‘Tanroads ishughulike na wanaoharibu barabara'

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Tanroads wataendelea kufanya kazi kwa bidii katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija
Dodoma. Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ametaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kushughulika kisheria na watu wanaosababisha barabara kuharibika kabla muda uliopangwa kumalizika.
Bashungwa amesema hayo jana Jumatano, Februari 14, 2024 wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tanroads.
“Lazima tupambane kuhakikisha barabara zinazoharibika kabla ya muda wake kwa sababu za kizembe za ununuzi lazima tushirikiane kupambana,” amesema.
Bashungwa amesema anataka kuona kwa vitendo kwa makandarasi wanaofanya uzembe wanachukuliwa hatua za kisheria.
Ameagiza Tanroads kutumia kikamilifu mtambo wa Ukaguzi wa Barabara wakati wa kufanya ukaguzi wa miradi ya barabara na madaraja na hata kutumia vifaa vingine vitakavyoweza kuwasaidia kubaini ubora wa mradi mapema kabla ya kukabidhiwa.
Ameielekeza Tanroads kuimarisha na kukijengea uwezo kitengo chake cha Usimamizi wa Miradi (Tecu) ili kusimamia miradi kwa weledi na ufanisi.
Bashungwa amewataka kusimamia sheria ya uzito wa magari barabarani na kutoa adhabu kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo.
“Hakuna kiongozi wala mtumishi ambaye yupo juu ya sheria, hata mimi siwezi kumsaidia yeyote anayekiuka sheria hii, atakayekiuka achukuliwe hatua na sio kunipigia simu,” amesema Bashungwa.
Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amemhakikishia Bashungwa kuwa watatekeleza maagizo waliyopewa na kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija.
Mweyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyingine (Tamico), Nchama Wambura amesema wataendelea kushirikiana kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa utekelezaji sahihi na ubora kwa miradi wanayoendelea kutekeleza nchini.