Kituo cha uwekezaji kuzinduliwa Arusha, Julai

Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza jijini Arusha leo Aprili 30, 2024 katika kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya utalii katika Mkoa wa Arusha lililokutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Muktasari:

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliomba kuwepo kwa kituo hicho ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wawekezaji wa ndani na nje

Arusha. Serikali inatarajia kuzindua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Mkoa wa Arusha kufikia Julai Mosi, 2024 ili kuondoa urasimu wanaokumbana nao wawekezaji.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Apili 30, 2024 jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumza kwenye kongamanao la uwekezaji kwenye sekta ya utalii katika Mkoa wa Arusha.

Kongamano hilo linaongozwa na kauli mbinu isemayo: “Uchangamkiaji wa fursa za uwekezaji baada ya programu ya Tanzania – The Royal Tour.”

Hatua hiyo inakuja kufuatia ombi la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati akizungumza kwenye kongamano hilo.

Akijibu ombi hilo, Profesa Kitila amesema suala hilo liko ndani ya uwezo wake na kumwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwa Julai Mosi, 2024 atakuja mkoani hapa kuzindua kituo hicho.

“Hili la TIC liko ndani ya uwezo wangu, kwa hivyo, Katibu Mkuu nikimaliza kikao cha bajeti Juni 30, tutakuja Arusha Julai Mosi ili tufungue kituo cha TIC hapa Arusha,” ameelekeza.

Kuhusu kongamano hilo, amesema ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeagiza kukuzwa kwa sekta ya uwekezaji hapa nchini ikiwemo katika sekta ya utalii.

Amesema sekta ya utalii ni mtambuka na ina mchango mkubwa katika pato la Taifa ambapo inachangia asilimia 25.

Amesema mchango wa sekta ya utalii katika bara la Afrika bado ni mdogo akitolea mfano mwaka 2019 kabla ya ugonjwa wa Uviko-19, mchango wa bara hilo katika duni bado ulikuwa ni asilimia 0.3.

“Tunatakiwa kupambana ili kuweza kukuza uchumi wetu zaidi lakini pia kusaidia kuongeza mchango wetu duniani kama bara la Afrika uweze kuongezeka na kuonekana,” amesema.

Profesa Kitila ametaja miongoni mwa masuala ambayo watalii huangalia ni pamoja na amani, utulivu na usalama, miundombinu, mikakati mizuri ya kutangaza vivutio vya utalii, uwepo wa miundombinu ya malazi, sera na sheria zinzovutia uwekezaji pamoja na mahusiano mema ya kimataifa.

“Kwenye suala la amani, utulivu na usalama, bado Tanzania tuko vizuri na tuendelee kuifanya Arusha kuwa jiji salama Tanzania lakini na Afrika kwa ujumla,” amesema Prof Mkumbo.

Awali, Makonda alimuomba Waziri Kitila ndani ya muda mfupi mkoa wa Arusha uwe na kituo cha pamoja cha uwekezaji ili kuweza kurahisisha utoaji wa huduma hiyo kwa wawekezaji

“Nikuombe, ndani ya muda mfupi tuwe na kituo cha pamoja cha uwekezaji, ili mwekezaji akija Arusha ndani ya siku moja anapata hati yake ya usajili, akishaweka taarifa zake kwenye mfumo unasoma kila idara na kila mtu anathibitisha na kuondoka na hati yake,” amesema Makonda.

Makonda amesema wameweka mikakati kuhakikisha mji wa Arusha unakua na taa na kamera kila mahali na kuwa shughuli ya kufungwa taa za barabarani inaendelea na kuomba uboreshwaji wa miundombinu hasa ya barabara ili kuvutia watalii zaidi.

Waziri  wa Maliasili na Utalii, Anjelah Kairuki, amesema fursa za uwekezaji zipo nyingi hasa katika mnyororo wa thamani wa utalii na kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje na kuweza kuvuka lengo la kuwa na watalii milioni tano ifikapo mwakani.

“Tuboreshe huduma katika mnyororo wa thamanai wa utalii. Kwa mfano, tukiangalia nchi nzima vyumba vya malazi ni  122,532 na Arusha vitanda 11,900 lakini vitanda vinavyotumika kote ni asilimia 56.7,”amesema.

Akizungumzia fursa za ushirikiano wa uwekezaji kati ya mashirika ya umma na sekta binafsi, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema ni muhimu wadau hao kuungana na kufanya uwekezaji wa pamoja kwenye sekta ya utalii ili kuendelea kukuza sekta hiyo hapa nchini.

“Tanzania sekta ya utalii ina naafsi kubwa na inafanya vizuri lakini bado hatujaitumia kwa ukamilifu wake na  tumeona juhudi za  Serikali katika kuiendeleza sekta hii. Kila mmoja atumie vizuri fursa ya uwekezaji katika sekta ya utalii na Arusha ndiyo kinara wetu na bendera yetu kwa utalii, taasisi zote ziboreshe huduma zake na kuchangamkoa fursa za uwekezaji,”amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amesema lengo la mkutano ni kujadiliana na wadau wa sekta hiyo kuhusu changamoto na fursa zilizopo, ikiwemo kuelimisha wadau wa utalii juu ya manufaa yaliyopo kwenye vivutio kupitia TIC na kumsaidia Mtanzania kuwekeza.

Amesema Watanzania wana fursa ya kuwekeza kwani vitu vingi vimesamehewa au kupunguziwa kodi na vitamwezesha Mtanzania kumiliki na kuwekeza katika sekta hiyo muhimu.

“Mtanzania mwenye ndoto ya kuanzisha mradi wake  hatakiwi kukwama ndiyo maana Serikali ilisema kuna kiwango kitatumika kumtambua nani ni mwekezaji, awali Mtanzania kwenye uwekezaji lazima alikuwa alipie Dola za Marekani  100,000  sasa hivi kimepunguzwa imekuwa Dola za Marekani 50,000, ila mgeni lazima aweze kuwekeza lazima awe na mtaji wa Dola za Marekani 500,000,” amesema.