‘Tuendelee kuyaishi maisha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan’

Waumini wa kiislamu wakiswali swala ya a Idd El-Fitri kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Manispaa ya Morogoro leo Aprili 10 2024.

Muktasari:

  Imeelezwa kuwa kumalizika kwa mfungo wa  Ramadhan isiwe kibali cha watu kuanza kuyageukia maovu bali waendelee kuishi kwa kuamini swala na toba

Morogoro. Wakati waamini wa wakiadhimisha Sikukuu ya Idd El-Fitri, Sheikh Ally Mussa amewaomba kuendelea kuyaishi maisha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao umemalizika kwa kufanya swala na toba.

Sheikh Mussa amesema hayo kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Manispaa ya Morogoro wakati wa Swala ya Idd El-Fitri.

Amesema kumalizika kwa mfungo wa  Ramadhan isiwe kibali cha watu kuanza kuyageukia maovu bali waendelee kuishi kwa kuamini swala na toba, ndiyo kiunganishi kikubwa kati ya Mwenyezi Mungu na wanadamu.

Kabla ya kuanza kwa Swala ya Idd El-Fitri  kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Forest Hill Manispaa ya Morogoro, waislamu waligawiwa tende kama kiashiria cha kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan leo Aprili 10 2024. Picha na Johnson James

“Leo ni siku ya huzuni na furaha kwetu, wengi tunasherehekea sikukuu ya Idd El Fitri lakini wakati tunasherehekea, tunapata huzuni kwa kuwa baadhi yetu watayaacha yale mema yote waliyoyatenda kipindi cha mfungo, nawaomba sana tusiyaache mema tuliyotenda bali tayaendeleza hadi mwisho wa uhai wetu,” amesema sheikh huyo.

Amesema kipindi cha mfungo watu hujinyima na kuwakumbuka wahitaji na maisha huwa ya furaha muda wote. “Kwa hiyo tusikengeuke tuendelee hivyo hivyo.”

Akizungumza na Mwananchi Digital katika viwanja hivyo, Sadick Juma amesema alichokisema Sheikh Mussa kwenye mawaidha yake yana msingi mkubwa kwa kila muumini wa kiislamu.

“Unakuta mtu kafunga mwezi mtukufu wa Ramadhan tangu siku ya kwanza mpaka ya mwisho, lakini siku kama ya leo anaharibu funga yake yote kwa sababu tu ya anasa za dunia, hii haifai,” amesema Juma.

Muumini mwingine, Ally Omary kwa upande wake amesisitiza kuwa kile kilichofundishwa na masheikh mwezi mzima wa mfungo kienziwe kwa watu kuendelea kutenda mema ili mwisho wa siku waifikie pepo njema.

“Mwezi wa Ramadhan unapomalizika watu wengi wanasahau kuswali na kumrejea muumba wao kama ilivyokuwa kwenye Ramadhan, alichokizungumza Sheikh Mussa tukizingatie,” amesema Omary.