Wamiliki 11 wafutiwa leseni umiliki maeneo ya madini
Muktasari:
- Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema uamuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2019 na marekebisho ya mwaka 2017 pamoja na kanuni ya 21 ya Kanuni za Madini (Haki Madini) za mwaka huu.
Dodoma. Serikali imefuta leseni 11 za umiliki wa maeneo ya madini nchini na kuyarejesha serikalini bila hakikisho la kuwarejeshea tena waliokuwa wakiyamiliki.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema uamuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2019 na marekebisho ya mwaka 2017 pamoja na kanuni ya 21 ya Kanuni za Madini (Haki Madini) za mwaka huu.
Aliwataja wamiliki wa maeneo yaliyofutiwa umiliki na maeneo wanakoyamiliki kuwa ni pamoja na kampuni za Kabanga Nickel (Ngara-Kagera), National Mineral Development Corporation (Kahama-Shinyanga) na Bafex Tanzania inayomiliki leseni za maeneo matatu ya Chunya mkoani Mbeya.
Zingine ni Mabangu Mining (Mbogwe-Geita), Resolute (Tanzania) Limited (Mbongwe-Geita), Wigu Hill Mining (Morogoro), Nachingwea Nickel (Nachingwea-Lindi) na Precious Metals Refinery (Bariadi na Busega-Simiyu).
Kwa mujibu wa Profesa Kikula, wamiliki wa maeneo hayo walikuwa na leseni zinazomaliza muda wake kati ya Agosti 31, 2019 na Aprili 20, 2020.
Profesa Kikula alisema hadi kufikia Julai 4, 2017 kulikuwa na maombi mapya ya leseni za uchimbaji wa kati zipatazo 15 na za kuhuisha 21.
“Pia maombi ya leseni za uchimbaji wa madini yalikuwa 4,345 katika ofisi za mikoa na wilaya kote nchini. Kadhalika, hadi kufikia Julai 4 mwaka jana kulikuwa na jumla ya maombi 240 ya leseni za utafutaji wa madini,” alisema.
Profesa Kikula alisema kati ya maombi hayo, 86 yalishalipiwa ada ya kuandalia leseni na yaliyobaki hayajalipiwa. “Kwa taarifa hii waombaji wote wa leseni za madini wanatakiwa kukamilisha maombi yao ili yaendane na matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kama yalivyorekebishwa mwaka 2017,” alisema.
Alisisitiza kuwa pamoja na hilo, wamiliki hao wanatakiwa kulipia ada za kuandalia leseni za madini kwa maombi yaliyokidhi vigezo vya kupewa leseni na kuwasilisha mpango wa jinsi gani watakavyowashirikisha wananchi wanaozunguka migodi husika (local content plan).
Mengine wanayotakiwa kuwasilisha ni mpango wa uwajibikaji kwa jamii na kiapo cha uaminifu kwa kadri ya kifungu cha 105 na 106 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 vinavyotamka.
Pia, waombaji wote wa leseni za utafutaji wa madini wanapaswa kuwasilisha taarifa za rasilimali za kiufundi (vifaa vya kitaalaamu vya madini, watalaamu) na taarifa za hesabu za fedha zilizokaguliwa.
Profesa Kikula alisema waombaji wote wa leseni za uchimbaji wa kati na kubwa wanatakiwa kuwasilisha vyeti vya tathmini ya athari ya mazingira, uthibitisho wa tathmini ya fidia na kutokuwepo kwa mgogoro ama migogoro katika eneo linaloombewa leseni ya uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake, katibu mtendaji wa tume hiyo, Profesa Shukrani Manya alisema wamiliki waliowasilisha maombi yao watalazimika kuangalia kama wametimiza masharti ya sheria hiyo na kanuni zake na kutuma ofisini kwake.
“Kuja kwenu ni kuwaambia Watanzania kwamba lile zoezi lililositishwa tangu mwaka jana sasa limefunguliwa. Walioomba leseni hasa zile za biashara na zile za uchimbaji mdogo watazipata katika ofisi zetu walikowasilisha maombi,” alisema.
Profesa Manya alisema leseni mpya zitaanza kutolewa Jumanne ijayo na kuwataka waombaji kwenda katika ofisi za madini za wilaya na kanda ambako watapatiwa huduma hiyo.