Vifo vya Profesa Kanywanyi na mmiliki wa A to Z Arusha vyatikisa

Vifo vya Profesa Kanywanyi na Jayant Shah vyatikisa

Muktasari:

  • Profesa Kanywanyi anajulikana kwa kuwa mhadhiri wa muda mrefu wa sheria UDSM lakini aliwahi kushika nyadhifa serikalini hata sekta binafsi.

Dar/Arusha. Habari za kutokea kwa vifo vya watu wawili maarufu nchini akiwamo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam (UDSM), Profesa Emiritus Kanywanyi na mfanyabiashara maarufu Arusha, Jayant Shah, vilitikisa jana.

Profesa Kanywanyi anajulikana kwa kuwa mhadhiri wa muda mrefu wa sheria UDSM lakini aliwahi kushika nyadhifa serikalini hata sekta binafsi.

Shah kwa upande wake anakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa wamiliki wa viwanda vya A to Z na mwanamichezo wa mbio za magari.

Baadhi ya mawakili walizungumzia kifo cha Profesa Kanywanyi wamesema tasnia ya sheria imempoteza nguli.

Profesa Kanywanyi aliyezaliwa Novemba mwaka 1938 alifariki dunia usiku wa kuamkia jana saa 7:00 katika Hospitali ya Kairuki alikokuwa akipata matibabu.

Kwa mujibu wa Profesa Frederick Kaijage, msemaji wa familia ya marehemu, mwili wa Profesa Kanywanyi unatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Heshima za mwisho zinatarajiwa kutolewa katika ukumbi wa mikutano wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alisema Profesa Kaijage jana.

Wakizungumza na gazeti hili nyumbani kwa marehemu, baadhi ya mawakili waliofundishwa na nguli huyo wa sheria walisema tasnia hiyo imempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa moja kwa moja katika utendaji kazi wake.

“Nitamkumbuka Profesa Kanywanyi kwa namna alivyoandaa andiko lake la PhD hadi chuo kikuu kikatunga kanuni za kuwataka wengine wasiandike andiko refu. Pamoja na kutufundisha, alikuwa mshauri elekezi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na alikuwa kiongozi kwa nyakati tofauti,” alisema wakili Julius Mutabazi.

Wakili huyo alisema marehemu alisimamia maadili na alisononeka mawakili wakituhumiwa. Kwa muda mrefu, alisema alikuwa mdhamini wa mfuko wa mawakili wanaofariki.

Wakati Dk Mutabazi akieleza hayo, wakili Bernard Mbakileki alisema enzi za uhai wake Profesa Kanywanyi hakuwa mjeuri wala mwenye majivuno.

“Wengi tumejifunza kutoka kwake, nakumbuka mwaka 1966 tulionana chuoni mlimani wakati akianza kufundisha. Mwaka 1999 tulianzisha kampuni ya uwakili na Profesa Kanywanyi alikuwa mwenyekiti wetu hadi umauti unamkuta, ni hazina kubwa,” alisema Mbakileki.

Enzi za uhai wake, Profesa Kanywanyi aliwahi kuwa msimamizi wa nje wa kitivo cha sheria wa Chuo Kikuu cha Haile Selassie nchini Ethiopia, Chuo Kikuu Cha Nairobi (Kenya), Makerere (Uganda), Shule ya Sheria Zambia, Idara ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Zimbabwe na Chuo Kikuu cha Swaziland.

Mbali na hilo, Profesa Kanywanyi aliwahi kuhudumu katika taasisi mbalimbali ikiwamo kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mjumbe tume ya huduma za mahakama.

Pia alifanya kazi kama kaimu jaji wa mahakama ya rufaa kati ya mwaka 1993-1994 na mwaka 1998-2000 alikuwa rais wa mahakama ya Comesa (Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika). Alikuwa wakili wa Mahakama Kuu tangu mwaka 1978 na alibobea kwenye sheria ya mabenki, bima na hifadhi za jamii.

Katika hatua nyingine, mkurugenzi wa viwanda vya A to Z, Shah alifariki dunia jana wakati akitibiwa jijini Nairobi nchini Kenya.

Shah, aliyeacha mke na watoto watatu, alikuwa mwanzilishi na mmoja wa wamiliki wa viwanda vikubwa viwili vya A to Z ambavyo vimetoa ajira kwa zaidi ya vijana 5,000 jijini Arusha.

Awali Shah alikuwa akimiliki viwanda hivyo na mdogo wake, Anold Shah aliyefariki mwaka 2016.

Meneja wa viwanda hivyo, Binesh Harria alisema taarifa rasmi za msiba huo zitatolewa na familia yake.

Viwanda viwili vya A to Z vinaongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengi mkoani Arusha .

Viwanda hivyo hutengeneza vifaa mbali mbali ikiwepo vyandarua na nguo.

Kiwanda cha A to Z cha Kisongo kiliwahi kupewa zabuni kupitia mfuko wa kimataifa wa Global Fund kutengeneza vyandarua vyenye dawa na kusambazwa nchi mbalimbali duniani katika vita ya kukabiliana na ugonjwa wa malaria.