Wanne mbaroni kwa kutumia majina ya viongozi kutapeli

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akiwaonesha waandishi wa habari vifaa vya Starlink vilivyo kamatwa baada ya kuingizwa nchini kinyume na sheria.

Muktasari:

Ikiwa siku nane zimepita tangu Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iwatie mbaroni watuhumiwa watano kwa makosa ya kutumia majina ya viongozi wa umma kwenye mitandao ya kijamii kuwatapeli watu fedha, wengine wanne wamekamatwa kwa makosa hayo.

Dar es Salaam. Ikiwa siku nane zimepita tangu Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iwatie mbaroni watuhumiwa watano kwa makosa ya kutumia majina ya viongozi wa umma kwenye mitandao ya kijamii kuwatapeli watu fedha, wengine wanne wamekamatwa kwa makosa hayo.

Idadi ya watuhumiwa hivi sasa inafikia tisa. Machi 14, 2024 Polisi ilitangaza kuwashikilia watuhumiwa watano.

Imeelezwa mbinu wanayotumia kutapeli ni kuanzisha majukwaa kwenye mitandao ya kijamii kuomba michango ya harusi, misiba na wengine kudai wanatoa mikopo.

Akizungumza Dar es Salaam leo Machi 22, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamewatia mbaroni watuhumiwa wapya ikiwa ni mwendelezo wa msako wanaoufanya wakishirikiana na kikosi cha makosa mitandaoni.

“Tumemkatama Wilfred Werandumi (44), mkazi wa Tungi, Morogoro na Abdulrahim Mwakibinga (30), mkazi wa Mwandege, Morogoro kwa tuhuma za kutumia majina ya viongozi wa nchi kutapeli watu, kwa kujifanya wanaomba michango ya harusi, misiba na matibabu,” amesema.

Kamanda Muliro amewataja mawaziri ambao majina yao yanatumika katika utapeli kuwa Dk Stergomena Tax (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Innocent Bashungwa (Ujenzi), Mohamed Nchengerwa (Ofisi ya Rais-Tamisemi), Mhandisi Hamad Masauni (Mambo ya Ndani), na Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo.

Amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Salum Kingu (25) na Loveness Silonga (24), wote wakazi wa Mbalizi, mkoani Mbeya wanaotuhumiwa kutumia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook yenye jina la Kopa Faster Tulia Trust Foundation kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali kwa kudai kuwa wanatoa mikopo kwa masharti nafuu na haraka.

"Watuhumiwa hawa wamekuwa wakitumia namba ya simu 0749 704 445. Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji mkali wa tabia hizi na watuhumiwa wote watashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria," amesema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amesema Jeshi hilo limewatia mbaroni watu wawili kwa tuhuma za kuingiza vifaa vya mawasiliano ya intaneti nchini vya 'Starlink Kit/Divice' bila kufuata utaratibu.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Claudia Makaranga (28), mkazi wa Kawe wilayani Kinondoni na Hongliang Yang (35), raia wa China, mkazi wa Kigamboni.

Ametaja vifaa walivyokamatwa navyo kuwa ni Starlink dish 12 na Starlink Router 12, ambavyo amesema thamani yake bado haijatajwa.

"Baadhi ya vifaa vilivyoingizwa nchini imebainika vilishauzwa na kutumika katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, kitendo ambacho ni kosa na kinyume cha sheria kwani havijaidhinishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)," amesema.

Kamanda Muliro amesema wananchi wanapaswa kuwa makini na mitandao ya kijamii na wale wanaotumia vibaya waache mara moja kwani jeshi hilo bado linaendelea kufanya doria.