110 wakutwa na dalili za saratani Mwanza, tezi dume tishio

Muktasari:

  •  Miongoni mwa watu 110 waliokutwa na dalili saratani, watu 49 sawa na asilimia 45 walikutwa na dalili za awali za saratani ya tezi dume.

Mwanza. Watu 110 sawa na asilimia 22 ya watu 500 waliofanyiwa uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kwa siku nne mkoani Mwanza na Simiyu, wamebainika kuwa na dalili za awali za magonjwa ya saratani.

Uchunguzi huo ulifanywa kwa siku nne na madaktari bingwa wa magonjwa ya saratani kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Mionzi ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) katika wilaya tatu ikiwemo Busega mkoani Simiyu, Sengerema na Nyamagana mkoani Mwanza.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 29,2024, wakati wa upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza uliohitimishwa hospitalini hapo, Mkuu wa Idara ya Mionzi Bugando, Dk Margreth Magambo amesema kati ya watu 110 wenye dalili hizo, watu 49 sawa na asilimia 45 walikutwa na dalili za awali za saratani ya tezi dume.

Pia amesema watu  20 kati ya 110 sawa na asilimia 18 wamekutwa na uvimbe kenye figo zao jambo linalotajwa kuwa dalili za awali za kuugua saratani ya figo, huku mtoto mmoja akigundulika kuwa na tatizo la kujaa maji kichwani.

Mtaalamu huyo amesema watu 41 kati yao walibainika kuwa dalili za magonjwa mengine ikiwemo saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, matiti, ini, saratani ya damu, mapafu, ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

“Kutokana na takwimu hizo niwaombe wanaume ambao wamefikia umri wa kuanzia miaka 15 kujitokeza kufanyiwa vipimo vya saratani ya tezi dume mara kwa mara. Pia waepuke tabia hatarishi ikiwemo ulevi, wasiwe na uzito kupindukia, wajitahidi kula mlo kamili na kufanya mazoezi ya mwili.

 “Magonjwa mengi yasiyoambukiza na yanayoambukiza yanaweza kudhibitika endapo yakibainika mapema. Jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kwenda vituo vya afya kufanyiwa uchunguzi wa afya zao, hii itasaidia kama kuna tatizo litibiwe kabla halijafika hatua mbaya,” amesema Dk Magambo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Dk Fabian Masaga amesema kila mwaka watu 10,000 wenye umri zaidi ya miaka 15 nchini, wanabainika kuugua magonjwa ya saratani huku watu 6,000 wakifariki kutokana na magonjwa hayo.

Hata hivyo, Dk Masaga amesema pamoja na Serikali kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na kuongeza vifaa na watalaamu watakaorahisisha kubaini magonjwa yasiyoambukiza, bado mwamko wa jamii kupima hairidhishi.

Dk Masaga amesema kutokana na changamoto ya mwamko mdogo wa jamii kupima afya, Bugando itaendelea kuagiza watalaamu wake kwenda maeneo ya vijijini kuhamasisha na kupima bila malipo ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo na kutoa tiba kabla haujafika hatua mbaya.

“Zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wanaogundulika na changamoto ya saratani hupoteza maisha kila mwaka, hii hutokana na sababu mbalimbali mojawapo kubwa ni wananchi kuchelewa kufika sehemu za kutolea huduma. Ndiyo maana Bugando tukaagiza wananchi wafikiwe kufanyiwa uchunguzi bure ili kurudisha fadhila kwa jamii (CSR),” amesema Dk Masaga.

Kwa upande wake, Mkazi wa Kishiri jijini Mwanza, Menge Nyamtamba ambaye amejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya saratani kwa hiari ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kufanya hivyo, kwa kile alichodai itasaidia kupunguza gharama pale unapogundulika katika hatua ya awali.

“Mtu ukipimwa ukabainika kuugua ugonjwa wowote ule itakuwezesha kuanza matibabu mapema kabla hata haujafika hatua mbaya, hii itakupunguzia gharama ambazo ungelazimika kuzilipia endapo ungebainika ukiwa hatua mbaya na ambazo haziwezi kutibika kwa urahisi,” amesema Nyamtamba.

Naye, Veronica Maingu ameishukuru Bugando kwa utoaji wa huduma hiyo bila malipo, huku akiomba iwe endelevu hasa maeneo ya vijijini ambako wakazi wake hawamudu gharama za uchunguzi na matibabu ya magonjwa hayo.