Kiswahili bila Kiingereza ni kazi bure

Kwanza niweke bayana kuwa mimi ni Mswahili halisi. Najivunia fika lugha yangu hii adhimu, japo najua maudhui ya makala haya yanaweza kuwaudhi walio wengi.

Tuvumiliane, ndivyo usomi ulivyo.Chambilecho Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kuwa hoja haipigwi rungu.

Twende katika mada. Leo hii Kiswahili kila uchao na uchwao kinazidi kuchanja mbuga. Tunaambiwa kuwa kimeshatambuliwa kama lugha rasmi katika jumuiya za kimataifa na za kikanda kama vile Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki, Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika na Umoja wa Afrika.

Katika ngazi ya nchi mojamoja, achilia mbali uwepo wa vyuo vikuu tele Afrika, Amerika na Asia vinavyofundisha kozi za Kiswahili, lugha hiyo kwa sasa ina msukumo mkubwa katika mifumo ya elimu katika nchi kadhaa barani Afrika.

Ni hivi karibuni tu Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tchisekedi alipopigilia msumari kwa kulisihi Shirika la Umoja wa Mataaifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), kuzidi kukienzi Kiswahili.

Kama haitoshi, Kiswahili sasa kinaadhimishwa rasmi na Umoja wa Mataifa kila ifikapo Julai 7. Ni siku maalumu ambayo wataalamu wetu wameamua kuipa jina la ‘Masikidu’.

Haya yote nimeyataja, lengo langu ni kutaka kusema kuwa hivi sasa Kiswahili ni lulu duniani. Ni lugha yenye fursa chekwa na bidhaa yenye thamani sokoni.

Hata hivyo, msomaj unaweza kujiuliza hizo fursa zi-wapi? Kwa uchache nikudokezee; Mosi, unaweza kuwa mwalimu wa lugha hiyo katika ngazi mbalimbali za elimu. Pia unaweza kufundisha wageni hapahapa nchini au kwa kutumia mtandao.

Pili, kuna fursa ya ukalimani na tafsiri hasa kwa kutambua kuwa kuna watu na taasisi kama tulivyoona hapo awali ambazo zinahitaji huduma ya Kiswahili.

Tatu, kwa walio na ujuzi wa uandishi, wana fursa ya kuandaa matini na machapisho mbalimbali kwa kutumia Kiswahili. Nimetaja fursa chache, zitoshe.

Hata hivyo, niseme na hapa naomba kusisitiza kuwa fursa zote hizi ni kazi bure kama mtafutaji wa fursa hizo atazipa kisogo lugha nyngine za kigeni hasa Kiingereza, ndio maana nashadadia kuwa bila Kiingereza hakuna Kiswahili!

Watanzania tusijidanganye kuwa kwa kusoma tu fasihi za kina Shaban Robert, Penina Penina Mlama, Mugyabuso Mulokozi na magwiji wengine; au kwa kusoma ngeli, kiima na kiarifu, basi tushazitia kibindoni fursa za Kiswahili. Tunahitaji kujiongeza kwa kujifunza lugha nyingine za kimataifa.

Hivi kwa mfano, unawezaje kwenda kufundisha Kiswahili huko Marekani kama hujui Kiingereza? Ukienda China au Uarabuni, utahitajika kuwa na maarifa ya kutosha ya Kichina na Kiarabu mtawalia, ili kazi yako ya ufundishaji iwe na tija.Kiswahili kikavu hakitakutoa.

Ukalimani ndio kabisa, mhusika atalazimiku kuwa mlumbi wa zaidi ya lugha moja. Wageni tunaowafundisha hapa nchini au wale tunaowaandikia kupitia mitandao, tunalazimika kujua lugha za kimataifa ili kuwasiliana nao.

Na Kiingereza ndio mwafaka zaidi kwa kuwa ndio lugha inayounganisha mataifa mengi. Mtaalamu wa Kiswahili anayepigwa chenga na Kimombo anakosa mengi.

Tusidanganyane! Tuwaeleze watoto wetu kuwa hata kama wanasoma Kiswahili vyuoni, ‘wakomae’ na lugha za kigeni hasa Kiingereza.
Kwangu na kwa hali ilivyo duniani, hizi ni kama lugha pacha. Kujifanya farisi wa ndaki, sanidi, kisakuzi, ukawa mweupe wa ‘is’ na ‘was’, ni kujitanibu na fursa zilizopo duniani.

Leo tunalalamika kuwa majirani zetu ndio waliojaa duniani wakitamba na Kiswahili. Siri ni mbili tu; moja wana uthubutu, sio sisi lelemama wa maisha na wapiga porojo.

Pili, wenzetu wanabebwa na Kiingereza, ndio maana licha ya ukweli kuwa Kiswahili chao ni cha kimachugwachugwa, ndio waliotamalaki katika soko la kimataifa.

Nihitimishe kwa kusema mkakati wowote wa kuimarisha Kiswahili, lazima uende sambamba na uimarishaji wa lugha nyingine za kimataifa hususan Kiingereza.

Hata sasa tunapokipigia chapuo Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia, jambo ninaloliafiki kwa asilimia mia na ushei, tutashangaza sana kama Kiingereza tutakipiga teke.

Tukiimarishe Kiswahili ili kiwe na sifa ya kufundishia, lakini wakati huohuo tuweke mazingira wezeshi ya Kiingereza kufahamika kimawasiliano zaidi badala ya mfumo wa sasa ambao lugha hiyo inaonekana kama lugha ya kitaaluma.

Matunda ya fursa za Kiswahili yataonekana na kuchangamkiwa kwa kuwa na Watanzania wajuzi wa Kiswahili na wenye ufahamu usio na shaka wa kuwasiliana kwa lugha ya Kiingereza, ambayo tutake tusitake, ndiyo kiswahili cha dunia!

Hata wataalamu wetu wa Bakita wanakula mema ya nchi, kwa sababu walijiongeza kwa kujua lugha mbalimbali.