‘Ofisi ubalozi mdogo wa Italia Zanzibar zipo’
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo
Muktasari:
- Katika swali lake, mbunge amehoji ni kwa nini ofisi ndogo za ubalozi wa Marekani, Uingereza na Italia zilizokuwa Zanzibar zilifungwa?
Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema nchi ya Italia bado ina ofisi ndogo ya ubalozi (Vice-Consulate) iliyopo eneo la Kiembesamaki, Barabara ya kwenda Uwanja wa Ndege wa Karume Unguja, Zanzibar.
Aidha imemtaja mwakilishi wake (Konseli Mkuu) anaitwa Stefano Totisco wa Cafe 27.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 25, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo wakati anajibu swali la Mbunge wa Bumbwini (CCM), Mwinyi Jamal Ramadhan.
Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji ni kwa nini ofisi ndogo za ubalozi wa Marekani, Uingereza na Italia zilizokuwa Zanzibar zilifungwa?
Waziri amesema hivi karibuni nchi ya Italia imeifahamisha wizara rasmi nia ya kupandisha hadhi ya ofisi hiyo kutoka Vice-Consulate kuwa Consulate General yaani Konseli Kuu yenye mwakilishi wa hadhi ya juu zaidi wa Serikali ya Italia nchini Tanzania kupitia uwakilishi wake uliopo Zanzibar.
"Bwana Stefano Totisco tayari ameshathibitishwa na Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa Konseli Mkuu ambapo sasa atashughulikia masuala ya wananchi wa Italia wenye makazi ama biashara zao Zanzibar hususan katika sekta ya utalii," amesema Balozi Kombo.
Kwa mujibu wa Balozi Kombo, Stefano atashughulikia masuala ya kikonseli ya Watanzania wenye mwingiliano wa usafiri na biashara na Italia.
Amesema huduma nyingi zaidi za uwakilishi wa Italia zitatolewa na Ofisi hiyo iliyopo Zanzibar kuliko hapo awali kabla ya kupandishwa hadhi yake akisema hiyo ni taarifa njema na ya faraja kwa Zanzibar hasa kwa sekta ya utalii, ambayo bado nchi ya Italia inaongoza kwa idadi ya watalii kwa mwaka.
Waziri amesema Serikali inatambua umuhimu wa nchi marafiki ikiwemo Marekani, Uingereza na Italia na nyingine zenye tija kwa Taifa kuwa na ofisi zao ndogo za ubalozi upande wa Tanzania Zanzibar katika kuratibu na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi, utalii, siasa na kitamaduni.
Ameeleza ofisi hizo ni muhimu kwa ajili ya kutoa huduma za Kikonseli kwa wananchi wa Zanzibar na raia wa nchi zao waliowekeza na wanaoishi Zanzibar kwa mujibu wa Ibara ya Tano ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1963 (Vienna Convention on Consular Relations 1963) unaosimamia uhusiano wa kikonseli na ofisi ndogo za ubalozi.
Ametaka mkakati kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kufanya mazungumzo na Serikali za nchi hizo ili kuzishawishi zifungue tena ofisi ndogo za balozi zao upande wa Zanzibar.