Utashi wa kisiasa unavyokosesha hamasa katika chaguzi za marudio

Madiwani wa  Chadema mkoa wa Arusha, ambao wamekihama Chama hichohivi karibuni na kujiunga na CCM, wakitambulishwa kwa Rais  John Magufuli wakati wa sherehe  za kutunuku Kamisheni maafisa wapya JWTZ,   kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha jana. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Wimbi la wanasiasa wanaoviacha vyama vyao na kuanza maisha mapya ya kisiasa ndani ya Chama tawala (CCM) linaendelea kuwa kubwa huku wahamaji wakitoka sababu mbalimbali.

Umeshawahi kujiuliza kwa nini idadi ya wananchi wanaojitokeza kupiga kura inapungua kila mara na hasa katika uchaguzi mdogo? Je, nini kinatokea katika jamii pale mbunge wao au diwani waliyemchagua anahama chama na kurejeshwa kugombea tena palepale?

Wimbi la wanasiasa wanaoviacha vyama vyao na kuanza maisha mapya ya kisiasa ndani ya Chama tawala (CCM) linaendelea kuwa kubwa huku wahamaji wakitoka sababu mbalimbali.

Mhamaji wa hivi karibuni kabisa ni mbunge wa Liwale (CUF), Zuberi Kuchauka akitanguliwa na mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na yule wa Monduli, Julius Kalanga. Orodha ni ndefu ikihusisha wabunge na madiwani.

Kutokana na wimbi hilo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo anatabiri kuwa hamahama hiyo inayoendelea haitakuwa na matokeo chanya kwa mfumo wa demokrasia ya nchi na ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wake.

Zitto anaandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa hamahama hiyo mbali na kuwakasirisha wananchi na kuwafanya waichukie siasa, inaweza kuhatarisha hata amani na utulivu uliopo.

Ina ukakasi

Si Zitto pekee mwenye mawazo hayo, hata Nape Nnauye, mbunge wa Mtama (CCM) anasema matukio hayo yana ukakasi.

Katibu huyo wa zamani wa itikadi na uenezi wa CCM anapendekeza kwamba ikitokea mtu anahama chama, basi ahame na nafasi yake anayoishikilia iwe ni ubunge, udiwani au uwakilishi.

Hata hivyo, Katiba inasema kinyume chake, mtu anapohama uchaguzi unaitishwa upya na kufanya uchaguzi mwingine. Zaidi ni kwamba kumeibuka pia tabia ya kuwasimamisha walewale waliojiuzulu na kugombea tena kupitia vyama walivyohamia.

Ni kutokana na hali hiyo, idadi ndogo ya wanaojitokeza kupiga kura inahusishwa na matukio hayo.

Hadi sasa zaidi ya madiwani 100 na wabunge sita wamehama vyama vyao, wengi wakitokea upinzani kwenda CCM. Chama kikuu cha upinzani, Chadema, kimeathirika zaidi. Wabunge ambao wamehamia CCM mpaka sasa ni Kalanga, Waitara, Kuchauka, Dk Godwin Mollel (Siha), Maulid Mtulia (Kinondoni). Aliyetoka CCM kwenda upinzani ni Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini).

Sababu za kuhama vyama

Uchambuzi wa sababu zinazotolewa na wahamaji unaweza kubaini sababu kuu tatu. Kuna wale – kama Mtulia na Mollel pamoja na wengine wengi—ambao uhusisha uamuzi wao wa kuhamia kwao CCM na kuridhika na utendaji wa Rais John Magufuli.

Wengine, kama Waitara, wanadai kuhama kwao kumetokana na kulaumiwa ndani ya vyama vyao vya zamani pale wanapo shirikiana na serikali katika harakati za kuwaletea maendeleo wananchi wa majimbo yao. mKundi la tatu linaweza kuwa lile linalojumuisha watu kama Nyalandu ambaye alidai amejiunga na Chadema ili atoe mchango wake katika vuguvugu la kudai Katiba Mpya.

Kuna madai ambayo hata hivyo yamekanushwa, kwamba wale wanaohamia CCM huwa wananunuliwa.

Hata hivyo, mamlaka zinazohusika na rushwa, kama Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hazionekani kuchunguza kutafuta ukweli.

Alama zimeshajidhihirisha

Dalili zinazoashiria hasira ya wapiga kura zimeanza kujitokeza na kuonekana waziwazi kwenye chaguzi ndogo za majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido zilizofanyika Januari 13 mwaka huu ambapo ni idadi ndogo tu ya wapiga kura ilijitokeza.

Ni watu 110,883 pekee kati ya 278,167 waliojiandikisha kupiga kura katika majimbo matatu yaliyotajwa hapo juu ndiyo waliyojitokeza kupiga kura, huku kukiwa na watu 167,284 ambao hawakushiriki katika zoezi zima la kupiga kura: kiwango cha asilimia 60.14 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura.

Uchaguzi mdogo wa jimbo la Siha uliofanyika Februari 27 mwaka huu pia haukunusurika ambapo ni wapiga kura 32,277 (asilimia 58.35) tu kati ya watu 55,313 waliojiandikisha kupiga kura ndiyo waliyojitokeza.

Hasira za wapiga kura zilikuwa dhahiri pia katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni ambapo ni wapiga kura 45,454 (asilimia 17.2) pekee ya watu wote waliyojiandikisha kupiga kura ndiyo waliyojitokeza kupiga kura.

Hoja zinazojengwa

Watu mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na hali hii ya idadi ndogo ya watu kujitokeza kupiga kura huku wengine wakiitupia lawama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushindwa kuendesha uchaguzi unaoonekana wa haki.

Mwanasafu wa gazeti la The Citizen, Profesa Zulfiqarali Premji anaihusisha hali hiyo na kukata tamaa na hisia za kutokujali miongoni mwa wapigakura. Hii pia inahusisha mtazamo—wa kweli au wa uwongo—kwamba kura ya mtu haitaleta tofauti yoyote ya matokeo.

Vyovyote itakavyokuwa, Profesa Premji anaonya dhidi ya tabia ya wananchi kususia kupiga kura, akisema kwamba demokrasia ni fursa, na kura ‘iliyopotea’ ni kitu cha hatari sana.

Anasema, ukweli ni kwamba uhalali wa serikali iliyopo madarakani unaweza kuhojiwa na kuingia matatani endapo idadi ndogo ya watu hujitokeza kupiga kura.

Hata Mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anakubaliana na Profesa Premji akisema “Kuacha kupiga kura ni hatari si kwa wananchi tu, bali hata kwa serikali iliyopo madarakani. Serikali haitakuwa na uhalali wa kuongoza, wananchi, kwa upande mwingine, wataongozwa na sera ambazo hawajaziridhia.

“Wakati wananchi wanaweza kuwa wamepoteza haki yao ya kuwawajibisha viongozi wao, matokeo ambayo yanaweza kuutokea utawala usiokubalika yanaweza kuwa mabaya zaidi ya yale yanayoweza kuwapata wananchi,” anafafanua Mbunda.

Mawazo ya Mbunda hata hivyo yanapingana na yale ya mhadhiri mwingine wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Hamad Salim anayesema wananchi wanaweza kukasirishwa na hamahama ya vyama inayoendelea. Lakini, hadhani kama hiyo inaweza kuathiri Uchaguzi Mkuu unaokuja,” anasema.

Hamad anaeleza kwamba watu kususia kupiga kura ni kitu cha kawaida duniani kote, ingawaje “si afya.” Anasema si afya kwa sababu uchaguzi hutoa fursa kwa wananchi kuamua hatma ya nchi yao kwa kukubaliana au kutokukubaliana na sera zinazopendekezwa kwao na wanasiasa wa vyama tofauti.

Kwa hiyo, kama hatma ya nchi itaamuliwa na watu wachache basi walio wengi wanaweza kuishia kupata serikali isiyowahusu.

Kwenye suala la uhalali wa serikali, Hamad anakubali kwamba uchaguzi ambao watu wachache hushiriki unaweza kukosa uhalali wa kisiasa.

Hata hivyo, “kadiri muda utakavyo kuwa unaenda, uhalali unaweza kupatikana, kutegemeana na ni kwa namna gani uongozi uliopo madarakani unawagusa watu na maisha yao.”

Lakini, Mbunda hakubaliana na wazo hilo kwa kusema kwamba uhalali uliopotea hauwezi kurejeshwa na kwamba migogoro ya kijamii, fujo na hujuma, vinaweza kuwa ndio matokeo ya serikali haramu.

Anatetea hoja yake kwa kutoa wito wa juhudi za makusudi kuchukuliwa ili kuepuka vitu ambavyo vinaweza kuwakatisha watu tamaa na kuwafanya waache kupiga kura. Kushindwa kuweka hisia ya umiliki wa serikali iliyopo madarakani kunaweza kupelekea uasi, anaonya Mbunda.

Sheria za uchaguzi

Njia moja ambayo inaweza kupunguza hasira za wapiga kuhusu hamahama za vyama zinazoendelea inaweza kuwa ni ile iliyotolewa hivi karibuni na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) ambapo jukwaa hilo limependekeza kufanyika marekebisho katika sheria za uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Hebron Mwakagenda alinukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema kuwa Jukata “Inasisitiza haja ya viongozi wa kisiasa kuruhusiwa kuhama vyama bila ya kupoteza nafasi wanayoshikilia,” kama ni ubunge, uwakilishi na udiwani, hoja sawa na aliyoitoa Nape

Kwa upande mwingine, Profesa Premji anawaomba Watanzania kutokuacha kamwe kupiga kura haijalishi ni nini kinachoweza kuwashawishi kufanya hivyo.

Hii ni kwa sababu ni kupitia upigaji wa kura pekee ndiyo wananchi hupata nguvu ya pamoja na kuwalazimisha watawala wao kukubali aina ya ushirikiano ambao una manufaa kwa wote, anasema Profesa Premji.

Anaamini kuwa hiyo haitaweza kutokea kama hatua za makusudi hazitachukuliwa katika kuziunganisha nguvu za wananchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha taasisi za kidemokrasia.