Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Wajasiriamali washirikishwe matumizi sahihi ya vyoo bora’

Sinki linalotengenezwa na Kampuni ya Sato ambalo ni nafuu na salama. Picha na mtandao

Muktasari:

“Magonjwa yatokanayo na uchafu yanahitaji ushiriki wa jamii nzima. Kila mtu akielewa hili, tutakuwa na jamii salama itakayoelekeza nguvu kwenye uzalishaji mali,” anasema Ashura Mahwewe, akiizungumzia Siku wa Vyoo Duniani.

“Magonjwa yatokanayo na uchafu yanahitaji ushiriki wa jamii nzima. Kila mtu akielewa hili, tutakuwa na jamii salama itakayoelekeza nguvu kwenye uzalishaji mali,” anasema Ashura Mahwewe, akiizungumzia Siku wa Vyoo Duniani.

Kila Novemba 19, Umoja wa Mataifa huadhimisha siku hiyo ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hatari za kutotumia choo bora kwa afya ya binadamu hata usalama wa mazingira.

Zaidi ya watu bilioni 3.6 duniani kote ambao ni karibu nusu ya watu bilioni nane waliopo ulimwenguni, wanatumia vyoo visivyo salama ndio maana tangu mwaka 2013 siku hii ilitambulika rasmi ili kuikumbusha jamii umuhimu wa kutumia vyoo salama kwa afya na mazingira.

“Serikali ina programu nyingi za kuhamasisha matumizi bora ya choo, lakini ni wangapi wanashirikishwa kwenye mpango huo? Vijana wapewe nafasi ya kutoa elimu kuanzia kwa wanafunzi wa shule za msingi mpaka watu wazima, wasiona kipato cha uhakika wawezeshwe,” alishauri Ashura.

Uchafuzi wa mazingira hutokea pale uchafu kutoka kwenye vyoo visivyo salama unapotiririka na kuingia kwenye mito, maziwa hata ardhini hivyo kuchafua maji na rasilimali nyingine zinazoonekana na zisizoonekana.

Meneja mkazi wa kampuni ya Sato Tanzania inayojishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa vyoo mbadala, Justin Mbowe alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na Serikali pamoja na wabia wake kuboresha vyoo nchini ili kupunguza kuenea kwa magonjwa yatokanayo na uchafu.

Kwenye kampeni ya nyumba ni choo kwa mfano, alisema Sato kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) na Wizara ya Afya wanasimamia usafi wa mazingira kwa kupita kila nyumba katika mikoa ya Iringa, Songwe, Mbeya, Njombe, Kigoma na Zanzibar kuhakikisha kila moja ina choo bora.

“Mjadala wa matumizi ya choo bora unapaswa kuanzia kwa watoto. Mwaka 2018 Sato tulisaidia kuboresha vyoo 80,000 ili kuepuka magonjwa yanayosababishwa na uchafu ambayo yanaigharimu Serikali wastani wa Sh1.6 bilioni kila mwaka.

“Vyoo vyote hivi vilipelekwa shuleni na kwenye zahanati na kila mkoa ulipata mgawo kulingana na mahitaji yake,” alisema Mbowe.

Vyoo vinavyotolewa na kampuni ya Sato ambayo mpaka mwaka 2025 inakusudia kuwafikia watu milioni 100, alisema ni vile vinavyoondoa harufu ambayo huwakimbiza watu na kuwafanya waende kujisaidia kichakani.

Kuhusu namna vijana na jamii inavyoweza kushiriki kuhamasisha matumizi ya vyoo salama, alisema ni muhimu kufahamu kwamba Serikali inatoa hamasa lakini haina bidhaa, hivyo kutoa fursa kwa wajasiriamali na wahamasishaji kushiriki.

“Wajasiriamali wa ndani wanayo nafasi muhimu ya kuwaelimisha na kuwawezesha wananchi kufanikisha kampeni hii. Katika mikoa ambako tumepeleka bidhaa zetu, kuna wafanyabiashara wanaouza vyoo vyetu hata vicoba navyo vinapata fursa hiyo.

“Sisi tunalenga kuwawezesha watu wenye kipato cha chini ambao wengi hawawezi kumudu vyoo vya marumaru vinavyouzwa madukani. Uzuri wa vyoo vyetu ni kwamba havitumii maji mengi kama hivi, hivyo kuwa rafiki hata kwa watu wasiounganishwa na mfumo rasmi wa maji,” alisisitiza Mbowe.

Akilizungumzia hilo, Laurent Maganga, mfanyabiashara jijini Mbeya alisema ushiriki wa wajasiriamali unahitajika kwa kiasi kikubwa, kwani maeneo mengi yenye makazi holela hayana miundombinu ya majitaka na watu wanajenga vyoo wanavyovimudu.

“Watu wanatumia vyoo vya matairi au pipa kutokana na kukosa fedha za kununua vyoo dukani.

“Wanatiririsha uchafu kila mvua inaponyesha kwa sababu ya kuwa na uchumi mdogo. Wajasiriamali wakishirikishwa kuleta ubunifu na Serikali ikawahakikishia soko tutakuwa salama zaidi,” alisema Maganga.

Naye Rehema John, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam alisema matumizi ya vyoo visivyo salama huhatarisha maisha ya wengi kutokana na uchafu wake kusambaa mtaani. “Mvua ikinyesha tu, kila mtu jijini hapa anaanza kuwa makini kuanzia kwenye kununua mboga mpaka maji ya kunywa. Kuna baadhi ya mitaa hata maji yao ya kisima unatakiwa usinywe kwa sababu maji huingiliana na ya vyoo kwa namna vilivyojengwa. Pia zipo mboga zinazomwagiliwa kwa maji yanayotiririka kutoka chooni,” alisema Rehema.


Umoja wa Mataifa

Vyoo vilivyojengwa vizuri, huzuia uchafuzi wa maji yaliyopo ardhini, hivyo Umoja wa Mataifa (UN) unahimiza kila mmoja kutumia choo kilichounganishwa na mfumo wa majitaka kuondoa uwezekano wa kuchafua rasilimali za ardhini.

Uhusiano wa uchafu wa chooni na maji yaliyopo ardhini ni jambo nyeti linalopaswa kutiliwa mkazo na kila mtu.

“Katika siku hii ya vyoo duniani, tuvifanye visivyoonekana vionekane,” inasomeka kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya mwaka huu.

Dunia imepanga kuhakikisha kila mtu anatumia choo safi ifikapo mwaka 2030. Kwa kufanya hivyo, itakuwa imetekeleza kifungu cha pili cha sehemu ya sita ya Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG). Lengo hili linapaswa kutekelezwa ndani ya miaka minane iliyobaki kabla ya mwaka 2030 ambao ndio ukomo wake.

Umoja wa Mataifa umetenga siku mbili, Desemba 7 na 8 kujadili namna ya kuyalinda maji yaliyo ardhini dhidi ya uchafuzi unaotokana na matumizi ya vyoo visivyo salama. Mjadala huo utafanyika jijini Paris, Ufaransa.

Mjadala huo unalenga kuibua uelewa wa maji ya ardhini kimataifa na utajadili ujumbe utakaojadiliwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwakani, kuwasisitiza watunga sera kutambua umuhimu wa kuyalinda maji yaliyopo ardhini.