Vita ya ukoma bado mbichi mikoa tisa
Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk Deus Kamara.
Muktasari:
Maambukizi ya Ugonjwa wa Ukoma yamepungua kutoka wagonjwa 40,000 kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita hadi kufikia 1,705 kwa mwaka 2022
Dodoma. Serikali imesema licha ya maambukizi ya ukoma kupungua kutoka visa vipya 40,000 miaka 40 iliyopita hadi 1,705 mwaka 2022, bado mikoa tisa ina maambukizi ya ugonjwa huo.
Mikoa hiyo kwa mujibu wa Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kuthibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk Deus Kamara ni Dodoma, Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Lindi, Mtwara, Geita, Kigoma na Pwani.
Akizungumza na wanahabari kuhusu mpango wa Serikali wa kutokomeza ugonjwa huo nchini, leo Jumamosi Januari 27, 2024 jijini Dodoma, Dk Kamara ametaka juhudi zifanyike kwa mikoa tajwa ili kumaliza ugonjwa huo.
“Pamoja na hamasa inayotolewa lakini bado kuna mikoa ambayo maambukizi ya ukoma kwa wastani wa wagonjwa 50 hadi 200 kwa mwaka, hivyo tumeiagiza mikoa hiyo kuhakikisha inaweka juhudi za kudhibiti ugonjwa huo,” amesema Dk Kamara.
Ameitaka mikoa yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa ukoma, kutoa elimu kwa wananchi, kuwafuatilia wagonjwa nyumbani na kutoa tiba kinga kwa watu ambao wameshirikiana na mgonjwa wa hao.
Dk Kamara amesema kuna juhudi zinafanywa na Serikali za kuwatibu watu wenye dalili au wanaoumwa ukoma, lengo likiwa ni kuutokomeza kabla ya kufika mwaka 2030.
“Sasa hivi tuna kampeni maalumu ya kutoa hamasa kwa jamii kuhusu Ugonjwa wa Ukoma ikiwa ni pamoja na kuwafuata wagonjwa hao nyumbani na kama itatokea tunawapata wagonjwa tunatoa tiba kinga kwa watu alioshirikiana nao ili kuwakinga wasipate ugonjwa huo,” amesema Dk Kamara.
Dk Kamara ametoa tahadhari juu ya dhana potofu iliyojengeka katika jamii kuwa Ugonjwa wa Ukoma ni wa kurithi, kulogwa au laana akisema unaambukizwa kwa njia ya hewa, hivyo ni rahisi kwa watu wa familia moja kuupata kwa sababu ya kushirikiana na mtu mwenye maambukizi.
Daktari Mshauri kutoka Shirika la Ujerumani la Kupambana na Ukoma na Kifua Kikuu (GLRA), Issa Garimo amesema dalili za ukoma ni kutokwa na mabaka kwenye ngozi, kuvimba kwa mishipa ya fahamu kusababisha ipate ganzi.
Amesema kwa watu ambao wameshapata madhara ya ukoma ikiwamo kukatika vidole vya miguuni na mikononi, hawana tena maambukizi na kwamba kinachoonekana ni madhara na siyo kwamba bado wana maambukizi ya ugonjwa huo.
Ameshauri watu wote wenye mabaka yasiyo ya kawaida kwenye ngozi za miili yao kwenda hospitali mapema kwa ajili ya kuchunguzwa afya na wataalamu ili waanze tiba mapema.