‘Wasionyonyesha watoto hatarini kuugua saratani ya matiti”

Muuguzi Bingwa wa Magonjwa ya Saratani Bugando, Agatha Manyanda (Mwenye tisheti nyekundu mbele) akitoa elimu ya magonjwa ya saratani na afya ya uzazi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Bujingwa wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Baadhi ya wazazi wanatajwa kusitisha kuwanyonyesha watoto wachanga kwa kisingizio cha kutingwa na kazi, kuhofia matiti yao kulala na utandawazi.

Mwanza. Imeelezwa kuwa wanawake waliojifungua na kutowanyonyesha watoto kwa kipindi cha angalau cha miaka miwili mfululizo, wako hatarini kuugua satarani ya matiti.

Muuguzi Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza, Agatha Manyanda ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 4, 2024, wakati wa mafunzo ya kujenga uwezo kuhusu afya ya uzazi kwa wanafunzi wa Sekondari ya Bujingwa wilayani Ilemela.

Muuguzi huyo amesema baadhi ya wanawake wanadaiwa kusitisha kuwanyonyesha vichanga wao kwa hofu ya matiti yao kulala  aukutokuwa saa sita’, majukumu ya kazi na msukumo kutokana na utandawazi.

Mbali na tishio la kuugua saratani, Agatha amesema uamuzi huo una athari kiafya na kisaikolojia kwa mtoto aliyeachishwa.

“Ukijifungua nyonyesha mtoto wako mpaka atimize angalau miaka miwili kama inavyoelekezwa na watalaamu, usiponyonyesha kwa miaka hiyo unajiweka hatarini kupata saratani ya matiti.

“Kwa sababu unapopata ujauzito, mwili wako una sense (unahisi) na kupeleka taarifa kwenye ubongo kwamba sasa anza kuandaa chakula cha mtoto (maziwa). Ukijifungua tu hakuna anayeyaambia maziwa kwamba toka, tena wengine yaanza kutoka hata wakati wa ujauzito,” amesema Agatha.

“Ukishayazuia unaanza kusababisha vitu vingine kwa sababu mwili wako kwa wakati huo unajua tayari kuna mtu anahitaji kile chakula, kwa hiyo chakula kile unakizuia kinaleta mabadiliko, matokeo yake kinakusababishia saratani,” amesema.

Amewaonya wanaosema watoto wao hawataki kunyonya na kutaja baadhi ya sababu zinazopelekea mtoto akatae kunyonya, ikiwemo mama kutojua namna ya kumshikisha titi mtoto wake na changamoto nyingine za kiafya anazoweza kuwa nazo mtoto, hivyo akawataka wanaopitia changamoto hiyo kuwapeleka watoto wao katika kituo cha afya kwa uchunguzi.

“Ndiyo maana Serikali ilikuja na mpango mahsusi ili kuruhusu watumishi waliojifungua na wameanza kazi baada ya likizo ya uzazi kupata muda wa kunyonyesha vichanga wao, pia maeneo ya umma yana sehemu maalumu za kunyonyeshea watoto, lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayesitishwa kunyonya kabla ya muda wake,” amesema.

Mtaalam huyo ametaja visababishi vingine vya saratani ya matiti kuwa ni pamoja na matumizi holela ya dawa za kuzuia mimba, matumizi ya kemikali, sababu za kimazingira na sababu za kibaiolojia.

Amesema unyonyeshaji wa watoto unahimizwa kwa sababu maziwa ya mama ni mlo bora, kamili na muhimu kwa mtoto wa binadamu kuliko chakula kingine katika siku za mwanzo za maisha yake.