Mwandishi Zephania Ubwani afariki dunia

Zephania Ubwani

Muktasari:

  • Taarifa zinasema Ubwani amefariki dunia wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Arusha. Mwandishi mkongwe wa habari nchini, aliyekuwa akiandikia Gazeti la The Citizen linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Arusha, Zephania Ubwani amefariki dunia leo mchana baada ya kuugua ghafla wakati akiwa katika majukumu ya kikazi katika Hoteli ya Kibo Pallace jijini humo.

Taarifa zilizopatikana kutoka Arusha zinasema Ubwani wakati anamfanyia mahojiano mmoja wa watoa habari wake ndani ya hoteli hiyo, alijisikia vibaya na alipatiwa msaada wa kupelekwa Hospitali ya AICC iliyopo jirani na hoteli hiyo lakini alifariki dunia wakati anachunguzwa kilichokuwa kikimsumbua.

Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV Arusha, Asraji Mvungi aliyekuwa naye wakati akifanya mahojiano hayo, amesema tatizo la kiafya lilianza kumtokea saa 8 mchana leo wakati wanamfanyia mahojiano mkurugenzi mkuu wa Costech.

“Mimi nilimaliza Interview yangu kwa hiyo naye akaanza ya kwake, lakini mimi sikuondoka nikawa hapo hapo sasa katikati ya interview (mahojiano) ghafla akakaa chini nilipomwangalia nikaona anatokwa na jasho jingi sana,”amesema Mvungi.

“Yaani ni ghafla tu, akakaa chini baada ya sekunde moja au mbili akalala chini. Nikamfungua koti alilokuwa amevaa na mkanda. Hapo akajinyoosha hakusema chochote nikachukua koti langu nikampepea lakini hali haikubadilika.”

Kwa mujibu wa Mvungi, hapo ndipo walipofanya utaratibu wa haraka wa kumpeleka Hospitali ya AICC ambayo ni hatua kama 15 kutoka Hoteli ya Kibo Pallace na walipomfikisha yeye aliondoka baada ya madaktari kuwataka wabaki nje.

“Sasa nikiwa huko kwenye kazi zangu ndio napigiwa simu kuwa kumbe amefariki. Kwa kweli ni tukio linanisumbua sana kwa sababu katika hayo mahojiano nilikuwa mimi tu na Ubwani. Ni msiba mzito sana na kwa kweli alikuwa mtu muhimu sana kwangu,” amesema.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Arusha (APC), Claud Gwandu amesema taarifa alizonazo ni kuwa Ubwani alikuwa na matatizo ya moyo na kwamba madaktari wamemweleza mwandishi huyo alipata shambulio la moyo lililosababisha umauti kumkuta.

“Amendoka nyumbani asubuhi akiwa na afya njema na kuelekea kwenye majukumu yake hapo Kibo Pallace Hotel. Sasa wakati anafanya mahojiano alijisikia vibaya na kuanza kutokwa na jasho wakamkimbiza AICC ndio hivyo ametutoka,”amesema Gwandu.

Mmoja kati ya waandishi ambao walifanya kazi na mzee Ubwani, Philbert Rweyemamu amesema amepokea taarifa za msiba huo kwa mshtuko mkubwa kwa sababu aliamka asubuhi akiwa mzima lakini ilipofika kati ya saa 8 na saa 9 mchana hali ilibadilika.

“Kwa hiyo alivyojisikia vibaya alipata msaada akakimbizwa AICC Hospitali kwa ajili ya kupata msaada wa haraka ndio wakati anafanyiwa vipimo daktari aka-declare (akatamka) kuwa ameshafariki. Ni msiba mzito na unaoshtua,” amesema Rweyemamu.

“Nimefanya naye kazi kwa miaka 10 nikiwa Mwananchi Communications Limited tangu 2010 mpaka 2021 kwa kweli ni mwalimu wangu na alikuwa mtu mwema sana,” amesema.

Mwakilishi wa mauzo wa MCL Kanda ya Kaskazini, Ewald John amesema yeye alitumiana naye ujumbe mfupi (SMS) wakiwa wanachati usiku wa juzi hadi mchezo wa Yanga na Mamelodi Sundowns ulipomalizika.

“Sasa leo ninaambiwa amekufa. Ni masikitiko makubwa,” amesema.