Tanzania ya nne duniani kwa saratani ya shingo ya kizazi

Waziri Afya, Ummy Mwalimu (wanne kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa dozi moja ya chanjo ya saratani ya mlango wa  kizazi uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema gharama ya matibabu ya mgonjwa mmoja anayeumwa saratani  ya mlango wa shingo ya kizazi kwa mwaka mmoja yanafikia zaidi ya Sh8 milioni

Mwanza. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha Tanzania ni nchi ya nne kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi ikongozwa na Eswatini, Zambia na Malawi.

Hata hivyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema gharama ya matibabu ya mgonjwa mmoja anayeumwa saratani  ya mlango wa shingo ya kizazi kwa mwaka mmoja yanafikia zaidi ya Sh8 milioni.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 22, 2024 wakati wa uzinduzi wa dozi moja ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi (HPV) kwa wasichana wa miaka tisa hadi 14 jijini Mwanza, Waziri Ummy amesema saratani hiyo ndiyo inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi nchini, akitaja njia ya kuitokomeza ni chanjo kwa wasichana ambao hawajaanza ngono.

“Tumepiga mahesabu kumuhudumia mgonjwa mmoja wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi inaweza kugharimu mpaka Sh8 milioni kwa mwaka. Chanjo ya HPV dozi moja ni Dola 3.50 za Marekani kwa hiyo ni sawa na Sh10,000 naomba tupime kutumia Sh10,000 kuliko kuja kutumia zaidi ya Sh8 milioni kwa ajili ya kutibu mgonjwa wa saratani  ndio maana tunasema kinga ni bora kuliko tiba,”amesema.

Ummy amesema katika kila wagonjwa 100 wanaougua saratani nchini, 23 kati yao wanaumwa ya mlango wa kizazi, huku  akiwataka viongozi wa mikoa na wilaya kuhamasisha wazazi kuwachanja watoto wao bila kutumia mabavu.

Amewataka wazazi kuondokana na dhana ya kuamini kuwa chanjo ya HPV ni ya uzazi wa mpango akidai ni salama kwani waliochanjwa wakati wa majaribio mwaka 2014 mkoani Kilimanjaro wameolewa, wamezaa na wapo na watoto wao akisisitiza hakuna Serikali inaypweza kuwaingiza watu wake katika matatizo.

“Kwa hiyo Tanzania tunateswa na saratani ya mlango wa kizazi, lakini kumbe sayansi iliyothibitishwa pasi na shaka tunaweza kuzuia saratani ya mlango wa kizazi endapo tutawapa chanjo mabinti ambao hawajaanza ngono.

“Tulianza dozi mbili mwaka 2018 lakini ukafanyika utafiti wa kisayansi tukawafuatilia watoto waliokuwa wamepata chanjo ya kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi dozi mbili, na kuna watu waliopewa dozi moja wataalamu wetu wa Tanzania ambao wanatoka Taasisi ya Utafititi wa Magonywa ya Binadamu  (NIMR) wamejiridhisha kwamba dozi moja ya saratani ya mlango wa kizazi inatosha kumkinga msichana asipate ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi,”amesema Ummy.

Utafiti wa kisayansi unasema saratani ya shingo ya kizazi inayotokana na Virusi vya Human Papiloma (HPV) huambukizwa kwa njia ya ngono.

“Virusi vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi vinatoka kwa wanaume, lakini mwanamke unavipataje? ni kwa kujamiiana; kwa hiyo kinga ya kwanza wanangu ni kujiepusha na mambo ya wakubwa (ngono) kabla ya umri,”Ummy amewaambia wanafunzi waliokusanyika wakati wa uzinduzi huo wa dozi moja ya HPV.

Amesema Serikali imedhamiria mpaka itakapofika Desemba, 2024 zaidi ya wasichana milioni 4.8 wenye miaka tisa hadi 14 wawe wamepewa chanjo.

 Mtaalamu bingwa wa afya ya jamii katika idara ya saratani  Hospitali ya Bugando, Dk Kidaya Bashari amesema hospitali hiyo inapata wagonjwa 46,000 kwa mwaka kutoka mikoa ya kanda ya ziwa huku, asilimia 70 hadi 80 wakiwa hatua mbaya ya tatu na ya nne ya ugonjwa huo.

“Kama hali itaendelea hivi, inakadiriwa wagonjwa hao wata-double (wataongezeka)  kufikia mwaka 2023 kwa hiyo lazima tuchukue hatua za awali za kukinga ugonjwa huu wa saratani kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wanaoongezeka siku hadi siku,”amesema Dk Bashari.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema kwa mwaka 2023 idadi ya waliofanyiwa uchunguzi wa saratani  Mwanza ilikuwa ni 40,470 kati yao wanawake 1,510 walikutwa na dalili za awali.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) Tanzania, Elke Wisch amesema juhudi za pamoja zinahitajika kuhakikisha kila msichana nchini anapata kinga muhimu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi. 

“Zaidi ya mpango wa chanjo, pia tutaendelea kuiunga mkono Serikali  kuimarisha utoaji wa huduma shirikishi, ikiwa ni pamoja na kuhuisha programu za afya shuleni, ili kutoa huduma ya afya kwa vijana,” amesema Wisch.