Watumishi wa umma watakiwa kumuenzi Sokoine kwa vitendo

Muktasari:
- Alitoa agizo hilo jana katika kumbukumbu ya miaka 34 ya kifo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani, iliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Engwiki wilayani Monduli mkoani Arusha na kuwaonya watumishi wa umma kutokuwa wabinafsi na wenye tamaa za mali. Alisema Serikali inajitahidi kupambana na rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi kama njia ya kumuenzi Sokoine kwa vitendo.
Arusha/mikoani. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ikiwa njia ya kumuenzi hayati Edward Sokoine.
Alitoa agizo hilo jana katika kumbukumbu ya miaka 34 ya kifo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani, iliyofanyika nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Engwiki wilayani Monduli mkoani Arusha na kuwaonya watumishi wa umma kutokuwa wabinafsi na wenye tamaa za mali. Alisema Serikali inajitahidi kupambana na rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi kama njia ya kumuenzi Sokoine kwa vitendo.
Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu aliyeongoza ibada alisema Sokoine alimcha Mungu na hakuwa mtu wa ovyo, “Huwezi kuwa mtu wa ovyo halafu umche Mungu. Tuwe waaminifu na tuache maisha ya unafiki na hiana.”
Akitoa salamu za familia, Lembris Kipuyo alisema wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuhakikisha anadhibiti rasilimali za nchi zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi akimzungumzia marehemu Sokoine alisema kuna watu wanakufa lakini bado wanaendelea kuwa hai na kwa hilo, wanafamilia wanapaswa kuendelea kumshukuru Mungu.
“Tangu alipofariki mwaka 1984, hakuna mtu aliyejua kwamba hadi sasa, miaka 34 imepita Sokoine ataendelea kuwa hai. Ninasema yu hai kwa sababu maneno na matendo yake, bado yanaishi,” alisema.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kumhusu Sokoine, Profesa wa sheria, Issa Shivji alisema alifanikiwa kuifanya Tanzania isimame vyema katika dhana ya kilimo kama uti wa mgongo wa Taifa.
“Sokoine licha ya mapungufu yake alikuwa kiongozi wa kipekee, tumemsahau sana. Michango yake mingi bado haitambuliki,” alisema.
Alisema wakati wa uongozi wake, pamoja na kupinga rushwa na uonevu, alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kilimo na ufugaji vinapewa umuhimu mkubwa, “Ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwataka wataalamu waende wakaishi vijijini yaani wawe karibu na wananchi akiamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee kwa Taifa kujitegemea.”
Sokoine alipata ajali katika barabara kuu ya Dodoma - Morogoro eneo la Wami Lukindo wilayani Mvomero mkoani Morogoro na eneo hilo kujengwa mnara wa kumbukumbu.
Jana, wanafunzi wa Shule ya Msingi Dakawa na vijana wa skauti walifanya usafi katika eneo hilo wakishirikiana na msimamizi, Hamis Mpandachalo.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Yakini Kikwembe alisema wameona ni vyema kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo ili kumkumbuka kiongozi huyo.
Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, Fatuma Saidi alisema anatamani kuiga vitendo ya Sokoine kwa kupiga vita rushwa.
Imeandikwa na Moses Mashalla (Arusha), George Njogopa (Dar) na Juma Mtanda (Morogoro).