NCC yaja na mkakati wa kuwa na sheria moja ya ujenzi

Mhandisi wa ujenzi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Geofrey Mwakasenga  akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  •  Wingi wa sheria zinazosimamia ujenzi umetajwa kusababisha usumbufu katika uendelezaji majengo na gharama zisizokuwa za lazima

Dodoma. Wingi wa sheria zinazosimamia sekta ya ujenzi umetajwa kukwaza ukuaji wa sekta hiyo iliyosababisha Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kuandaa andiko la dhana linalolenga kuondoa changamoto hiyo pamoja na nyinginezo.

Andiko hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano wa watumishi wa Serikali na sekta binafsi limeshakabidhiwa kwa Wizara ya Ujenzi.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Desembe 21, 2023 na Mhandisi Ujenzi NCC, Geofrey Mwakasenga ofisini kwake jijini Dodoma.

Amesema tangu kuanzishwa kwa baraza hilo mwaka 1979 na kuanza utekelezaji wa majukumu yake 1981, kumekuwa na mkanganyiko wa wingi wa sheria za usimamizi.

“Wizara iliona kuwepo na sheria ya majengo nchini, hivyo kuhakikisha inaanzishwa, kazi ya kuratibu na uandaaji wa sheria hiyo tayari andiko lipo Wizara ya Ujenzi,” amesema Mwakasenga.

Amesema changamoto hiyo iliweka msukumo kwa Serikali kuanza kuandaa mfumo bora wa kisheria wenye kanuni na miongozo inayojitosheleza utakaotumika katika usimamizi wa ujenzi wa majengo nchini.

Amesema baadhi ya sheria zinazosimamia ujenzi wa majengo nchini ni ile ya Mipango Miji, Sheria ya Afya ya Usalama Mahali pa Kazi, Zimamoto na Uokoaji, Sheria ya Mazingira, Sheria ya Kandarasi na Usajili na zile zinazosimamia taaluma na wanataaluma.

Ofisa Habari wa NCC, Eliezer Rweikiza amesema moja ya mikakati katika sheria hiyo itakuwa ni kuangalia namna ya kuwasaidia makandarasi wazawa katika kuwajengea uwezo ili waweze kutimiza vigezo kwenye miradi mikubwa ya ujenzi.

Rweikiza amesema taasisi hiyo imejizatiti kufanya kazi karibu na wananchi na wataalamu ili kumaliza upungufu ambao umekuwa ukijitokeza mara nyingi kwenye ujenzi.