Wenye nyumba Bonde la Msimbazi washtukiwa kutaka malipo ya wapangaji

Muktasari:

  • Sh52.6 bilioni zimetengwa kwa ajili ya fidia; watu 2,155 kati ya 2,329 wameshalipwa.

Dar es Salaam. Wamiliki wa nyumba zinazoguswa na mradi wa uendelezaji Bonde la Mto Msimbazi wakiwa wameshalipwa fidia na kuanza kuhama, kumeibuka malalamiko ya waliokuwa wapangaji katika nyumba hizo kutolipwa licha ya Serikali kuwaahidi malipo.

Kwa mujibu wa Serikali, malipo yamesitishwa kutokana na baadhi ya wahusika kubainika kughushi nyaraka.

Katika utekelezaji wa mradi huo unaogharimu Dola milioni 260 za Marekani (Sh675 bilioni), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), wenye nyumba walifanyiwa tathmini na kufidiwa, huku wapangaji wakiahidiwa malipo ya Sh170,000 kwa ajili ya kusaidia usafiri watakapokuwa wanahama.

Imeelezwa Sh52.6 bilioni zimetengwa kwa ajili ya fidia na mpaka sasa watu 2,155 kati ya 2,329 wameshalipwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), ambao ni watekelezaji wa mradi huo, unaosimamiwa na Wizara ya Tamisemi.

Miongoni mwa wapangaji hao, Asia Fupe, akizungumza na Mwananchi Digital amesema alikuwa na nyumba Jangwani lakini baada ya kuvunjwa mwaka 2016 akaenda Mtaa wa Magomeni Suna kupanga, akilipa Sh35,000 kwa mwezi.

Asia amesema kila wanapouliza kuhusu fedha walizoahidiwa wanajibiwa kuwa wasubiri, licha ya kuwa tayari wameshafungua akaunti kama walivyotakiwa na kusainishwa kwa ajili ya malipo.

“Hali hii imeniathiri, hapa nilipokuwa nimepanga imebidi nitafute sehemu nyingine jirani kwa kuwa sina hela ya kusafirisha mizigo,” amesema.

Mbali ya hilo, amesema fedha ambayo Serikali inawalipa ni ndogo ikizingatiwa kuwa wenyewe nyumba kwa sasa wanataka kodi ya kuanzia miezi mitatu na kuendelea, hivyo walau wangepewa Sh350,000.

Said Hassan, amesema suala la wapangaji kulipwa na Serikali ndilo limewapa tabu, akieleza ni vema wangewaacha wakamalizana na wenye nyumba.

“Kwa kuwa walitangaza hili mbele ya wenye nyumba nao walivyopata malipo yao wameondoka bila kutupa hata shilingi kumi,” amesema.

Said, mwenye familia ya watu sita amesema mpaka sasa amehifadhiwa kwa jirani.

Amesema mpango wake ni kuwa akipata fedha arudi kijijini kwao mkoani Morogoro.

Hata hivyo, amesema ana shaka iwapo fedha hizo zitatosha kusafirisha familia na mizigo.

Ameiomba Serikali kwa wale ambao nyaraka zao zimejitosheleza walipwe ili kuwaondolea adha ya kuishi kwenye nyumba za watu.

Habiba Mondoma, mwakilishi wa wananchi katika mitaa 18 inayopitiwa na mradi huo, ameiomba Serikali kuharakisha malipo kwa kuwa wapo wananchi wanaolala kwenye baraza za watu na wengine ndani ya nyumba zilizobomolewa, hivyo kuhatarisha afya zao na hasa kipindi hiki cha mvua.

Serikali yatoa ufafanuzi

Ofisa Habari Mwandamizi wa Mradi wa Bonde la Msimbazi, Raphael Kalapilo, amekiri kutengwa fedha za malipo kwa ajili ya wapangaji.

Hata hivyo, amesema kuna changamoto zimejitokeza hivyo wameamua kusitisha kuwalipa.

“Ni kweli kuna malipo ya Sh170,000 ambazo ni kiwango sawa kwa wapangaji wote wa nyumba zilizoguswa na mradi. Serikali iliamua iwalipe kama fedha ya usumbufu kuwasaidia kuhama. Wanaolipwa ni wale ambao walikutwa kwenye nyumba wakati uthamini ukifanyika,” amesema.

Kalapilo amesema, “Lakini kumejitokeza changamoto wakati wa uandikishaji, tumekuta wengi waliojiandikisha wameghushi nyaraka.”

“Mfano kuna waliojiandikisha kuwa ni wapangaji lakini tulipohakiki tukakuta ni walewale wenye nyumba ambao walishalipwa fidia, mbaya zaidi wengine wameweka hadi majina ya watoto wao kuwa ni wapangaji, hivyo tukaamua kusitisha kutoa malipo mpaka tutakapopitia upya nyaraka hizo na kujiridhisha,” amesema.

Amesema pia wapo ambao hawana mikataba ya upangaji kama ambavyo mkataba wa malipo ya fidia unavyowataka.

Kalapilo amebainisha kati ya wapangaji 395 waliojitokeza, wenye mikataba ni 181.

Amesema kati ya hao 181, asilimia 80 wameghushi nyaraka ambazo inabidi zipitiwe upya.

Licha ya ulipaji fidia kuwahusisha wapangaji wa nyumba za makazi na biashara, inaelezwa hakuna wafanyabiashara waliojitokeza.

Moja ya vigezo walivyotakiwa kuwa navyo ni vielelezo vya miaka mitatu vya kulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).