Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Waandishi wa habari wanolewa umuhimu wa hifadhi ya jamii

Muktasari:

  • Inakadiriwa zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawajajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, jambo linalowaweka kwenye hatari ya kukosa usalama wa kifedha wanapougua, kupata ulemavu au kushindwa kuendelea na kazi.

Dar es Salaam. Changamoto ya ukosefu wa hifadhi ya jamii kwa waandishi wa habari, hususan wanaofanya kazi katika sekta binafsi na wanaojiajiri, imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowaweka katika mazingira magumu wanapokumbwa na maradhi, ulemavu au wanapofikia umri wa kustaafu.

Hali hiyo imeibuliwa katika mafunzo ya siku moja kuhusu mpango wa Hifadhi Scheme wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), yaliyoandaliwa kwa ushirikiano na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), yakilenga kuongeza uelewa wa waandishi kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika Julai 24, 2026 jijini Dar es Salaam, Mweka Hazina wa Taifa wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Dk James Kalanje amesema waandishi wa habari hutekeleza majukumu yao katika mazingira yenye hatari mchana na usiku, lakini wengi wao bado hawapo katika mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii.

Amesema inakadiriwa zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawajajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, jambo linalowaweka kwenye hatari ya kukosa usalama wa kifedha wanapougua, kupata ulemavu au kushindwa kuendelea na kazi.

Suluhisho la changamoto hiyo limeelezwa kuwa ni kujiunga na mpango wa Hifadhi Scheme unaowapa nafasi wafanyakazi wa sekta binafsi na wanaojiajiri kuweka akiba kulingana na uwezo wao huku wakinufaika na mafao ya hifadhi ya jamii pamoja na huduma za bima ya afya.

“Waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii kupitia kalamu zao, vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii,” amesema.

Mwenyekiti wa Jowuta, Mussa Juma amesema ushirikiano kati ya NSSF na chama hicho utasaidia kuwafikia waandishi wengi, hasa wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi, ili kuongeza ushiriki wao katika mifumo ya hifadhi ya jamii.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jowuta, Suleimani Msuya amesema chama hicho kina wanachama 500 katika mikoa mbalimbali nchini, huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 80 bado hawajajiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii.

“Ushirikiano kati ya NSSF na Jowuta unatarajiwa kupanua mafunzo hayo hadi mikoani ili kuongeza idadi ya waandishi watakaojiunga na mpango wa Hifadhi Scheme na kujenga usalama wa maisha yao baada ya kipindi cha kazi,” amesema.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata imewapa mtazamo mpya kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii na kuwahamasisha kuanza kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Mwandishi wa habari, Harold Shemsanga amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa waandishi wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa kujituma bila kuwa na uhakika wa maisha yao wanapostaafu au wanapopatwa na majanga.

“Waandishi wengi tumekuwa tukifikiria zaidi kazi za kila siku kuliko maisha ya baadaye. Kupitia mafunzo haya nimeona umuhimu wa kujiunga na Hifadhi Scheme ili kujijengea usalama wa kifedha mimi na familia yangu,” amesema.

Kwa upande wake, mwandishi wa habari, Hilda Samson amesema ushirikiano wa NSSF na Jowuta unapaswa kuendelezwa ili elimu hiyo iwafikie waandishi wengi zaidi nchini.

“Waandishi wa habari ni sehemu muhimu ya jamii, hivyo nasi tunahitaji kuwa na hifadhi ya jamii kama ilivyo kwa kada nyingine. Tunawashukuru NSSF na Jowuta kwa kutupa elimu hii ambayo naamini itabadilisha maisha ya waandishi wengi,” amesema.