Muwsa yamaliza kero ya maji, Mbunge akisema ndoa zitapona Moshi
Wajumbe wa kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi, Moshi vijijini,wakifungulia maji wakati walipotembelea kukagua mradi wa maji wa Miwaleni-Njiapanda ambapo umekamilika kwa asilimia 100. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Mradi huo ambao umegharimu Sh2.378 bilioni hadi kukamilika, umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) kwa fedha kutoka serikalini na utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100 na zaidi ya wananchi 13,734, wamefikiwa na huduma.
Moshi. Zaidi ya wananchi 13,734 wa Kata ya Njiapanda na maeneo jirani, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama, baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Miwaleni-Njiapanda.
Hatua hiyo imeelezwa kwamba itasaidia ndoa nyingi upande wa kina mama kutoingia migogoro kwa sababu awali walikuwa wanatumia muda mwingi kutafuta maji.
Mradi huo ambao umegharimu Sh2.378 bilioni hadi kukamilika, umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) kwa fedha kutoka serikalini na utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wameanza kupata huduma.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 16, 2023 na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Muwsa, Innocent Lugodisha wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya siasa ya Wilaya ya Moshi Vijijini, walipofika kuanguka maendeleo ya mradi huo ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa utekekezaji wa ilani ya chama hicho.
Amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha Mita za ujazo 2,592 kwa siku na kukamilika kwake kumeboresha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya Kata ya Njiapanda na maeneo jirani ikiwemo Miwaleni na Mabungo.
Amesema kabla ya kukamilika kwa mradi huo, upatikanani wa maji Kata ya Njiapanda ulikuwa ni mita za ujazo 770 kwa siku, huku mahitaji yakiwa ni mita za ujazo 1,190 kwa siku hivyo kukamilika kwa mradi huo, kumemaliza kabisa mgao wa maji uliokuwa ukiwakabili wananchi wa maeneo hayo.
"Kukamilika kwa mradi huu ni ukombozi kwa wananchi wa Kata ya Njiapanda, maana kwa sasa wanapata maji kwa saa 24 na kimsingi mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wamefikiwa na huduma hii muhimu," amesema.
Akizungumza Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Maleko ameipongeza Muwsa kwa kukamilisha mradi huo wa maji na kueleza kuwa kwa sasa wananchi wataweza kutumia muda mwingi kufanya shughuli za kimaendeleo tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo waliteseka kusaka huduma ya maji.
"Tumeona kwa vitendo hapa Njiapanda mkimtua mama ndoo kichwani, niipongeze serikali, maana kina mama walikuwa wakiteseka na ndoa zimekuwa zikivunjika kwa suala la maji, serikali imeonyesha ni namna gani inatujali kina mama kwani familia ikiwa na maji ya kutosha mama hapotezi muda kwenda mitaani kutafuta maji," amesema.
"Lakini pia niwapongeze sana Muwsa, kwani katika miradi yote ambayo kamati ya siasa tumeshaitembelea leo, huu ndiyo mradi ambao tumeukuta hauna dosari, hii ni kazi nzuri, tuombe muendelee kufanya kazi nzuri katika kuletea wananchi huduma na kufikia malengo ya kumtua mama ndoo kichwani"
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi vijijini Siril Mushi amepongeza mradi huo na kueleza kuwa kamati ya siasa imeridhishwa nao kwa kuwa hakuna dosari waliyoiona ambapo pia amewataka wananchi kuutunza ili kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
"Mradi nimeupenda kwa sababu umemtua mama ndoo kichwani kama ilivyo malengo ya serikali, mradi huu ni wa kuigwa sasa niombe mradi utunzwe na miundombinu yake yote, ili udumu na kunufaisha hata vizazi vijavyo".
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori amesema mradi huo wa maji umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kama ilivyokusudiwa na serikali.
"Niombe miradi yote inayotekelezwa katika wilaya ya Moshi itekekezwe kikamilifu, tukija kuikagua iwe ni kicheko, serikali ikishatoa fedha, watendaji tufanye upande wetu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kama ilivyopangwa ili kazi iendelee"