Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata la ununuzi wa Tanga Cement laibuka bungeni…Mwigulu yamkuta

Dodoma. Sakata la ununuzi wa kampuni ya saruji Tanga Cement limeibuka bungeni kwa wabunge kusema kuruhusu mkataba huo kuendelea kutasababisha ukiritimba utakaoleta madhara makubwa katika bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa ujenzi.

 Wakijadili makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2023/24, baadhi ya wabunge walisema ununuzi uliopangwa wenye thamani ya Sh137 bilioni utachochea kupanda kwa bei ya saruji, hasa pale mtengenezaji mkuu atakapofanya matengenezo ya kawaida ya viwanda vyake.

“Nimesoma kwenye magazeti kuhusu mpango wa kuunganishwa kwa kampuni ya Twiga Cement na Tanga Cement. Iwapo (Twiga Cement) atachukua hisa za Tanga Cement hatutakuwa na uwezo wa kudhibiti ongezeko la bei,” alisema Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo.

Alisema Watanzania hawataweza kujenga nyumba zenye hadhi iwapo saruji itachukuliwa kuwa ni bidhaa ya anasa, hivyo aliliomba Bunge kuangalia jambo hilo na Serikali kutoa taarifa za kina kuhusu suala hilo.

Wakati Nollo akitoa mchango wake, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu alisimama kwa hoja na kueleza kwa mujibu wa sheria ya ushindani wa haki, hakuna kampuni iliyoruhusiwa kuwa na umiliki wa soko kwa zaidi ya asilimia 36.

“Muungano anaouzungumzia utajenga ukiritimba wa soko unaovuka kizingiti cha ukiritimba wa soko kwa mujibu wa sheria iliyoidhinishwa na Bunge tukufu na kwa njia hiyo, Watanzania watakuwa katika nyakati ngumu katika suala zima la bei ya saruji,” alisema Kingu.

Muunganisho unaozungumziwa ulianza Oktoba 2021, wakati Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement – na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement, ilipotoa taarifa ya pamoja kuwa wamekamilisha masharti ambayo awali angepata asilimia 68.33 ya hisa katika Tanga Cement.

Awali, Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) iliidhinisha mapendekezo ya kutwaliwa kwa kampuni hiyo kwa masharti kuwa itakayoinunua isifunge shughuli za Tanga Cement; kwamba iendelee kuzalisha na kuitangaza chapa ya Simba Cement (Tanga Cement), na kwamba ilizuiliwa kuwaachisha kazi wafanyakazi waliokuwapo Tanga Cement.

Hata hivyo, baadhi ya wawekezaji katika uzalishaji wa saruji walipinga uamuzi huo kwa misingi kwamba kuruhusu muunganisho huo kuendelea kungezuia, kuweka vikwazo au kuvuruga ushindani sokoni kinyume na sheria ya ushindani wa haki, 2003.

Ni kutokana na sababu hizo ambapo Kampuni ya Chalinze Cement Limited na chama cha watetezi wa watumiaji Tanzania (TCAS) walikata rufaa FCT, ambayo ilitengua muunganisho huo uliopingwa kupitia hukumu yake iliyotolewa Septemba 23, 2022.

Hukumu ya hivi karibuni iliyotolewa na Jaji Salma Maghimbi, Dk Godwill Wanga na Boniface Nyamo-Hanga ilieleza: “Kwa mujibu wa kifungu cha 11 (1) cha FCA (Sheria ya Ushindani wa Haki), baada ya kufuta sheria ukiweka kando uamuzi wa FCC, Mahakama inakataza kuunganishwa kati ya Scancem International DA na Tanga Cement.”


…Mwigulu yamkuta

Katika hatua nyingi, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuelezwa alitumia jina la Rais mahali ambapo hahusiki.

Hoja hiyo iliyozua mjadala wa miongozo ni kauli ya Dk Mwigulu ya kuwa malipo yote yanapata idhini na kibali cha Rais kabla ya kulipwa, jambo ambalo wabunge walianza kuhoji.

Hali hiyo ilitokea wakati wabunge wakichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka fedha 2023/2024.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimaliza mgongano huo kwa kumweleza Dk Mwigulu kuwa ni sahihi alichokisema, lakini hakuwa sahihi kwa mazingira aliyoyasema.

Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alionyesha kuchukizwa na kitendo cha ongezeko la fedha za manunuzi ya ndege mpya ya mizigo kinyume na fedha zilizokuwa kwenye mkataba wa awali, akataka watumishi wa Serikali waliokubali ongezeko hilo bila kuhoji waachie nafasi zao kwa kuwa hawana uchungu na fedha.

“Kuna mradi hapa tumetengeneza ndege ya mizigo ambayo tunakaribia kuipokea, last installments (awamu ya mwisho) ilikuwa tulipe dola 37 milioni, invoice imekuja na dola 86 milioni, unauliza mkataba ulisemaje? Hii imetokana na wapi? Ooh vifaa vimepanda bei, vipi? Mkataba wetu ulisemaje?” alihoji Rais Samia.

Jana, sakata lilianzia kwa mbunge wa viti maalumu, Ester Matiko aliyedai kuwa kuna ubadhirifu mkubwa katika manunuzi ya ndege, lakini wahusika wanaendelea kuwa kimya bila mamlaka kusema jambo lolote.

Matiko alisema haikubaliki na wala haiingii akilini na Tanzania itakuwa Taifa la ajabu kuruhusu watendaji hao kuendelea kuwepo wakati wametia hasara.

Hata hivyo, bila kumtaja kwa jina alisema kila siku Waziri wa Fedha anavaa tai shingoni yenye rangi ya bendera ya Tanzania inayoashiria uzalendo, lakini akahoji uzalendo wa waziri uko wapi.

Mbunge huyo alisema malipo ya ndege ni makubwa, lakini akahoji kwa malipo madogo inakuwaje kwa watendaji ndani ya Serikali kwa madai kuna mianya mikubwa ya kufuja fedha za umma.

Kauli hiyo ilimwamsha Waziri Mwigulu baada ya kuomba atoe taarifa kwa mzungumzaji wa wakati huo (Matiko) na kusema mifumo ya malipo iko imara, huku akidai waliohusika kuongeza fedha za manunuzi ya ndege watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Katika taarifa yake, Dk Mwigulu alisema utaratibu wa malipo uliowekwa uko imara na kwamba hakuna vitu vya hovyo ambavyo vinaweza kupitishwa.

“Hakuna malipo ya mwezi yanayoweza kufanyika bila Rais kujua na mahitaji yote hupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kuombea ridhaa kwa Rais,” alisema Dk Mwigulu na kuongeza:

“...na hilo la ndege unalolisema yalipoletwa mahitaji wizarani tuliliona lina ongezeko ambalo kama ni la kimkataba lazima tupate ushauri wa Mwanasheria Mkuu.”

Baadaye mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliomba mwongozo baada ya kipindi cha maswali akiomba kujua kauli iliyotolewa na Waziri Mwigulu kama ni sahihi kwamba Rais anahusika na malipo.

Ole Sendeka alijielekeza katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 35 kwamba imetaja kuwa Rais atakasimu madaraka, lakini inashangazwa anatajwa kwenye malipo hayo.

“Je, ni sahihi kulitumia jina la Rais katika mazingira haya wakati wabunge wanaonyesha masikitiko yao juu ya malipo yasiyo sahihi ambayo Taifa limeingia kwa wakati huu?” alihoji Ole Sendeka.

Spika alimpa nafasi Waziri Mwigulu ili kutoa ufafanuzi ambaye alirudia kauli yake kuwa, licha ya kuwepo kwa mlipaji mkuu wa Serikali ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya fedha, lakini Rais hutakiwa kuidhinisha kwa baadhi ya malipo na matumizi.

Dk Mwigulu alisema matumizi makubwa na yenye ulazima hupelekwa kwa Rais kabla ya tarehe 10 ya mwezi husika na anayapitia na kuidhinisha ndipo anatoa idhini kabla ya tarehe 17 ya mwezi huo.

“Huo ndiyo utaratibu ambao tumekuwa tukiutumia tangu awamu ya nne, na mimi nina karibu miaka 10 tangu nilipokuwa Naibu Waziri wa wizara hii, muhimu kutengeneza silinji ambayo Rais atatoa kibali chake,” alisema Dk Mwigulu.

Hata hivyo, kwenye suala la ndege, alisema hakukuwa na taarifa kwa mwezi husika ambazo wangezipeleka kwa mwenye nchi ili zikapate kibali chake.

Spika wa Bunge alihitimisha kwa kusema kuwa mwongozo wa Ole Sendeka ndiyo sahihi, kwani ibara ya 35 ya Katiba inaelekeza kuwa malipo hufanywa na waliodhinishwa kwa niaba ya Rais.

Dk Tulia alisema kumtwisha mzigo Rais kwamba alikuwa anajua kila kitu wakati tayari alishakasimisha madarakani, si sahihi na wala si lazima ajue kila taarifa, hivyo akaomba kauli ya Dk Mwigulu inayomtaja Rais isichukuliwe kama ilivyo.