‘Upigaji’ Hazina waibua kiu ukaguzi maalumu

Rais Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere wakati akitolea maelezo taarifa zake za ukaguzi kwa mwaka 2019/2020 Ikulu ya Chamwino, Dodoma. Picha na Maktaba

Muktasari:

 Ubadhirifu wa fedha za umma uliofichuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Wizara ya Fedha umeongeza kiu ya wananchi kutaka kujua ulipofikia uchunguzi ambao Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza ufanyike katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Dar es Salaam. Ubadhirifu wa fedha za umma uliofichuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Wizara ya Fedha umeongeza kiu ya wananchi kutaka kujua ulipofikia uchunguzi ambao Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza ufanyike katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mei 28, mwaka huu Majaliwa aliwasimamisha kazi watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango ambao wametafuna zaidi ya Sh1.67 bilioni kati ya Machi 31 na Mei mwaka huu kwa ajili ya posho na malipo mengine yasiyo na tija.

Waliosimamishwa kazi ni pamoja na mkaguzi mkuu, mkaguzi msaidizi na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo, sasa wamepisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Ubadhirifu huo umetokea wakati tayari Rais Samia akiwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kufanya ukaguzi maalumu wa fedha zote zilizotoka BoT kati ya Januari na Machi mwaka huu.

Machi 28, Rais Samia alipokea ripoti ya CAG pamoja na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na akaziagiza taasisi hizo kufanya uchunguzi maalumu wa fedha zote zilizotoka BoT kwenda kwenye miradi ya maendeleo.

Licha ya Samia kutoeleza bayana kilichokuwa kikiendelea BoT, kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kwenye mitan[1]dao ya kijamii kwamba mamilioni ya fedha yalichotwa BoT kipindi ambacho Hayati John Magufuli alikuwa anaumwa mpaka alipofariki, Machi 17. Aprili 22 wakati akilihutubia Bunge, Samia aliwaonya baadhi ya watendaji wanaodhani usimamizi wa mali za umma, ukwepaji kodi, uzibaji wa mianya na kukemea wizi yameondoka kufuatia kifo cha kiongozi huyo akisema wanajidanganya.

Alisisitiza kwamba Hayati Magufuli amekwenda peke yake, Serikali bado ipo na mikakati na falsafa aliyoiachia inaendelea kufanya kazi. Mbali na kuagiza uchunguzi huo, Rais Samia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko, kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha bandarini na baadaye alimteua Eric Hamissi kujaza nafasi yake.

Rais Samia aliwaagiza Takukuru kushughulikia suala hilo kwa sababu ripoti ya CAG ilibainisha kwamba kulikuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma pale TPA. Mpaka sasa suala hilo liko mikononi mwa Takukuru wakiendelea na uchunguzi.

Wasomi wazungumza

Kufuatia hali hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Luisilie amesema matokeo ya uchunguzi huo maalumu ni muhimu kwa sababu bado kuna mianya inatumika kufanya ubadhirifu licha ya kwamba kuna viongozi katika taasisi husika.

Akizungumza na Mwananchi jana, Luisilie alisema pengine watendaji wameona kuna mabadiliko ya uongozi wa juu wakaona hiyo fursa yakufanya ubadhirifu.

Alishauri uchunguzi kama huo, mbali na kuwekwa hadharani, unatakiwa kufanyika pia kwenye taasisi nyingine. “Inawezekana kuna upenyo mkubwa wa matumizi ya pesa kwa sababu mpaka wamefikia hatua hiyo lazima kulikuwa na mianya. Kwa hiyo uchunguzi kama unaofanyika ni muhimu na wananchi tuambiwe yaliyojiri,” alisema.

Kuhusu ubadhirifu uliotokea wizara ya fedha, msomi huyo alisema watu wasipodhibitiwa watafanya mambo kinyume na matarajio ya wengi, hasa wananchi ambao wanategemea kupata huduma kutoka serikalini.

 Alisema kuna umuhimu wa kuwapa watumishi motisha ili kuimarisha utendaji, hasa katika kazi za ziada au kazi maalumu, lakini motisha hiyo ikizi kiwango inatakiwa kudhibitiwa kabla haijageuka kuwa ubadhirifu. “Baadhi ya watu hawajali, hawana uchungu na fedha za umma.

Hawajali kama kuna watu wanahitaji nyongeza ya mishahara, wanahitaji dawa hospitali,” alisema Dk Luisilie. Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Andrew Bomani alisema uchunguzi maalumu unaofanywa na CAG ni muhimu kwa sababu walipakodi wangependa kujua fedha zao zimetumikaje.

“Ripoti hiyo ikitoka, ningependa kuona waliohusika na ubadhirifu huo wanachukuliwa hatua za kisheria badala ya kuhamishwa au kupewa kazi nyingine,” alisema Bomani na kuongeza kwamba Rais Samia anatakiwa kuwa mkali katika mambo haya.

Mbali na matukio ya Hazina na Bandari, kumekuwapo na taarifa za ubadhirifu katika maeneo mbalimbali nchini na baadhi yake hatua kadhaa zimechukuliwa. Aprili 19, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Suzana Chaula baada ya kutoridhishwa na utendaji wake hasa katika kusimamia ukusanyaji wa mapato katika mradi huo.

Waziri Mkuu alikuta mifumo ya tiketi za kielektroniki katika miundombinu ya Dart haifanyi kazi badala yake wanatumia tiketi ambazo tayari zimechapishwa, jambo ambalo alisema linatoa mwanya wa upotevu wa mapato ya Serikali