Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waililia Serikali kiongozi wa CCM kupigwa risasi

Bukoba. Wakazi wa Kata ya Ruroto Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameiomba Serikali kutatua mgogoro wa muda mrefu kati ya wafugaji, wakulima na wawekezaji wa ranchi za mifugo inayosababisha madhara kadhaa vikiwamo vifo vya watu.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa kata hiyo walisema migogoro kati ya makundi hayo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 15 sasa tayari imesababisha uharibifu wa mali, majeraha na watu kupoteza maisha.

“Kata yetu ya Rutoro kuna wakulima, wafugani na wawekezaji wenye vitalu vya kufugia, kwa miaka 15 sasa tumeshuhudia mivutano kati ya makundi haya yanayosababisha siyo tu uharibifu wa mali bali vifo vya watu. Serikali ichukue hatua kabla mambo hayajaharibika zaidi,” alisema Gerald Mutembei, mkazi wa Kijiji cha Byengeregere wilayani Muleba.

Hata Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Byengeregere, Ayoub Rusheruka alisema utatuzi wa migogoro hiyo inashindikana kutokana na wanaodaiwa kuhusika kwenye uvamizi na uharibifu wa mali za wengine kati ya wananchi na wawekezaji kumalizwa kupitia usuluhishi usiogusa kiini.

“Kipindi cha nyuma migogoro hii ilikuwa inamalizwa kwa njia ya usuluhishi lakini kadri siku zinavyosonga mbele tunaanza kushuhudia vurugu zinazosababisha vifo kama ilivyotokea Machi 3, kwa kuuawa kwa kupigwa risasi aliyekuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Rutoro, Respikius Aspro na mtu anayedaiwa kuwa ni mmoja wa walinzi wa kitalu cha mwekezaji,” alisema Rusheruka.

Akizungumzia tukio hilo katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) aliiomba Serikali kukomesha migogoro hiyo kwa kuwawajibisha wanaohusika na vitendo hivyo vya kihalifu.

“Serikali ichukue jukumu la kulinda maisha ya wananchi kwenye eneo hili,” alisema Mwijage.


Mauaji yalivyotokea

Akizungumzia kifo cha kiongozi huyo wa CCM ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Mabare kilichoko Kijiji cha Byengeregere, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Byengeregere, Ayoub Rusheruka alisema Aspro alipigwa risasi iliyoingilia mgongoni na kutokea tumboni.

“Respikius Aspro alifika hapa kijijini Machi 3 baada ya kupata taarifa za mashamba ya wananchi kuvamiwa na mifugo ya wawekezaji, akiwa njiani kwenda kuwasikiliza wananchi, ghafla alipigwa risasi ya mgongo iliyotokea tumboni na mmoja wa walinzi wa kampuni binafsi katika kitalu namba saba ambaye hakufahamika jina,” alisema ofisa huyo.

Baada ya tukio hilo, alisema katibu huyo alikimbizwa Hospitali ya Rubya lakini alifariki dunia wakati anatibiwa.

“Tunaisihi Serikali kuingilia kati mgogoro huu kwa kutenga na kuweka mipaka kati ya ardhi ya wananchi na wawekezaji,” alisema Rusheruka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Wiliam Mwampaghale alisema uchunguzi wa mauaji hayo tayari umeanza na watahakikisha wote waliohusika wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria huku akiwasihi wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiana utakaowezesha kupatikana kwa watuhumiwa wote.

“Jalada la uchunguzi kuhusu mauaji ya aliyekuwa katibu wa CCM Kata ya Rutoro, Respikius Aspro kilichotokea mwanzoni mwa mwezi huu tayari limefunguliwa. Nawasihi wananchi wenye taarifa wajitokeze kusaidia uchunguzi ukamilike mapema na wahusika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Kamanda Mwampaghale.