Polisi wabaini utapeli wa kutumia picha za viongozi kwa matangazo

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limetangaza msako mkali kwa watu wanaotumia nembo na picha za viongozi kutapeli watu.

Dodoma. Jeshi la Polisi limetangaza msako mkali kwa watu wanaotumia nembo na picha za viongozi kutapeli watu.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime leo Januari 14, imeeleza kuwa kuna wimbi kubwa la utapeli ambalo limeibuka kwa siku za hivi karibuni.

Kamanda Misime ametaja njia wanazotumia matapeli hao ni kuweka picha za viongozi kisha kutangaza kuwa wanamaonyesho ambayo kiongozi huyo atakuwa mgeni rasmi kisha wanaanza kuomba kiingilio kwa wanaotaka kushiriki.


Amesema tayari Polisi imeanza kuwafuatilia baadhi ya watu ambao watakamatwa na kuwa mfano kwa watu wengine wenye nia ovu kama hiyo.

"Polisi haitawavumilia watu wa aina hiyo, tumewabaini na wengine tunawafiatilia, niwaambie kuwa hakuna atakayesalia kwenye shughuli hiyo kwani tumekipanga kila kona," amesema Misime katika taarifa yake.

Msemaji huo amewaomba wananchi kutoa taarifa haraka kwa Polisi pindi wanapokutana na watu wa aina hiyo ili wakamatwe haraka kabla ya kutapeli huku akiwatahadharisha wananchi kuwa makini na watu wa aina hiyo.

Katika hatua nyingine Polisi imeonya madereva wanaokwenda mwendo kasi na kusababisha ajali za vifo na majeruhi kwamba hawazitendei haki taaluma zao.

Amesema nchi ina amani na ulinzi umeimarishwa lakini madereva hawatendi haki nankuwaagiza abiria kuwa makini kwa vyombo vya moto ili pindi wakibaini kuna ukiukwaji wa sheria za barabarani watoe taarifa.