‘Wanawake wengine wanachukulia rushwa ya ngono kama bahati’

Muktasari:

  • Jamii imetakiwa kuungana kwa pamoja kukemea vitendo vya rushwa ya ngono kwani vimekuwa vikidumaza haki na kuwanyima fursa wanawake.

Dar es Salaam. Jamii imetakiwa kuungana kwa pamoja kukemea vitendo vya rushwa ya ngono kwani vimekuwa vikidumaza haki na kuwanyima fursa wanawake.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Maendeleo (Wajiki), Janeth Mawinza katika hafla maalum iliyoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) ijulikanayo kama The Citizen Rising Woman katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani leo Jumatano Machi 8, 2023.

Mawinza alitolea mfano wa kuwa aliwahi kuondolewa kazini pamoja na mumewe kwa sababu ya kukataa kutoa rushwa ya ngono.
"Wapo wanawake wengi waliopitia changamoto kama niliyopitia mimi na kutokana na rushwa ya ngono, wamepoteza kazi au kukosa fursa mbalimbali,"alisema.

Pia alisema katika jamii kuna wanawake bado hawana elimu ya kutosha kuhusu rushwa ya ngono hali inayowafanya wengine kuona ni jambo la kujitakia na baadhi yao kuchukulia kama bahati.

"Hivyo kuna haja ya elimu hii kuendelewa kutolewa katika jamii ili kufahamu namna gani rushwa ya ngono inachangia katika kudumaza haki za wanawake," alisema.

Aliongeza kuwa katika utoaji wa elimu kwa jamii kuna haja ya wanaume nao kupewa elimu hiyo kwa kina ili kujua namna rushwa ya ngono inavyoteketeza.