Ni Mtikisiko

Sunday June 13 2021
mtikisiko pic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Tahadhari imetolewa kuwa sekta tatu zinazogusa watu wengi huenda zikatikiswa kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuanzisha na kupandisha kodi na kubadili utaratibu wa tozo kwenye maeneo hayo. Hayo ni miongoni mwa mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2021/22 iliyosomwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi, Dk Mwigulu Nchemba.

Serikali ilitoa mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka 2021/22, ambayo inatarajia kutumia Sh36.33 trilioni.

Hata hivyo, wachambuzi, wadau wa masuala ya uchumi na wananchi wameeleza kuwa hatua hizo za Serikali zinaweza kuwa mwiba kwa maisha ya kila siku ya watu na hasa wale wa kipato cha chini.

Maeneo ambayo yametajwa kupata maumivu ni pamoja na mawasiliano ya simu, kodi ya majengo na usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda.


Tozo za simu

Advertisement

Kwa kipindi kirefu watoa huduma za simu wamekuwa wakipaza sauti juu ya kodi kwenye sekta ya mawasiliano wakieleza kuwa, ndicho chanzo cha wao kupata faida kiduchu lakini pia suala la bei ya vifurushi hasa vya intaneti.

Katika eneo hilo kipengele cha bajeti kilichogusa watu wengi ni tozo mpya za simu Serikali inatarajia kukusanya Sh1.65 trilioni.

Siku kadhaa kabla ya kusomwa kwa bajeti Mtendaji Mkuu wa Vodacom, Hisham Hendi alizungumzia umuhimu wa Serikali kufanya mapitio ya sera na kodi ili kuhakikisha kunakuwa na ukuaji wa uwekezaji nchini na kuvutia uwekezaji wa kampuni kubwa za mawasiliano kutoka nje ya nchi.

Katika bajeti ilisomwa na Dk Mwigulu, Serikali inakusudia kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja za mkononi, vishikwambi (Tablets) na modemu.

Alisema sekta ya mawasiliano imekuwa ikikua vizuri na kuwa kiungo muhimu cha kuongeza wigo wa wananchi ambao wako kwenye ulimwengu wa kidijitali na kwenye sekta ya fedha.

Hatua hiyo itasaidia kupunguza bei ya simu nchini jambo ambalo linaweza kusababisha watu wengi kumiliki simu ambazo kwa sasa ni kitu muhimu kwa maisha ya binadamu, lakini jambo hilo linaweza kuathiriwa na tozo mpya katika matumizi ya simu.

Dk Mwigulu alisema Serikali inakusudia kutoza tozo ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.

“Kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala unaotumwa au kutolewa, pendekezo hili litaongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh1.25 bilioni,” alisema Dk Mwigulu.

Pia, alisema Serikali inakusudia kutoza kiasi cha Sh10 hadi Sh200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji na pendekezo hili litapelekea kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh396.30 bilioni.

Licha ya kuwa Dk Mwigulu hakufafanua namna utozaji wa kodi hiyo, lakini kwa hatua hizo za kikodi maana yake ni kuwa Watanzania wengi watakuwa na uwezo wa kununua simu lakini gharama za uendeshaji ni mzigo mpya.

“Kumiliki laini nyingi za simu sasa itakuwa ni ufahari na ishara ya mtu mwenye ukwasi mkubwa, gharama za makato ya huduma za miamala ya simu nazo zinakwenda kuongezeka licha ya kilio cha muda mrefu kutaka zipunguzwe,” alisema Osward Joseph, ambaye ni mtumiaji wa simu.

“Hatua hii ya kuanzisha tozo hizi kwa watumiaji wa simu zitakuwa mzigo kwa wananchi na hasa kwa wale wa wananchi wa kipato cdha chini na inaweza kuathiri ukuaji wa sekta ya mawasiliano,” aliongeza Hendi.

Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kuna jinsi mbili tu katika ongezeko la tozo ya simu kwa kutengeneza mfuko maalum wa fedha zake ili zifanye kazi maalum au kuzifuta.

Nayo Kampuni ya ushauri wa kodi ya PWC katika uchambuzi wake jana ilisema hatua hiyo ya kikodi inaweza kuathiri lengo la kuwa na matumizi ya fedha jumuishi (financial inclusion). Pia, haifahamiki namna ambavyo kampuni za simu zimejipanga kutekeleza kodi hizo pendekezwa.


Kodi ya majengo

Wakati Serikali ikitangaza kusudio la kuanza kukusanya kodi ya majengo kwa kutumia mfumo wa wa umeme kupitia mashine za kulipia umeme kadiri unavyotumia (Luku), baadhi ya watu wameonyesha wasiwasi wa kulipia kodi nyumba zisizokuwa zao.

Hiyo ni kutokana na kile walichokibainisha kuwa si nyumba zote zilizojengwa nchini wanaishi wenye nyumba ambao, jukumu la kulipia kodi hiyo ni lao.

Dk Mwigulu alipendekeza kufanya marekebisho hayo kwenye Sheria ya Kodi ya Majengo, Sura 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa Luku.

“Kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo au mtumiaji wa mita, kwa kuwa Sheria ya Kodi ya Majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo, napendekeza kodi ya majengo ya kiwango Sh1,000 ikatwe kwa mwezi kwenye nyumba.

“Kiwango hicho kwa nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa katika ununuzi wa umeme. Napendekeza kiwango cha Sh5,000 kwa mwezi kwa kila ghorofa au ‘apartment’ zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme,” alisema.

Wakati azma hiyo ikilenga kurahisisha ukusanyaji kodi hiyo, Dk Abel Kinyondo wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anabainisha kuwa vipo vitu vingi vya kuangaliwa kabla ya kuanza kutumia mfumo huo.

“Hiyo ni kwa sababu utahamisha jukumu la ulipaji kodi ya majengo kutoka kwa mmiliki kwenda kwa mpangaji, watu wote kulipa kodi ya aina moja na baadhi ya nyumba hazitalipa kodi hiyo kabisa.

“Ukisema ukate kodi hii katika luku kuna nyumba ambazo wanaisha wapangaji, wao ndiyo wanunuzi wa umeme na wao ndiyo watalipa kodi hii hivyo, utakuwa umehamisha jukumu la kulipa kodi kutoka kwa mlengwa kwenda kwa mpangaji,” alisema Dk Kinyondo

Kuhusu kulipa kodi aina moja alisema mita haiwezi kutofautisha nyumba ya ghorofa 50 na ile ya kawaida hivyo, ikatwe kiwango kinachotakiwa na mwisho wa siku watu wanaweza kujikuta wanalipa kiwango sawa cha kodi na baadhi ya mapato kupotea.

“Pia kuna nyumba zinatumia vyanzo vingine vya umeme kama sola hawahitaji kuwa na mita ya Luku hivyo hawatalipa kodi, kuna nyumba ambazo zimejengwa watu wanaishi bado hawana umeme hawatalipa kodi hivyo, naweza kusema hili pendekezo halijaangaliwa vizuri,” alisema.


Shughuli faini za bodaboda

Wakati madereva wa bodaboda wakiendelea kushangilia punguzo la kiasi cha faini watakachotozwa kwa kila kosa moja watakalotenda, wamesema wapo wanaosema baadhi ya vitu vilivyoongezewa ushuru havitaathiri na wengine wakiwa na mtazamo tofauti.

Dk Mwigulu alisema kuanzia Julai mosi waendesha pikipiki na bajaji wamepunguziwa faini ya makosa ya barabarani kutoka Sh30,000 hadi Sh10,000.

Licha ya kupunguza faini, imeongezwa Sh100 kwa kila lita moja ya dizeli na petrol kama ushuru wa barabara, pia ongezeko la ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye matairi mapya.

“Wengine walikuwa wanapoteza maisha kwa sababu ya kuwakimbia trafiki, kwa ajili ya madeni au makosa waliyonayo ikiwemo kutovaa kofia ngumu sasa faini ikiwa ndogo hawatakimbiana,” alisema Simon Akili ambaye ni dereva wa bodaboda.

“Kuna wakati inakuwa kama mkosi, kila baada ya siku mbili cheti (unaandikiwa faini), zinasoma tu kule, mwisho unajikuta unadaiwa Sh120,000 naitoa wapi, huna uhuru na biashara yako, matokeo yake ikawa ukikamatwa unatoa kitu kidogo,” alisema. Hata hivyo, wengine wanasema kuwa Serikali imewapa maumivu kwenye ongezeko la kodi za vipuri.

“Wapo bodaboda wengine ambao wanamaliza mwaka bila kuandikiwa faini, hivyo punguzo hilo la faini halina maana sana. Kupanda kwa ushuru wa forodha katika matairi, vipuri na mafuta hapa kuna maumivu,” alisema Juma Kassi ambaye ni bodaboda.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu alisema ushuru wa forodha utapungua kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwa waunganishaji pikipiki za matairi matatu bila kujumuisha fremu kwani zinatengenezwa nchini.

Akizungumzia hoja hizo, Dk Donald Mmari ambaye ni Mkurugezi Mtendaji wa Utafiti wa Sera ya Uchumi na Fedha wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (Repoa), alisema kilichofanyika kwa ujumla kitasaidia kuchochea uzalishaji wa ndani wa vifaa vya usafirishaji jambo ambalo litapunguza bei, kutoa fursa za ajira.

Hata hivyo, alionyesha wasiwasi wake wa kushushwa faini watakayotozwa bodaboda na waendesha bajaji kuwa huenda kikachochea uvunjaji sheria za barabarani.

Kuhusu kushuka kwa ushuru wa bajaji zitakazounganishwa nchini, Joel Kishaka alisema utachochea kushuka kwa bei za bodaboda ambazo zimeajiri vijana wengi.

“Bei ikishuka hata tutakuwa na uwezo wa kununua tena, kama ulikuwa na moja inakuwa unaongeza nyingine. Kwa nafuu hiyo inaweza kuchangia vijana wengi kujiajiri na kufungua fursa za ajira kwa wengine kupitia usafiri huo,” alisema.

Advertisement