Tarura lawamani ujenzi wa makalavati

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tangini, Primin Gama akiwa jirani na makalavati yanayoelezwa kukaa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 10 pasipo kujengwa. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

 Meneja wa Tarura Wilaya ya Kibaha Samuel Ndoveni amesema watakapopata fedha watashughulikia changamoto hizo

Kibaha. Kati ya maeneo 11 yanayopaswa kuwekwa makalavati kwenye barabara zilizomo ndani ya Mtaa wa Tangini Halmashauri ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani ni matatu pekee yaliyojengwa.

Kati ya hayo matatu, imeelezwa mawili yamejengwa kwa nguvu za wananchi takribani 5,000 wa eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wamesema maisha yao yako shakani hasa kwa wagonjwa na wanafunzi ambao huvushwa kwa kubebwa mgongoni mvua zinaponyesha, jambo linalohatarisha usalama wao.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tangini, Primin Gama amesema licha ya wananchi kujitokeza kuchangia maendeleo, yakiwamo ya miundombinu ya barabara, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) unawakatisha tamaa.

Amesema maeneo mengi ndani ya mtaa huo hayafikiki kwa gari kutokana na kuwapo makorongo, hivyo kuhitajika makalavati.

Ghama amesema wataalamu wa Tarura wamekuwa wakifika maeneo hayo na kutoa ahadi za kufanyika matengenezo ambazo hazitekelezwi.

"Mwaka 2016 tuliomba makalavati Tanroads tukapewa, yaliletwa kutoka Visiga ili yajengwe kwenye barabara zetu, Tarura waliahidi kuja kujenga lakini hawakufanya hivyo,” amesema.

Ameeleza mwaka 2022 na 2023 wananchi walichanga fedha zikapatikana Sh9 milioni, mbunge akaongeza Sh2 milioni wakaweka makalavati kwenye  barabara moja.

Amesema baadaye Tarura walijenga kwenye eneo moja pekee na hadi sasa kazi hiyo haijatekelezwa tena.

Meneja wa Tarura wa Wilaya ya Kibaha, Samuel Ndoveni akizungumza kwa simu na Mwananchi Digital amesema watakapopata fedha watashughulikia changamoto hizo.

“Tunafanya kazi kwa mpango na bajeti, sasa hivi tunaenda kwenye bajeti kwa hiyo yale yatakayokuwa yamepata pesa tutayashughulikia," amesema Ndoveni.

Diwani wa Tangini, Mfalume Karanguti, amesema katika mpango wa bajeti ya Tarura ya mwaka 2023/24 kata hiyo ilitengewa Sh202 milioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara.

Amesema wanasubiri msimu wa mvua upite ndipo kazi ya ukarabati ianze.

Mwajuma Ramadhani, mkazi wa kata hiyo amesema wanapitia wakati mgumu mvua inaponyesha kwa kuwa maji husambaa hadi kwenye nyumba.

Mganga Athumani, kwa upande wake amesema kilio chao ni kujengewa makalavati, barabara zichongwe na ziwekwe kokoto za kutosha.