahili, Mswahili ni ni zaidi ya kuishi maeneo ya mwambao wala kuzungumza lugha ya Kiswahili.

“Mswahili ni mtu ambaye anafanya mambo ya Kiswahili, anazungumza Kiswahili na mambo yafananayo na uswahili,” anasema Flora Mallema, Mwenezi wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (Chalufakita)

Akizungumza na Mwananchi jijini Mwanza leo Jumatatu Agosti 7, 2023, Flora anasema Waswahili wanaunganishwa kwa lugha, mila, desturi na tamaduni za kistaarabu.

‘’Uswahili ni zaidi ya maeneo ya kuishi wala lugha; Uswahili ni ustaarabu katika nyanja na maeneo yote,’’ anasema Mwenzi huyo wa Chalufakita

Mwenyekiti wa Chalufakita, Dk Mussa Hans amasema Mswahili ni mtu anayefahahamu na kutumia lugha ya Kiswahili kidiplomasia, hasa inapofikia suala la kupatanisha watu penye mifarakano.

“Pale watu wakiwa wanagombana anatafutwa Mswahili kuwapatanisha,” anasema Dk Mussa

Anasema kuhusisha Uswahili na mambo yasiyotahili ni dhana potofu huku akifichua kuwa tafiti zinaendelea kuhusu namna ya kukabiliana na dhana potofu ya ‘Mswahili’ ni nani.

“Kiswahili kinanasibishwa na utamaduni na lugha, kwa hiyo, hizo dhana potofu hazipo kwa mswahili pekee, bali zipo kila mahali ikiwemo kwenye asili ya watu,’’ anasema

Dk Mussa anasema neno Mswahili lina asili ya Kiarabu na lilitokana na wageni wa Kiarabu waliofika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi ambao waliwaita wenyeji Waswahili.

“Waarabu walipofika maeneo ya Pwani waliwakuta wenyeji na kuwaita ‘Sahili’ wakimaanisha watu wa Pwani” anasema Dk Mussa

Kuhusu upotoshaji wa neno ‘Mswahili’ mtaalam huyo wa lugha ya Kiswahili anasema; “Neno Mswahili hupotoshwa kulingana na matakwa na malengo ya watu na huimarishwa kwa kuegemea matumizi ya lugha ya Kiswahili,’’

Katibu Mkuu Chalufakita, Athumani Salum anasema tofauti na Waswahili wenyewe, jamii ya watu walio nje ya nchi (Wageni) wanathamini zaidi lugha ya Kiswahili kwa kuipa kipaumbele kwa sababu ndio lugha pekee ya Kiafrika inayounganisha Waafrika na iliyopewa hadhi kuwa na siku maalumu ya kuisheherekea.

“Unakuta mtu anasema huyu usimsikilize sana huyu ni Mswahili Mswahili akimaanisha ni mtu asiyeaminika, asiye muungwana wala kusimamia maneno na kauli zake,” anasema Athumani

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Chalufakita anasema wakati mwingine, ndani ya matumizi hayo yenye muelekeo hasi kuna mitazamo chanya ikionyesha kuwa Mswahili ni mtu mwenye ufundi wa kutumia lugha ya Kiswahili.

Anaishauri jamii, hasa ya Waswahili wanaozungumza lugha ya Kiswahili, waliostaarabika na ambao maisha, mila, desturi na tamaduni zao zinaakisi Uswahili kuondokana na dhana potofu inayofifisha na kudunisha hadhi ya Mswahili kwa kuchukua tafsiri yenye uelekeo na upande chanya.

“Ni jukumu na wajibu wetu sote siyo tu kuutetea, bali pia kujivunia Uswahili wetu unaojengwa kwenye misingi imara ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili ambayo ni moja ya lugha zinazotambulika na kupewa hadhi maalum duniani kwa kutengewa siku ya kuadhimishwa,’’ anasema Athumani