Mwanzo wa kampeni Uchaguzi Mkuu 1975

Baada ya Oktoba 30, 1970, ilipita miaka mingine mitano hadi ulipofanyika uchaguzi mkuu mwingine Oktoba 26, 1975. Kama ilivyokuwa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1970, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mgombea pekee wa Tanu na aliibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Maandalizi ya uchaguzi huo yalianza Jumatatu ya Juni 22, 1975, siku ambayo mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Erasto Mang’enya alitangaza tarehe ya kupiga kura.

Mang’enya aliwaambia waandishi wa habari kuwa uandikishaji wa wapiga kura ungeanza Julai 8 na kumalizika Agosti 7. Ilitarajiwa kuwa wapigakura wapatao milioni 6 wangeandikishwa katika uchaguzi huo, ikilinganishwa na wapigakura milioni 4.85 walioshiriki uchaguzi wa mwaka 1970.

Mang’enya aliwaambia waandishi kuwa ingawa uandikishaji ulifanyika mwaka 1970, ilibidi ufanyike tena mwaka huo kwa sababu wilaya za Tanu zilikuwa zimebadilika kuwa wilaya za uchaguzi na kwamba, makazi ya wapigakura nayo yalikuwa yamebadilika kutokana na wananchi wengi kuhamia katika vijiji vya ujamaa vilivyokuwa maeneo mapya.

Muda wa kampeni za wagombea ubunge uliongezwa kutoka wiki mbili hadi tatu ili kuwapa nafasi zaidi wagombea kujieleza kwa wananchi.

Jumanne ya Julai 22, 1975, msemaji wa Tume ya Uchaguzi, William Maina alisema mikutano ya mwaka ya wilaya za Tanu ambayo ingetambua majina ya wagombea wa ubunge ingefanyika Agosti 18 ya mwaka huo katika majimbo yote ya uchaguzi.

Maina, ambaye pia alikuwa Katibu wa Bunge, alisema ofisi yake imeshapeleka maagizo hayo kwa wasimamizi wa uchaguzi na kwamba mikutano ya halmashauri za maendeleo za mikoa nayo ingefanyika Agosti 14 ili kujadili majina ya wagombea.

Uteuzi wa mwanzo kwa wagombea ubunge kwa majimbo yote pamoja na wagombea ubunge wa mkoa, ulifanyika Agosti 11, 1975 na siku iliyofuata ilikuwa ni ya mwisho kwa wenye malalamiko.

Agosti 4, katibu mtendaji wa Tanu, John Mhaville alitangaza kuwa wagombea ubunge wote katika majimbo watapewa maelekezo maalumu ya chama ambayo ndiyo watayatumia katika kampeni zao.

Vuguvugu la uchaguzi huo lilianza kuonekana rasmi Agosti 11 wakati wagombea walipoanza kuwasilisha fomu zao za uteuzi wa mwanzo kwa wasimamizi wa uchaguzi kabla ya saa 10:00 jioni katika majimbo yote ya uchaguzi. Wengi walijitokeza kugombea ubunge kuliko uchaguzi wa 1970.

Hata hivyo, Jumatatu ya Agosti 11, mmoja wa wagombea wa mwanzo kabisa kuthibitishwa kwamba hana mpinzani alikuwa Joseph Mungai, ambaye alikuwa waziri wa kilimo. Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Job Lusinde, aliondoa jina lake katika orodha ya wagombea wa jimbo la Dodoma.

Waziri Mkuu Rashidi Kawawa, ambaye alikuwa mgombea wa ubunge wa Liwale, pamoja na mawaziri wengine wawili wadogo hawakuwa na upinzani katika majimbo yao. Mawaziri hao ni Isael Elinawinga, Waziri wa Maji na Nguvu za Umeme, na Mungai.

Waziri wa Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Wilbert Chagula; Waziri wa Ustawishaji wa Makao Makuu, Adam Sapi Mkwawa na Waziri wa Fedha, David Msuya, hawakuwahi kugombea viti vya ubunge katika uchaguzi wowote uliopita na wala hawakugombea katika uchaguzi huo wa mwaka 1975.

Majina yote ya wagombea yaliyopokewa na ofisi ya Bunge na yalijadiliwa kwenye vikao mbalimbali vya chama.

Vikao hivyo ni kamati za utendaji za wilaya, mkutano mkuu wa wilaya, kamati kuu na mwisho kabisa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo ndiyo iliyokuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu majina ya watu wawili waliogombea viti katika kila jimbo la uchaguzi.

Majina ya wale waliotaka kugombea viti vya ubunge vya mikoa yalijadiliwa kwanza na halmashauri za maendeleo za mikoa kabla ya kupelekwa mbele ya vikao vya juu vya chama.

Wakati maandalizi ya uchaguzi yakiendelea katibu wa Tanu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Joseph Rwegasira, Oktoba Mosi, 1975 alitahadharisha kwamba kuna baadhi ya viongozi wa klabu ya mpira ya Yanga ya Dar es Salaam waliokuwa wanatumia mgogoro wa uongozi katika klabu hiyo kwa madhumuni ya kisiasa ya kuchafua uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Alisema katibu mwenezi wa klabu hiyo, Abdul Masoudi alikuwa akitumiwa katika mipango hii bila ya kujua kwamba ilikuwa hatari.

Rwegasira alisema wanachama wa Yanga, ambao alisema ni wanachama safi wa Tanu kama walivyokuwa wanachama wa klabu nyingine za michezo, walikuwa wakitumiwa na viongozi hao wachache ili waipinge Tanu.

Alionya kuwa Tanu na Serikali haviwezi kukaa kimya kuwaangalia watu wachache wakitumia mbinu za kupinga chama kwa kutumia vikundi vya michezo.

kwa upande mwingine, wagombea walitakiwa kufafanua maelezo yaliyokuwa katika Ilani ya Uchaguzi yenye uhusiano na mazingira ya wilaya zao badala ya kukariri maelezo yote.

Makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Pius Msekwa alisema wagiombea walitakiwa kutumia ibara za ilani ya uchaguzi zinazohusiana na maeneo yao, kuelezea wakati wa kampeni zao zilizoanza Oktoba 2.

Kwa wakati wote wa kampeni, lilitolewa onyo kuwa magari yote ya Serikali yapigwe marufuku kwenda vijijini kwa hofu kwamba viongozi wa Tanu na Serikali wangejiingiza katika shughuli za kampeni ya uchaguzi huo.

Onyo hilo lilitolewa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Tanu, Thomas Mussa mwishoni mwa mkutano wa kamati ya utendaji ya Tanu wilayani Dodoma.

Hata hivyo, wakati kampeni hizo zikiendelea, viliibuka vikundi mbalimbali vya ngoma, bendi, majumba ya sinema na madhehebu ya dini mkoani Dar es Salaam kushiriki wa kutumika katika kampeni ya uchaguzi wa Rais.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa Tanu mkoani Dar es Salaam uliofanyika makao makuu ya mkoa.

Mkutano huo ulifunguliwa na kuendeshwa na katibu mkuu wa umoja huo, C. Liundi.

Katika uchaguzi huo kulikuwa na viti 96 vya ubunge wa kuchaguliwa, wabunge 15 wanaowakilisha taasisi za kitaifa, wabunge 20 wa Taifa wanaowakilisha mikoa na waliochaguliwa na Bungena 62 walioteuliwa na Rais.

Pia walikuwepo 32 kutoka Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, wananchi 20 wenye sifa kutoka Zanzibar na wengine 10 raia wa Jamhuri ya Muungano). Walikuwepo wengine 20 ambao ni makatibu wa mikoa, wakuu watano wa mikoa ya Zanzibar.

Kesho tutaangazia mazingira ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1975 ulivyofanyika na washindi walivyopatikana.