Wananchi wataka utatuzi kero ya maji Handeni

Mbunge wa jimbo la Handeni Mjini,(CCM) Reuben Kwagilwa (Mwenye fimbo) akiwa na viongozi wengine wakikagua bomba ambazo zitatumiwa katika mradi wa maji wa Miji 28, ambapo Handeni imo. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Mradi mkubwa wa maji wa miji 28 unatajwa kuwa suluhisho la kero ya maji safi na salama inayokabili maeneo mengi katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Handeni. Wananchi wa Kata ya Kwediyamba Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga, wamemuomba Mbunge wa jimbo hilo, (CCM) Reuben Kwagilwa kuwasaidia kukamilisha mradi wa maji uliopo kwenye eneo hilo kukamilika, ili kuondokana na shida ya maji inayowakabili.

Wakizungumza wakati wa ziara ya mbunge huyo ya  kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye jimbo hilo jana Aprili 5, 2024, wananchi hao wamesema kwa sasa hawana huduma ya uhakika ya maji, hivyo endapo mradi uliopo kwenye kata yao ukikamilika utaondoa shida hiyo.

Mkazi wa kata ya Kwediyamba, Fatuma Mwilo amesema eneo hilo lina shida kubwa ya maji, ambapo wananchi wanalazimika kukesha  kwenye visima kutafuta maji, hivyo mradi huo ukikamilika utakuwa ni mkombozi kwao na wataepukana na tatizo hilo.

Amesema kuwa kwa sasa wanatumia maji ya visima vya asili na mvua lakini vyanzo hivyo maji yake sio salama.

Akizungumza  na wananchi hao Kwagilwa amesema  Serikali imetoa zaidi ya Sh1.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata hiyo, ili kutatua tatizo la kukosekana huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.

Amesema ndani ya siku 30 mpaka 60 kuanzia sasa mradi utakuwa umekamilika na wananchi wataanza kupata  huduma ya maji, hivyo atakwenda kuhimiza wizara ya maji kutoa kiasi cha fedha kilichobaki ili mkandarasi amalizie mradi huo.

Fundi sanifu kutoka Mamlaka ya Maji  ya Handeni Trunk Main (HTM), Ali Shemahonge amesema mradi huo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 63 na inahitajika Sh478 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na umaliziaji.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni, Amiri Changogo amewataka wataalamu wanaosimamia mradi huo, kuhakikisha unajengwa kwenye viwango vinavyolingana na thamani ya fedha iliyotolewa..