Wanaodaiwa kusafirisha kilo 332 za dawa za kulevya, wakosa dhamana

Washtakiwa tisa wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha kilo 332 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine, kinyume cha sheria.Picha na Hadija Jumanne 

Muktasari:

 Washtakiwa hao muda wote walikuwa wamefunika nyuso zao kwa kutumia mashati na fulana walizokuwa wamevaa

Dar es Salaam. Mvuvi wa samaki,  Ally Ally(28) na wenzake wanane, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya  heroin na methamphetamine, zenye uzito wa kilo 332.

Washtakiwa hao ambao muda wote walikuwa wamefunika nyuso zao kwa kutumia mashati na fulana walizokuwa wamevaa, wamefikishwa mahakamani hapo leo, Jumatatu Aprili 22, 2024 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Batilda Mushi.

Mbali na Ally, washtakiwa wengine ni Bilal Hafidhi (31)ambaye ni mfanyabiashara; Mohamed Khamis (47) mvuvi wa samaki na Idrisa Mbona (33) muuza magari.

Wengine ni Rashid Rashid(24) Beach Boy na mkazi wa Ubungo Maji; Shabega Shabega(24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.

Vilevile, yupo Dunia Mkambilah(52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke;  Mfanyabiashara Mussa Husein (35)mkazi wa Mwambani na Hamis Omary(25) ambaye kazi yake ni shughuli za ufukweni (Beach boy) na hana makazi.

Wakili Mushi amedai mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 10561 ya mwaka 2024.

Hata hivyo, kabla kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Kabate amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo, kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikilizwa kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Hakimu Kabate baada ya kumaliza kutoa mwongozo huo, upande wa mashtaka waliwasomewa mashtaka yao.

Mushi alidai shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote ambalo ni kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.

Katika shtaka hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hotel ya White Sands, iliyopo Kinondoni, walisafirisha kilo 100.83 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine, kinyume cha sheria.

Shtaka la pili siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 232.69 za heroin, wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Upande wa mashtaka umeieleza  Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Kabate ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 6, 2024 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana kesi inayowakabili, haina dhamana kwa mujibu wa sheria.