Mtanzania mwingine auawa mapigano ya Israel, Hamas
Muktasari:
- Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Joshua alitekwa na Hamas, familia kupelekwa Israel kwa hatua zaidi
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema Mtanzania mwingine amefariki dunia katika mapigano yanayoendelea kati ya Isarel na kundi la Hamas.
Amesema Mtanzania huyo aliyepoteza mawasiliano na ubalozi wa Tanzania nchini Israel, amebainika kuuawa Oktoba 7, 2023.
Mtanzania huyo, Joshua Mollel, alikuwa masomoni Israel pamoja na wenzake. Alitoweka pamoja na Clemence Mtenga, ambaye pia ilibainika kufariki dunia.
Mwili wa Mtenga (22), uliwasili nchini Novemba 27, 2023 na maziko yalifanyika Novemba 28, mwaka huu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
Waziri Makamba katika taarifa aliyoitoa leo Desemba 14, 2023 saa 3.42 asubuhi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amesema Serikali imejulishwa na Serikali ya Israel kuwa Mollel (21) aliuawa baada ya kutekwa na kundi la Hamas Oktoba 7,2023.
“Nimeongea na mzee Mollel, baba mzazi wa Joshua, kuhusu ujumbe huo wa Serikali ya Israel. Tunaendelea na mpango wa awali wa kuwapeleka mzee Mollel na mwanafamilia mwingine pamoja na ofisa wa Serikali nchini Israel kuungana na Balozi wetu na maofisa waliopo huko, kukutana na kuzungumza na mamlaka za nchi hiyo ili kupata taarifa za ziada,” ameandika Waziri Makamba.
“Kwa ridhaa ya familia, itakapobidi, tutatoa taarifa za ziada katika siku zijazo.”
Mtenga na Mollel walipoteza mawasiliano na ubalozi wa Tanzania nchini Israel tangu Oktoba 7,2023 baada ya kundi la Hamas kuwateka mamia ya watu.
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na ya Israel ilianza juhudi za kuwatafuta vijana hao ambao ni miongoni mwa wanafunzi 260 waliokuwa masomoni nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili Oktoba, mwaka huu, Loitu Mollel, ambaye ni baba mzazi wa Joshua alisema mara ya mwisho kuzungumza na mwanaye ilikuwa Oktoba 5, 2023.
Mollel alisema Joshua alikwenda Israel Septemba mwaka huu, kujifunza masomo ya kilimo kupitia programu maalumu iliyoratibiwa na Serikali.
Kabla ya kuchaguliwa kwenda kwenye programu hiyo, Joshua alikuwa mwanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo ya Katrin iliyopo Ifakara, mkoani Morogoro.
Mollel alisema mtoto wake alikwenda Israel Septemba 18, mwaka huu, hivyo hadi ghasia zilipoanza alikuwa na mwezi mmoja nchini humo.
Oktoba 18, 2023 Watanzania tisa walirejea nchini zikiwa siku nne tangu Serikali ilipowataka wajiandikishe ubalozini ili warejee nyumbani kutokana na mapigano yanayoendelea nchini Isarel.