Watatu kortini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya

Muktasari:

  • Wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 27, 2020 eneo la Kiwalani Migombani, Wilaya ya Ilala, ambapo wanadaiwa kukutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa gramu 145.76, kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Charles Mgonella (29) na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine na bangi.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapa leo, Aprili 19, 2024 na kusomewa mashitaka  na Wakili wa Serikali, Glory Kilawa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.

Mbali na Mgonella, washtakiwa wengine ni Inocent Wanna (21) na Collin Mgonella (19).

Akiwasomea mashitaka hayo, Glory amedai katika shitaka la kwanza ambalo ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi linawakabili washtakiwa wote.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 27, 2020 eneo la Kiwalani Migombani, Wilaya ya Ilala, ambapo wanadaiwa kukutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa gramu 145.76, kinyume cha sheria.

Shitaka la pili na tatu linamkabili mshtakiwa Charles peke yake, inadaiwa siku hiyohiyo eneo la Ununio Wilaya ya Kinondoni, alisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 65.09.

Shitaka la tatu inadaiwa siku hiyohiyo eneo hilohilo  alikutwa akisafirisha dawa tiba zenye kulevya zinazojulikana kama delta 9 tetrahydrocannahinol zenye uzito wa gramu 20.24. Washtakiwa baada ya kuwasomea mashitaka hayo, walikana na upande wa mashitaka, ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo uliomba tarehe nyingine ya kuwasomea mshitakiwa hoja za awali (PH).

Hakimu Mbuya, alisema uzito wa dawa za kulevya aina ya heroine ambazo wanadaiwa kukutwa nazo hazina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo walirudishwa rumande hadi Mei 2, 2024 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.