Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Vilio’ vyatawala vifaa vya shule kupanda bei

Muktasari:

  •  Muhula mpya wa masomo kwa mwaka 2024 utaanza Januari 8 huku baadhi ya wazazi na walezi wakikutana na changamoto ya bei za vifaa vya shule kupanda bei

Dar es Salaam.  Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari nchini, vilio vya kupanda kwa baadhi ya vifaa vya shule vimesikika kutoka kwa wazazi na walezi.

Wakati wazazi wakilia, wauzaji nao wanalia kukosa wateja kutokana na bei kuongezeka huku wakibainisha hali hiyo imechochea kushuka kwa uwezo wa kununua bidhaa kwa wananchi.

Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanatarajia kuanza muhula mpya wa masomo Jumatatu ya Januari 8, 2024 huku ukiwa umebeba siku 59 za masomo kabla ya kwenda likizo fupi Machi 28, 2024.

Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti wakati Mwananchi ilipokuwa ikipita katika Soko la Kariakoo, Dar es Salaam kuangalia mwenendo wa biashara ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa masomo.

Januari ya kila mwaka hutajwa kama msimu mpya wa masomo kutokana na wanafunzi wapya ikiwamo wa awali na darasa la kwanza na wale wa kidato cha kwanza kuanza safari yao ya elimu.

Alipozungumza na Mwananchi, Zagallo Msangi ambaye ni mfanyabiashara mdogo katika Soko la Kariakoo amesema kupanda kwa bei ya jumla katika baadhi ya bidhaa ikiwamo sare za shule kumefanya baadhi ya wazazi kupunguza kiwango cha ununuzi wanayofanya.

"Mfano mashati ya watoto wadogo kabisa tulikuwa tunanunua Sh2,300 kwa moja hata nikija kuuza Sh5,000 haikuwa mbaya lakini sasahivi tunanunua hadi Sh3,800 huwezi kuuza bei ileile," amesema Msangi.

Amesema hali hiyo imefanya wazazi badala ya kununua mashati mawili hadi matatu na wengine matano kama ilivyokuwa zamani sasa wananunua moja.

Bei ya mashati ya shule katika soko la Kariakoo yanategemeana na aina, uzito na hivyo kufanya bei sasa kuwa kati ya Sh5,000 hadi Sh7,000 tofauti na zamani mashati hayo ya mikono mifupi yaliuzwa Sh5,000.

Pia, wauzaji hao wanapanga bei kulingana na mzigo aliochukua kwa kuwa kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kuchukua kwa jumla wamekuwa wakinunua kwa wenzao kwa bei hadi ya Sh4,500 kwa shati moja.

Mbali na sare pia viatu kwa ajili wanafunzi navyo vimegeuka kilio kwa wazazi kwa kuwa ili mwanafunzi apate kilichokuwa bora wanalazimika kuingia mifukoni zaidi.

"Mwezi wa kumi hiki kiatu kilikuwa Sh10,000 leo Sh16,000 hata nguvu za kujitetea unakosa maana hela uliyokuja nayo ni tofauti na unachoambiwa. Unajua sisi wamama ukijua bei ni Sh10,000 unajipanga na pungufu ili ukijitetea ndiyo iangukie kwa bajeti," amesema Asha Khalid Mkazi wa Keko.

Akiwa mama wa watoto watatu anaeleza ongezeko la bei linamfanya akose namna ya kuhakikisha wanawe wote wanapata wanavyohitaji ikiwemo sare, mabegi na hata vifaa vya kujifunzia.

"Hizo begi ndiyo basi tena kuanzia Sh20,000 ndiyo unapata angalau linaweza kudumu miezi sita vinginevyo bei rahisi kila baada ya miezi mitatu ununue,” amesema.

Haya yanasemwa wakati ambao wanafunzi milioni 1.09 wamepangiwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari nchini ikiwa ni baada ya kufanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2023.

Hali hiyo imefanya wazazi kukosa chaguo bali kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto wao kuanza ngazi hiyo ya masomo.

"Nisingekuwa na sababu ya kununua hizi sare kama angekuwa anaendelea darasa linalofuata, hata hivyo hatapata vitu vyote alivyokuwa anahitaji kutokana na bajeti kubana," amesema Miriam Mziwanda mkazi wa Kigogo.

Anasema mwanaye aliyechaguliwa Shule ya Bweni Kibaha mkoani Pwani hatopata tena shati tatu kama alivyohitaji na badala yake atapata mbili ili aweze kupata jozi mbili za viatu.

"Bei, hapa alipo tu ameshachelewa kuripoti shule tukisema tuendelee kusubiri atachelewa zaidi bora apate kilichopo," amesema Miriam.