Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhusiano wa ngono na UTI kwa wanaume

Muktasari:

  • Wakati wanaume wakitajwa kuwa si waathirika wakubwa wa UTI ukilinganisha na wanawake, wanashauriwa kuepuka ngono zembe kwa kutumia kondomu wakati wa kujamiiana

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa wanaume (UTI) asilimia kubwa husababishwa na kutokutumia kinga wakati wa tendo la kujamiiana.

Hayo yameelezwa siku moja tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ataje ugonjwa huo kuwa miongoni mwa magonjwa 10 yaliyotesa Watanzania kwa kipindi cha mwaka 2023.

Takwimu zinaonyesha UTI ni ugonjwa wa pili kuleta athari kwa idadi ya Watanzania milioni 4.09 sawa na asilimia 15.8 ukitanguliwa na magonjwa ya mfumo wa hewa yaliyoathiri watu milioni 4.9.


Takwimu hizo, zinaashiria ukubwa wa tatizo huku wataalamu wa afya wakishauri hatua zaidi zichukuliwe kwa jamii kujikinga ili kuondokana na magonjwa hayo ambayo huathiri figo.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Januari 11, 2024 Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa wanaume, kutoka kitengo cha Urolojia Hospitali ya Taifa Muhimbili, Steven Kaali amesema si rahisi kwa wanaume kupata UTI ikilinganishwa na wanawake.

Amesema licha ya kwamba wanaume wanaugua magonjwa hayo, lakini asilimia kubwa husababishwa na njia ya ngono kwa kuwa UTI ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kwa njia hiyo.

“Mwanaume anaweza kupata kutoka kwa mwanamke kwa sababu ni magonjwa ya kuambukiza hii ni tofauti na mwanamke ambaye yeye kimaumbile ni rahisi kupata UTI,” amesema.

Dk Kaali ameshauri wanaume kutulia katika uhusiano au kuwa na tabia ya kutumia kinga ili kujiepusha na maambukizi.

“Mwanamume anatakiwa awe mtaratibu kwenye maisha yake, awe msafi vyoo vya jamii asipende kuvitumia na akilazimika kutumia viwe katika hali ya usafi, kwani shughuli za kawaida kujisaidia wao husimama tofauti na wanawake.

“Pia, tabia za kujamiiana basi awe mtaratibu katika eneo hilo, kama yupo na mtu wake atulie na kama ameoa yupo na mkewe naye awe mtaratibu asiwe kiruka njia,” amesema Dk Kaali.

Alipoulizwa iwapo mabwawa ya kuogelea ‘swimming pool’ yanasababisha maambukizi, Dk Kaali amesema, “inaweza kuwa chanzo iwapo watu wanatabia ya kukojoa humo lakini sina uhakika sana na hilo.”


Dk Kaali amesema maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa wanaume huhusisha figo, kibofu cha mkojo, mrija wa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo pamoja na mrija unao unganisha figo na kibofu cha mkojo.


Kwanini nadra mwanamume kuugua UTI

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa mwanaume, Dk Erasto Wambura anafafanua kuwa mtoto yeyote bila kujali jinsia anavyozaliwa huwa katika hatari ya kupata maambukizi hayo.

Amesema hali ni tofauti kwa mtoto wa kiume kwa kuwa anapofikisha umri wa miaka mitatu wengi wao huwa wameshafanyiwa tohara, hivyo tatizo hilo huondoka kwao na hubaki wachache wanaoandamwa na maradhi hayo hasa wale ambao bado hawajapitia tohara.

Hata hivyo, Dk Wambura amesema kwa watoto wa kike hali hiyo huendelea kwa kipindi chote kulingana na maumbile yao, usafi hasa ikilinganishwa na njia ya mkojo na haja kubwa kukaribiana hivyo asipojua namna ya kujifanyia usafi anaweza kupata maambukizi mara kwa mara.

“Mwanamume pia njia yake ni ndefu ukilinganisha na mwanamke ambaye njia yake ni fupi kwa sentimita tano, mwanaume yeye kutoka nje katika njia ya mkojo mpaka kufikia kibofu umbali wake ni sentimita 16, hii inakuwa ni sababu mojawapo ya kuwafanya wanawake kuathirika zaidi,” amesema.

Amesema bado wanaume hupata maambukizi na kupatiwa matibabu ya kawaida isipokuwa wachache huumwa sana hasa wale ambao wana matatizo katika njia yao ya mkojo.


Maambukizi hayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na bakteria jamii ya E. coli, lakini katika mazingira machache fangasi na virusi wanaweza kuwa chanzo cha maambukizi hayo.

Dalili, athari za UTI   kwa mwanamume

Wataalamu wametaja dalili na UTI kwa mwanamume kuwa ni pamoja na kusikia maumivu wakati wa kukojoa, homa na maumivu katika viungo vya mkojo, kuhisi kuhitaji kukojoa mara kwa mara na pia mkojo kuwa na hali ya kuunguza wakati wa kukojoa.

Dalili zingine ni pamoja na maumivu ya tumbo chini ya kitovu au mgongo kwa chini na mkojo wenyewe unaweza kuonekana una ukungu, damu au usaha.

Madhara ya UTI kwa mwanamume ni figo kushindwa kufanya kazi na hii hutokana na bakteria kushambulia figo, magonjwa ya kibofu cha mkojo kama vile kibofu cha mkojo kuziba, kushindwa kukojoa hali ambayo hupelekea mgonjwa kukojoa kwa mrija.


Athari zingine ni maumivu ya mgongo, kiuno na nyonga, kupoteza hamu ya tendo la ndoa na UTI sugu.


Sababu wanawake kuugua UTI

Kwa wanawake, maambukizi ya njia za mkojo ndiyo hutokea mara nyingi zaidi katika aina zote za maambukizi ya bakteria. Asilimia 10 ya wanawake hupata maambukizi ya njia za mkojo kila mwaka.

Dk Wambura amesema kwa upande wa wasichana huanza kupata maambukizi zaidi wanapofikia katika umri wa kuanza kujamiiana na hapo huwa katika hatari zaidi ingawaje maambukizi ya UTI kwa kundi hilo hayasababishwi na njia ya ngono pekee.

“Katika tendo lile kunakuwa na ukaribisho kutoka sehemu moja kwenda nyingine hivyo usafi usipozingatiwa ni rahisi zaidi kupata maambukizi na ndiyo maana huwa tunashauri mwanamke akojoe mara baada ya tendo la ndoa.

“Kwa mwanamume kuna bakteria wanaoweza wakatembea kupitia njia ya damu akaja kwenye njia ya mkojo ni mara chache sana wanapita ila kwa wanawake wanakuwa na hatari kubwa kutokana na maumbile yao yalivyo,” amesema.


Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Living Colman amesema UTI haiambukizi isipokuwa tendo linachochea mwanamke akapata zaidi.

“Mke na mume wanaweza wasiambukizane pia UTI sanasana anaathirika zaidi mwanamke kama hatakuwa makini kwa usafi kwa kuwa mwanamke kibofu chake kipo jirani na mwanamume ni mbali sana.”

Dk Colman amesema maambukizi katika njia ya mkojo yakiwa sugu yanaweza kuleta madhara kwa kuwa huanzia nje kabisa kwenye kibofu na baadaye huanza kupanda katika mrija wa mkojo mpaka kwenye figo na kama mtu akikaa na maambukizi hayo kwa muda mrefu anaweza kupata magonjwa ya figo.

“Nyakati zingine yanaweza kuwa mawe kwenye njia ya mkojo, ikiziba wadudu wanazaliwa mara kwa mara hata ukitumia dawa lazima uone UTI imebaki, kina mama kuanzia miaka 45 tundu lao la mkojo linapungua hivyo husababisha mkojo kubaki kwenye kibofu kila wakipima wanaona ana UTI kinachofanyika tunatanua tundu na ndiyo matibabu yake,” amesema.

Dk Colman amesisitiza kuwa UTI inapokuwa sugu, maambukizi ya figo yanaweza kufuatia baada ya maambukizi ya njia ya mkojo.