Upepo wa kisiasa Afrika wabadilika

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir (mwenye fimbo) akisalimiana na Makamu wake, Riek Machar mjini Juba, Sudan Kusini siku chache baada ya kufikia makubaliano ya kumaliza tofauti zao. Awali, Machar aliikimbia nchi hiyo walipoto-fautiana na kwenda kuishi nchini Afrika Kusini. Picha na maktaba

Muktasari:

  • Tukio la karibuni zaidi ni la juzi, wakati Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe alipomuwekea dhamana kiongozi wa upinzani nchini humo, Tendai Biti baada ya kutiwa mbaroni na polisi. Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir kutangaza kuwasamehe waasi akiwamo aliyekuwa Makamu wake wa Rais, Riek Machar.

Dar es Salaam. Kuna wimbi jipya linaibuka katika mataifa mengi ya Afrika hivi sasa hususan katika masuala ya kisiasa. Viongozi wengi wamekuwa ama wakitoa msamaha kwa wapinzani wao au kupata nao, jambo ambalo awali lilionekana kuwa gumu kutekelezeka.

Tukio la karibuni zaidi ni la juzi, wakati Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe alipomuwekea dhamana kiongozi wa upinzani nchini humo, Tendai Biti baada ya kutiwa mbaroni na polisi. Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir kutangaza kuwasamehe waasi akiwamo aliyekuwa Makamu wake wa Rais, Riek Machar.

Kadhalika, Februari, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dk Abiy Ahmed alikutana na kufanya mazungumzo na chama cha upinzani cha ODF na kuahidi kushirikiana.

Aidha, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alikutana na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga mnamo Machi na kuombana radhi kwa lengo la kuijenga Kenya mpya.

Nchini Ivory Coast nako, siasa za uhasama zimeondoshwa baada ya Rais Alassane Ouattara kumsamehe Simone Gbagbo, mke wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo aliyefungwa kutokana na mzozo wa kisiasa wa baada ya uchaguzi mwaka 2011.

Mnangagwa na Biti

Hatua ya Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe kuingilia Mahakama iliyoamuru kiongozi wa upinzani nchini humo, Tendai Biti kukamatwa inaweza kulaumiwa, lakini kwa upande mwingine imeendeleza mtindo wa viongozi wa Afrika kutafuta suluhu na wapinzani wao.

Rais Mnangagwa ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter hatua hiyo akisema lengo lake ni kutaka kuwa na amani huku pia akisisitiza taratibu zaidi za kisheria zitafuata mkondo wake.

Biti ambaye ni kiongozi wa chama cha MDC alikamatwa akidaiwa kuutangazia umma wa Zimbabwe kuwa chama hicho kimeshinda uchaguzi wa hivi karibuni, kitendo kinachotajwa kuchochea vurugu kwa wananchi.

Biti aliyejaribu kutorokea nchini Zambia alirejeshwa na vyombo vya usalama ili kukabiliana na kesi yake hiyo.

Kurejeshwa kwake kulitokana na agizo la Mahakama la kumtafuta popote alipo, baada ya tamko alilolitoa la ushindi wa chama cha upinzani kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika hivi majuzi na kumuweka madarakani mwanasiasa Mnangagwa.

Kiongozi huyo ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa na waziri wa zamani wa fedha kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa na Rais wa zamani, Robert Mugabe na aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Morgan Tsvangirai.

Ushindi wa Rais Mnangagwa dhidi ya mpinzani wake, Nelson Chamisa wa MDC umehojiwa kutokana na kasoro zilizojitokeza hasa za Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kuchelewesha matokeo jambo lililosababisha vurugu jijini Harare.

Kenyatta na Odinga

Hatua ya Rais Mnangagwa kumwokoa Biti inatajwa kuwapoza wapinzani wanaolalamika kuporwa ushindi wao.

Hatua hiyo pia imefanana na mapatano yaliyofikiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga Machi mwaka huu.

Awali wawili hao walifarakana katika uchaguzi mkuu uliokuwa na upinzani mkali ambapo licha ya Rais Kenyatta kushinda, alipingwa mahakamani na kuamriwa kurudiwa Oktoba 26, 2017.

Hata hivyo, Raila aliyekuwa kiongozi wa muungano wa Nasa alisusia uchaguzi huo na kupinga matokeo yaliyomrudisha Rais Kenyatta madarakani jambo lililopingwa na Mahakama.

Baada ya kuona ameshindwa, Raila naye aliamua kujiapisha Januari 30, 2018 na kuzidisha utata zaidi.

Hata hivyo, baada ya miezi miwili ya misimamo mikali kutoka kwa chama cha Jubilee na muungano wa Nasa, Rais Kenyatta na Raila walifanya mkutano wa ghafla Ijumaa, Machi 5 katika jumba la Harambee, wakikubaliana kuweka tofauti zao kando na kuliunganisha Taifa.

Miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni pamoja na kushirikishwa kwa watu wote kunastahili kuimarishwa ili kuiuza Kenya zaidi na kuinua udhabiti wake kiuchumi.

Walikubaliana pia kushirikiana katika masuala ya usalama na hasa janga linalowakabili la ugaidi kutoka kwa kundi la Al-Shabaab la Somalia.

Kuhusu ufisadi, Rais Kenyatta na Raila walikubaliana kuwa kila mtu lazima achangie katika vita hiyo, wakiahidi kuwalinda wanaowafichua wafisadi.

Hata hivyo, walionya kuwa vita dhidi ya ufisadi isitumiwe kuwamaliza wengine au kufanyika kwa njia fisadi.

Vilevile walikubaliana kuhusu usawa ambapo, Rais Kenyatta na Raila walizitaka serikali zote za kaunti kuhakikisha kuwa watu wote wanafaidi kutokana na miradi iliyopo ili kuwaondoa raia kutoka katika umaskini

Kuhusu haki za binadamu, Uhuru na Raila walikubaliana kuwa Wakenya wana haki za kibinadamu na za kiraia na kuwa, haki hizo hazistahili kukiukwa na Mkenya yeyote.

Raila atakuwa na ofisi na washauri ambao watamsaidia kuafikia ajenda zao baada ya kuzindua mpango huo rasmi.

Dk Ahmed na wapinzani Ethiopia

Mbali na Kenya, nchini Ethiopia kulitokea mabadiliko ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn alijiuzulu Februari mwaka huu na nafasi yake kushikiliwa na Dk Abiy Ahmed ambaye ameleta mageuzi makubwa.

Tofauti na Desalgn aliyekuwa na misimamo mikali dhidi ya wapinzani, Dk Ahmed amefanya mazungumzo na chama cha upinzani cha ODF wakiahidiana kushirikiana.

Dk Ahmed alikutana na wawakilishi wa chama cha upinzani kilichokuwa kinafanya shughuli zake uhamishoni cha Oromo Democratic Front (ODF) baada ya chama hicho kukubali kushiriki mjadala wa siasa za Ethiopia kwa amani.

Katika taarifa yake ya Mei 13, ODF ilithibitisha kwamba ilifikia makubaliano na Serikali baada ya kufanya mazungumzo katika eneo ambalo halikuwekwa wazi ili warudi nyumbani washiriki katika mchakato wa kidemokrasia.

Viongozi wa ODF wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Front Lencho Leta waliwasili jijini Addis Ababa hivi karibuni ambapo, Leta alimwambia mwanahabari kwamba matokeo ya mazungumzo yamewezesha ODF kushiriki siasa za Ethiopia. “Kwa kuzingatia masharti na namna mazungumzo na Serikali yatakavyokuwa, ODF itaamua kufanyia shughuli zake za kisiasa katika ardhi ya Ethiopia na kuanzisha muungano na vyama vingine vya siasa,” alisema Leta.

Shirika la Utangazaji la Serikali la Fana BC liliripoti kwamba pande zote mbili zimekubaliana kufanya kazi pamoja ili kujenga umoja wa Taifa na kuimarisha mchakato wa kidemokrasia.

Leta aliongeza kwamba chama chake kimekubali kurudi nchini baada ya kuridhishwa na mchakato wa mageuzi ya demokrasia yanayoendelea.

Mbali na kushirikiana na wapinzani, Waziri Mkuu Ahmed amewafungulia gerezani waliokuwa wafungwa wa kisiasa na kuondosha siasa za uhasama.

Rais Ivory Coast asamehe

Nchini Ivory Coast nako, siasa za uhasama zimeondolewa baada ya Jumatano iliyopita, Rais Alassane Ouattara kumsamehe Simone Gbagbo ambaye ni mke wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo aliyefungwa kutokana na mzozo wa kisiasa wa baada ya uchaguzi mwaka 2011.

Gbagbo anashikiliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC mjini Hague, Uholanzi

Mwanamama huyo aliyefahamika nchini kama “mwanamke shupavu” ni miongoni mwa wafungwa 800 waliosamehewa na Rais Ouattara siku ya mkesha wa sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Ivory Coast.

Rais Outtara amesema hatua hiyo ni harakati za kitaifa za kuhubiri msamaha na mshikamano wa Taifa hilo la Afrika Magharibi.

Mwanamama huyo alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela kutokana na hukumu ya mwaka 2015 kwa kosa la “kuhatarisha usalama wa Taifa.”

Hatua hiyo imeonekana kuongeza juhudi za kuijenga upya nchi hiyo tangu ulipozuka mzozo wa baada ya uchaguzi.

Mbali ya Simone, mtu mwingine mashuhuri aliyenufaika na msamaha huo ni aliyekuwa msaidizi mwandamizi wa Spika wa Bunge, Guillaume Soro.

Kiir na Machar Sudan Kusini

Hivi karibuni pia Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amefanya mapano na mpinzani wake aliyekuwa makamu wake, Riek Machar baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ya muda mrefu.

Makubaliano hayo yametangazwa hivi karibuni na televisheni ya Taila la nchi hiyo ambapo Rais Kiir na kiongozi wa SPLM-IO, Machar walitia saini kusitisha mapigano katika mji mkuu wa Khartoum nchini Sudan.

Ugomvi wa makundi hayo ulianza mwaka 2013 na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu uku wengine wakikimbilia nje ya nchi hiyo.

Vilevile, Rais Kiir amemsamehe Machar makosa mengine aliyokuwa amefunguliwa akiwa uhamishoni yakiwamo ya kuchochea vurugu nchini humo.

Mtazamo wa msomi

Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Hamad Salim amesema licha ya viongozi hao kuwaweka karibu wapinzani wao, bado wanahakikisha vyama vyao vinaendelea kutyawala dhidi ya wapinzani.

‘Ni kweli siasa za upatanisho kati ya vyama tawala na vyama vy upinzani zimeshika kasi barani Afrika, lakini vyama tawala bado vinahakikisha vinaendelea kushika dola,” anasema Dk Hamad.

Hata hivyo amekosoa hatua za marais kuingilia Mahakama na kuwasamehe viongozi wa upinzani kwa lengo hilo.

‘Kama tayari kuna Bodi ya Parole inayoamua nani apunguziwe adhabu, Rais anapata wapi mamlaka ya kuingilia mamlaka ya Mahakama? Mimi naamini wanafanya hivyo ili tu kupata umaarufu na kuongeza wafuasi,” anasema.