Tume ya hakijinai yazua mjadala

Dar/mikoani. Uteuzi wa wajumbe wa Tume ya kuangalia namna ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai, uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan juzi umezusha mjadala mkubwa ambapo baadhi wanapinga uwepo wa wastaafu wa vyombo vya dola huku wengine wakipongeza.

Mjadala huo unaendelea kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali wakihoji sababu za kuteuliwa Wakuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wastaafu, Said Mwema na Ernest Mangu ambao wanadaiwa kuwa sehemu ya matatizo yanayozikabili taasisi walizoziongoza.

Baadhi ya wadau, wakiwamo wanasheria wameweka wazi kuwa uwepo wa wajumbe ambao ni sehemu ya tatizo kwenye taasisi walizowahi kuziongoza na kukosekana kwa wajumbe kutoka asasi za kiraia za haki za binadamu ni ishara kuwa Tume haitokuja na majibu ya kuziimarisha taasisi za haki jinai.

Kukosekana kwa wajumbe kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Asasi nyingine za kiraia (NGO’s), zilizokuwa mstari wa mbele kutaka mfumo wa haki jinai ufumuliwe kunadaiwa kutainyima Tume fursa ya kuaminika zaidi.

Uwepo wa wakuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wastaafu, Saidi Mwema na Ernest Mangu umezidisha mjadala wa uteuzi huo, huku baadhi ya watu wakidai walipokuwa madarakani wawili hao, kulikuwa na kukanyagwa kwa haki za binadamu ndani ya Jeshi la Polisi.

Uteuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kwa kuwa miezi michache iliyopita Rais Samia alimtangaza Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande ndiye atakayeongoza tume hiyo na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue ataongoza sekretarieti yake.

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza, alisema matokeo chanya ya Tume yanahitaji wajumbe wasio na mgongano wa masilahi, wenye fikra huru na maoni huru.


Uteuzi wao

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus juzi usiku, iliwataja wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi ambaye aliwahi pia kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), ambayo ni moja ya Taasisi ya Haki jinai inayonyooshewa kidole kwa utendaji mbaya wakati wa awamu ya tano na kulikuwa na ubambikiziaji watu kesi, zikiwamo za kisiasa.

Wengine ni Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurent Ndumbaro, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Profesa Edward Hosea ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Omary Issa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Saada Makungu, ambaye ni Polisi mstaafu.

Mbali na wajumbe hao, wamo pia Baraka Leonard ambaye ni Ofisa Mwandamizi Ofisi ya Rais na Yahya Khamis Hamad, ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti Chuo Kikuu Zanzibar na Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Zanzibar.

Taasisi nyingine za Haki Jinai ambazo Tume hiyo itawajibika kuzipitia na kutoa mapendekezo ya maboresho ni Jeshi la Polisi, Mahakama, Ofisi ya DPP, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) na Uhamiaji.


Mtandaoni nako ni moto.

Mara baada ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, kutoa taarifa ya uteuzi huo kupitia ukurasa wake wa Twitter juzi saa 3:30 usiku, baadhi ya wananchi walimiminika, baadhi wakipongeza uamuzi wa Rais na wengine kukosoa wajumbe.

Mchangiaji mmoja aliandika “maoni yangu tafadhali boresheni Tume hiyo kwa kuongeza wadau ambao moja kwa moja wanashughulika na masuala ya haki. Wafanyakazi na CMA (Baraza la Usuluhishi wa migogoro ya ajira).”

“Kwa kweli hii Tume haija balance (haina uwiano) hata kidogo. Kuna baadhi humo ndio waliotengeneza tatizo halafu wanateuliwa tena wakajitizame. Hiyo sio sawa. Hebu tuelezane Tanesco na Haki Jinai wapi na wapi?” alihoji mwananchi mmoja.

Mchangiaji mwingine anayesomeka kama Grace Kavishe aliandika “Fikiria hii Tume ilivyo nyeti ila wajumbe wake wanatia shaka kutokana na rekodi zao. Hakuna uwiano wa uwakilishi kimakundi. Haki Jinai inahusisha makundi yote.”

“I’m thinking about (namfikiria huyu) ndugu kutoka Tanesco. Labda kazi yake ni kuhakikisha umeme haukatiki wakati Tume ikifanya kazi yake,” alisema Grace.

Mwananchi mwingine katika kundi la Whatsapp alihoji “Dk Hosea japo sasa hivi yuko TLS lakini alikuwepo Takukuru. Ili kuifanya iwe huru yeye hakupaswa kabisa kuwepo kwa sababu naye alikuwepo huko Takukuru inayolalamikiwa.”

Wakili Peter Madeleka katika ukurasa wake wa Twitter aliweka taarifa hiyo ya uteuzi na kuandika, “miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa katika mfumo wetu wa haki jinai ni watuhumiwa kufia vituo vya polisi na watu kubambikiwa kesi. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan baadhi ya uliowateua katika tume hii hii walishiriki kufanya uovu huu kwa nafasi walizokuwanazo. Hutopata uhalisia.”

Wakili Madeleka ambaye amewahi kuwa Ofisi wa Jeshi la Polisi alisema, “mheshimiwa Rais Samia, pamoja na nia njema uliyonayo katika kuboresha mfumo wa haki jinai nchini, ingekuwa vema katika tume hii ungewateua na waathirika wa mfumo huu na watetezi wa haki za binadamu ili kupata uhalisia wa ubovu wa mfumo.”

Naye Fatma Karume, aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alikosoa uteuzi huo akisema tume hiyo si ya kuboresha taasisi jinai, “hajateua mtu kutoka Magereza na hii ni taasisi muhimu ya jinai.”


Kauli ya Askofu Bagonza

Akizungumza na gazeti hili, Askofu Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya KKKT alisema kuunda tume ni jambo jema, lakini matokeo chanya ya kazi ya tume yanahitaji wajumbe wasio na mgongano wa masilahi, wenye fikra huru na maoni huria.

“Kwa aina ya wajumbe walioteuliwa, sidhani kama tutapata kile ambacho umma wa Tanzania unakipigania na kutarajia kwenye eneo la haki jinai, kwa sababu siyo tu waliopigania haki jinai hawamo kwenye orodha,” alisema na kuongeza:-

“Bali pia baadhi ya wajumbe ni viongozi au wamewahi kuongoza taasisi zinazonyooshewa vidole kwa ukiukwaji wa haki jinai.” Japo hakuzitaja, lakini baadhi ya taasisi hizo ni ofisi ya DPP, Takukuru na Jeshi la Polisi.


Walichokisema mawakili

Wakili Majid Kangile wa jijini Mwanza alisema jambo muhimu na la msingi ni wote wenye dhamana ya utekelezaji wa haki jinai kuheshimu na kuzingatia katiba na sheria.

Akifafanua, mwanasheria huyo alitoa mfano wa jinsi watuhumiwa wanavyotiwa mbaroni, kuwekwna mahabusu ya polisi kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani kinyume cha sheria na ukiukwaji wa kisheria katika mahojiano.

“Ile kanuni ya mtu kuwa na haki hadi pale inapothibitishwa bila shaka yoyote kuwa ana hatia haizingatiwi, licha ya Katiba na Sheria zetu kusisitiza hilo; hii ndio inanifanya niendelee kusisitiza suala la utii wa sheria na Katiba kama nyenzo ya kuboresha taasisi zetu za haki jinai,” alisema Wakili Kangile.

Wakili Jebra Kambole, alisema anaona wajumbe wengi ni watu wa mfumo na hakuna ushirikishwaji wa asasi zisizo za kiserikali na watu wa magereza pia hawajashirikishwa vya kutosha.
“Sisi tukiitwa tutatoa maoni kwa sababu tuna nia ya kurekebisha mfumo wa haki jinai” alisema

Mhadhiri mwandamizi kitivo cha sheria Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Dk Elifuraha Laltaika kwa upande wake ameeleza ana imani kubwa na tume hiyo, akisema imesheheni watu wenye uzoefu mpana katika sekta ya Haki Jinai.


NGO zaja na mapendekezo

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu ya Uraia na Msaada wa Kisheria (CILAO), Odero Charles Oderos, alisema anapongeza nia ya Rais kuunda Tume kwa ajili ya utafiti kuhusu mfumo wa Haki Jinai ambayo imekuwa kero kubwa nchini.

Hata hivyo, Oderos alisema changamoto anayoona ni kwamba Tume hii sio shirikishi kwa maana kwamba haijabeba wadau muhimu wa mfumo wa haki jinai, akisema alitegemea aone wadau ambao ni NGO’s kama LHRC na THRDC .

Oderos alisema anapendekeza Tume hii ikutane na wadau mbalimbali na kwa uwazi zaidi kama ilivyokuwa Tume ya Jaji Warioba wakati wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya kwamba itasaidia kupata maoni na hali halisi.

“Mimi nipendekeze kwa mojawapo ya maboresho iwe ni makosa yote yawe na dhamana na pia kuwe na chombo cha kusimamia utendaji wa Jeshi la Polisi,” alisema na kusisitiza hiyo italifanya Jeshi la Polisi lisijitizame lenyewe.

Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Ofisi ya Arusha, Wakili Hamis Mayombo, alisema Tume imekuwa ya kiserikali zaidi, wengi wa wajumbe waliokuwepo kwenye mfumo unaolalamikiwa ndio haohao wameteuliwa.

Mayombo alisema baadhi ya wajumbe wa Tume ni hao hao walijenga mfumo uliopo ambapo Mwenyekiti wa tume, Jaji Chande alipokuwa Jaji Mkuu alikuwa na fursa ya kuleta mabadiliko na kuboresha haki jinai, lakini hakufanya hivyo.

“Nilitarajia wajumbe wa tume watoke pia taasisi binafsi, pia wawepo wajumbe ambao tayari waliathirika na mfumo wa haki jinai wangesaidia sana,” alisema.

Mkurugenzi wa shirika la wanahabari la kupiga vita dawa za kulevya na uhalifu (OJADACT), Edwin Soko, alisema anaheshinu uteuzi kwa kuwa ni mamlaka ya kiti cha Rais, ila akakosoa mfumo wa uteuzi kuingiza wajumbe wenye doa.

Soko alisema Tanzania imekuwa na shida kwenye uteuzi, katiba yetu imempa mamlaka hayo Rais lakini hakuna mfumo maalumu juu ya teuzi.

“Mfano Tume ya uteuzi ambayo ingekuwa na wajibu wa kufuatilia na kuchunguza sifa za wajumbe, kasoro hii inasababisha watu wenye kasoro kuteuliwa na inaondoa umakini,” alisema na kusisitiza uteuzi unafanyika kwa majina yale yale.


Wananchi nao watoa ya moyoni

Mjasiriamali Fredrick Mumburi, alimpongeza Rais Samia walau kuona kuna tatizo katika mifumo ya haki jinai, lakini hata hivyo alisema Tume hiyo inakosa watu wenye mawazo huru na kupendekeza Rais angetafuta sura mpya.

“Tunampongeza sana Rais wetu anafanya kazi nzuri sana na ana nia njema, ila katika Tume hii angepata sura mpya na watu ambao wanajua madhara ya kukosa haki zao nadhani ingesaidia sana. Sio waliotengeneza tatizo,” alisema.

Jumanne Saria, mkazi Hai mkoani Kilimanjaro, alitaka Rais kuwaingiza katika tume viongozi wa dini, watu waliofungwa kimakosa na kuwaondoa baadhi ya wajumbe kama wakuu wa polisi wastaafu ambao nao ni sehemu ya waliotengeneza tatizo.

Neema Lukumay, mfanyabiashara jijini Arusha, alisema uamuzi wa Rais Samia kuunda Tume ni wa kupongeza na akawataka wanaobeza baadhi ya wajumbe waache na kusisitiza kuwa yeye hana shida na muundo huo wa wajumbe.

“Mimi binafsi sina shida na wajumbe wote, kwani ni watu makini na wanajua vizuri changamoto za haki kwa sababu walikuwa serikalini kwenye nafasi mbalimbali, naomba tuwape muda wafanye kazi waliyotumwa na Rais,” alisema.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Mussa Juma (Arusha) na Peter Saramba (Mwanza).