Ripoti ya Twaweza ilivyozua mjadala, sababu za viongozi kupoteza umaarufu
Muktasari:
- Utafiti huo, uliohusisha takwimu zilizokusanywa kutoka kwa watu 1,241 waliohojiwa kutoka Tanzania Bara mwezi Aprili, unaonyesha uungwaji mkono wa Rais John Magufuli umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 mpaka asilimia 55 mwaka 2018, ikiwa ni kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea kwenye historia ya nchi.
Dar es Salaam. Ripoti ya Taasisi ya Twaweza iliyotolewa juzi jijini Dar es Salaam imeibua mjadala mzito, huku wengi wakihoji sababu ya viongozi wa kuchaguliwa kupoteza umaarufu.
Utafiti huo, uliohusisha takwimu zilizokusanywa kutoka kwa watu 1,241 waliohojiwa kutoka Tanzania Bara mwezi Aprili, unaonyesha uungwaji mkono wa Rais John Magufuli umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 mpaka asilimia 55 mwaka 2018, ikiwa ni kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea kwenye historia ya nchi.
Hata hivyo, utafiti huo unaonyesha kuwa kama uchaguzi ungefanywa wakati huo, asilimia 55 ya wananchi wangempigia kura. Vilevile umeonyesha bado wananchi kwa kiasi kikubwa wanaendelea kuunga mkono wagombea wa CCM.
“Zaidi ya nusu wangewapigia kura wagombea wa CCM wa udiwani (asilimia 51), wabunge (asilimia 51), na urais (asilimia 55). Uungwaji mkono wa CCM kama chama umeendelea kuwa imara kiasi kwenye miaka ya hivi karibuni kukiwa na asilimia 63 ya wananchi wanaosema wako karibu na CCM mwaka 2017 ukilinganisha na asilimia 58 mwaka 2018,” imeonyesha sehemu ya utafiti huo.
Wakizungumza katika hafla ya kuwasilisha ripoti hiyo, baadhi ya wachangiaji walielezea sababu za kushuka huko huku pia wakitoa suluhisho.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Vicencia Shule alihusisha kushuka huko na suala la kijinsia, akisema wanawake ambao ndiyo wapigakura wengi wamepuuzwa.
Alisema licha ya kupuuzwa, utafiti huo umeonyesha kuamka kwa wanawake hasa kwenye suala la maandamano.
“Kwenye suala la maandamano, ufahamu wanawake na wanaume na wanaume kitakwimu hawakupishana sana. Wanaume ni asilimia 43 na wanawake ni asilimia 41. Pamoja na kuogopa vurugu, wanawake wameelewa kwamba yale madai yaliyoleta maandamano ni madai yao,” alisema Dk Shule.
Mbali na wanawake, Dk Shule alisema uelewa wa wanaume umeshuka kwenye matatizo ya kijamii, wakati wao ndiyo wameshikilia uongozi wa Dola.
“Wanaume wa nchi hii ndiyo waliojitwalia madaraka ya kuongoza nchi bila kujali idadi ya wanawake. Kitu kingine kizuri zaidi ni umaarufu wa Rais unazidi kushuka. Wananchi wameelewa kipi kinatekelezeka na kipi hakitekelezeki,” alisema.
Alisema kumekuwepo na tishio la viongozi kupiga wanawake, jambo linalosababisha kushuka kwa kukubalika kwao kwa kuwa wanawake ni wengi katika idadi ya wapiga kura.
“Hakuna mtu atakukubali kama unapiga mashangazi, hakuna mtu atakupenda kama unatisha wanawake. Kwa hiyo hii ni ‘wake-up call’ kwa mwenyekiti wa chama, kwamba matendo yake kwa wapigakura ambao wengi ni wanawake, yanathibitisha wazi kuwa umaarufu wake unashuka kwa kuwakosea haki hata kuwanyima fursa ya kushika dola,” alisema.
Inaendelea uk 22
Inatoka uk 21
Hoja hiyo iliungwa mkono na mdau wa habari, Maria Sarungi aliyetaja mchango wa mwanadada MangeKimambi anayeishi Marekani akisema alichangia kuhamasisha wanawake.
“Utaona wanawake wamehamasika na walikuwa na utayari wa kuandamana. Nadhani Mange Kimambi ameweza kuwafikia wanawake wengi kupitia mitandao anayotumia,” alisema Sarungi.
Alizungumzia pia kundi la watu ambao hawajaamua upande wa kupigia kura, akisema kuongezeka kwake ni hatari kwa chama tawala.
“Mara nyingi idadi ya watu ambao hawajaamua kumpigia mtu kura ilikuwa ndogo kama asilimia 10. Lakini sasa imefikia 30, yaani theluthi moja. Hiyo inamaanisha kwamba hao ndiyo watakuja kufanya maamuzi mwaka 2020,” alisema.
Kuhusu kushuka kwa umaarufu wa viongozi, Sarungi alihusisha na hofu ya wananchi kutoa maoni akisema hali hiyo inaweza kuwa kukubwa zaidi.
“Kwa upande wa vijijini, CCM ina asilimia 59 kwa wananchi, lakini kwa Rais ni asilimia 52. Ukiangalia kwa wanawake wana asilimia 53 wanaunga mkono CCM vijijini. Ina maana kubwa sana kwa chama na kwa wabunge,” alisema.
“Aliposhuka hadi asilimia 71 mwaka jana tukajua ni ya kihistoria. Tungefuatilia zaidi kujua kama kuna woga uliotawala kwa wahojiwa.
“Tulichoona ni kwamba watu wanaojisikia woga kujieleza kisiasa ni asilimia 52. Je wakati wanajibu Twaweza walikuwa wanajisikia huru? Kama kwa hali hiyo tu asilimia 55 tu wamesema ina maana iko chini ya hapo.”.
Mkurugenzi wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo alisema kushuka kwa CCM maeneo ya vijijini na kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na upande wowote ni fursa kwa wapinzani.
Kwa upande wake Rais wa TLS, Fatuma Karume alizungumzia uhuru wa kujieleza, akisema CCM inapaswa kujua Watanzania wengi wanataka uhuru huo.
“Ukitazama takwimu, zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanaona huo ni uhuru muhimu na wamejikita demokrasia kwenye uhuru. Sasa CCM wanasema, demokrasia ni haki ya kupiga kura kwa miaka mitano. Tafsiri ya demokrasia si haki ya kupiga kura, ni pana. Si sawa kudharau maoni ya watu wengi,” alisema Karume.
“Unajua Serikali inadhani ikiwaambia wananchi itawapiga kama mbwa koko, itawatisha wananchi. Asilimia 18 tu hawakutaka kupigwa, lakini asilimia zaidi ya 50 wanaona kutaleta vurugu. Lakini, wasidhani polisi, washawasha kauli chafu au za kutisha zitawatisha wananchi kuandaana.”
Akijibu hoja za wachangiaji, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema idadi kubwa ya wananchi wanaoendelea kukiunga mkono chama hicho ambao ni wazee na wasio na elimu ni wanyonge.
“Hawa mnaosema wameelimika, halafu kuna wale ambao hawajasoma (asilimia 66) na wale shule (asilimia 60) ya msingi na sekondari, nitakupa hesabu rahisi. Ni asilimia 66 kwa sababu wengi kati yao ni wanyonge wanaoona namna ambavyo tunashughulika na shida za wananchi. Hao lazima waikubali CCM,” alisema Polepole.
Alitaja mambo matatu akisema wakiyatekeleza kukubalika kwa Rais na chama hicho kutaongezeka ndani ya mwaka mmoja. Alitaja vitu hivyo kuwa ni maji, umeme vijijini na afya.
Alisema mengine ni kuboresha uduma ya elimu na miundombinu ya usafiri na kuwepo kwa mkakati wa kukuza kilimo kwa ajili ya malighafi za viwandani.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na mwanahabari nguli nchini, Jenerali Ulimwengu aliyesema maendeleo ya vitu hayaondoi kiu ya wananchi kudai mabadiliko
“Tuzungumzie ushiriki wa wananchi na wananchi ndiyo CCM. Majibu yake (Polepole) ni kuweka mkate mezani. Bwana Yesu au Issa bin Mariam alisema binadamu hataishi kwa mkate peke yake,” alisema.
“Unaweza kuweka mkate na siagi, lakini kama hukumpa matumaini ya kiroho, atakuja kugeuka siku moja. Development can neverbe inflicted (maendeleo hayawezi kulazimishwa).
“Sawa maedeleo ni barabara, SGR (reli ya kisasa), na mengine, lakini spiritural development (maendeleo ya kiroho). Ukisikia mtu anasema utapigwa kama mbwa koko, huyo hana hiyo spiritual development.”
Wakati utafiti huo ukionyesha asilimia 64 ya wananchi wanaosema uhuru umepungua kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano na kutoa maoni yao na vyombo vya habari kukosoa au kuripoti maovu ya Serikali (asilimia 62), Polepole alisema mikutano hiyo haijakatazwa.
Kuhusu mikutano ya hadhara, alisema haikuzuiwa bali imewekewa utaratibu zaidi ya namna ya kufanya siasa.
“Mikutano ya hadhara tumesema, ndugu (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe anatoka Hai. Ni mbunge ana kofia nyingi, chama chake kina uongozi. Lakini yeye kama mbunge ana jukumu la kufanya mikutano ya hadhara pale. Mtu mwingine asiingie pale Hai kufanya kazi ya siasa,” alisema.
Nini kifanyike?
Akihitimisha mjadala huo, Ulimwengu alisisitiza kuwepo kwa hofu kwa wananchi kutokana na matukio yaliyojitokeza siku za karibuni.
“Kama watu hawajulikani wako wapi, Ben Saanane hajulikani yuko wapi, Azory (Gwanda) hajulikani, Lissu (Tundu) bado yuko Ubelgiji. Siyo kwamba imefanywa na CCM hapana,” alisema.
“Watu hawa wanatekwa, hawa wanapigwa. Hatujasema nani anawapiga, lakini kama unaletewa ripoti kila baada ya miezi mitatu kwamba mtu kapigwa risasi au mtu kapotea, ningekuwa na wasiwasi sana.”
Alizungumzia pia malumbano yaliyojitokeza kati ya Serikali na viongozi wa dini, akisema Serikali haitaweza kuwatisha viongozi hao bali ijenge utamaduni wa kuwasikiliza.
“Serikali inapaswa kujenga utaratibu wa watu kutoa mawazo. Watu wapinge na kuuliza maswali kwa nini mnafanya hivyo ndiyo mnajenga utaratibu huo. Lakini si kuwatisha. Wale hamwezi kuwatisha, wale siyo Chadema,” alisema.
Kama unafanya mema kwa Watanzania, basi wangependa kujua. Kama kuna mahali mnakosea, basi waseme. Yoyote anayetoa mazuio kutoa maoni kuhusu mema anayowatendea basi hawatendei.”
Katibu Mkuu wa Chadema Dk VincentMashinji alisema licha ya chama chao kuitisha maandamano ya Umoja wa Kupiga Udikteta (Ukuta) kushindikana, maandamano yaliyoitishwa na Aprili 26 yalipata nguvu baada ya wananchi kubanwa zaidi kiuchumi.
“Ndiyo maana kwenye maana kwenye maandamano ya Aprili 26, watu wengine walisema ofisi yangu inaratibu, vyovyote vile. Halikuwa jambo letu bali ulikuwa ni mwamko wa raia, kwa sababu waliona kwamba ule Ukuta wa Agosti 2016 unahitaji kujengwa sasa hivi. Ndiyo maana idadi ya iliongezeka,” alisema.
“Jambo ambalo CCM wanatakiwa kulifanya, kwanza waache kuingilia mambo ya wananchi. Ndiyo maana juzi waliwaita wale wazee, wachukue waliyoyasema. Lazima kuwe na juhudi za elimu ya uraia zifanyike. Huwezi kuongoza wananchi wanaosema wewe ni mchafu halafu suluhisho lake liwe ni kuwapiga.”