'Wazee wa kubeti' kila mkeka kukatwa asilimia 10
Muktasari:
- Serikali imekusudia kuanza kutoza asilimia 10 katika kila dau la Kamari, ili isaidie kugharamia huduma za afya kwa watu wasiojiweza na makundi maalumu.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imekusudia kuanza kutumia michezo ya kubahatisha (kamari) kukusanya fedha zitakazotumika kulipia bima za watu wasiojiweza na makundi maalumu.
Hilo litawezekana baada ya kukusudia kuanza kutoza asilimia 10 kwenye thamani ya dau la kamari kwenye michezo ya kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa.
Pia, imetangaza kutoza asilimia 10 katika kila ada ya matangazo ya biashara za michezo ya kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa yanayotangazwa kupitia vituo vya televisheni, redio na tasnia ya uchapishaji.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akisoma mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25.
Dk Mwigulu amesema kupitia kuanzishwa kwa tozo hizo, Serikali inatarajiwa kukusanya kiwango kikubwa cha fedha.
Amesema mapato yatakayotokana na asilimia 10 kwenye thamani ya dau la kamari kwenye michezo ya kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa yatakuwa kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalumu, hususan wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
“Hatua hii inatarajia kupeleka kiasi cha Sh29.522 bilioni katika mfuko huo,” amesema Dk Mwigulu.
Dk Mwigulu amesema asilimia 10 itakayokusanywa katika kila tangazo katika vyombo vya habari vilivyoainishwa unalenga kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh9.15 bilioni.