Wakazi, wanafunzi wakwama kivuko kikisimama kufanya kazi Lindi

Kivuko cha MV Kitunda kikiwa kimeegeshwa.

Muktasari:

Jana, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania  (Temesa) umetangaza kusitisha huduma za vivuko katika mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Pwani kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kimbunga Hidaya

Lindi.  Kivuko cha MV Kitunda kinachofanya safari zake kutoka Ng’ambo ya Lindi Mjini kwenda Kitunda kimesitisha safari kwa hofu ya Kimbunga Hidaya.

Jana, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania  (Temesa) umetangaza kusitisha huduma za vivuko katika mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Pwani kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kimbunga Hidaya.

"Kusema ukweli hapa tumekwama mahitaji yetu yapo huku na wengine yapo kule ng’ambo, tunaomba watufanyie maarifa tupate usafiri wakurudi Kitunda tukibakia huku hali itazidi kuwa mbaya na watoto wetu hali zao zitakuwa mbaya tunaomba watusaidie tupate usafiri,” amesema Rashidi Mponji mkazi wa Kitunda, leo Jumamosi Mei 4, 2024.

Baadhi ya wananchi wa Lindi waliokwama kuvuka baada ya Kivuko cha MV Kitunda kusitishwa kutoa huduma.

Mkazi wa Kitumbikwela Iddi Bakari amesema yupo kivukoni tangu saa mbili asubuhi, hajui atarudi vipi nyumbani kwake.

“Nilipoona hali nzuri kidogo alfajiri nilivuka kuja kutafuta mahitaji huku mjini, nimemaliza narudi hapa naambiwa kivuko hakivushi kimesimama, hatujui kimesimama hadi saa ngapi amesema Bakari anayefanya biashara ya kuuza supu eneo la Kitunda.

“Shabani Juma, mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Msinjahili katika Manispaa ya Lindi amesema leo walikuwa wana mitihani ya majaribio shuleni, hivyo aliwahi kwenda shule na alipofika mwalimu aliwarudisha kwamba mitihani hiyo imeahirishwa.

“Tukarudi hapa kivukoni kuja kupanda kivuko turudi nyumbani, tukaambiwa safari zimesitishwa kutokana na hali ya hewa kutoruhusu kivuko kufanya kazi.

Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Lindi, Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabeja amesema wamesimamisha safari zote za majini hadi hali itakapokuwa sawa na wavuvi wote hawatakiwi kuingia tena bahari kwenda kuvua mpaka watakapotarifiwa.

"Watu wasipuuze uwepo wa mvua kubwa pamoja na upepo unaosababishwa na Kimbunga Hidaya. Hiki Kimbunga kipo sio kama wanavyosema ni taarifa ya kizushi tumezuia kuvusha, labda niwaambie tu, mali inanunuliwa uhai haununuliwi,” amesema kamanda huyo.