Wakazi bonde la Msimbazi walalamika majina yao kutorudi

Muktasari:

  • Hii ni baada ya wao kukubali kulipwa fidia kupisha mradi wa uboreshaji wa bonde hilo, wanashangaa majina yao kutorudi ili walipwe.

Dar es Salaam. Wakati shughuli ya ulipaji fedha za fidia kwa wakazi wanaopisha mradi wa uendalezaji wa bonde la mto Msimbazi ikiwa imeanza, baadhi ya majina hayajarudi licha ya kukubali kulipwa fidia hiyo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Novemba 23, 2023 na mwenyekiti wa kamati ya waathirika wa fidia Mtaa wa Msimbazi Bondeni, Saleh Cheyo, alipozungumza na Mwananchi Digital.

Pia wananchi hao wamesema Sh4 milioni walizoongezwa kwa ajili ya kulipwa fidia ya ardhi ambayo haikuwepo awali, nayo haijaingia hivyo wamebaki njia panda hawajui lini hasa watalipwa.

Nyongeza ya fidia hizo zilitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mohammed Mchengerwa alipokutana na wananchi hao kwenye viwanja vya Jangwani akisema ni fidia ya ardhi tofauti na ile ya awali ambayo ilihusisha ulipaji wa jengo pekee.

Akitoa tangazo hilo, Mchengerwa alisema Serikali imeamua iwalipe watu wote Sh4 milioni, licha ya kuwa hawakustahili kupewa fedha hizo kwa kuwa eneo hilo linatambulika kama ni sehemu isiyofaa kuishi watu (eneo oevu).

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekubali fidia hiyo huku wengine wakisema ni ndogo, kwani haiendani na thamani ya eneo husika.

Akizungumzia majina kutorudi, Cheyo amesema kuna majina yapatayo 40 hayajarudi na wala hawajui hatma ya wao kulipwa fidia.

Akizungumzia hilo, mratibu msaidizi wa mradi huo kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura), Emmanuel Manyanga amesema majina kutorudi kumechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi kuenguliwa.

“Kuna majina yameenguliwa kutokana na ukweli kwamba hawa walishalipwa viwanja Mabwepande, lakini pia wapo wanaoendelea kuhakikiwa kutokana na taratibu za kimalipo za kibenki zinavyotaka wakiwemo wale wenye akaunti mpya,” amesema na kuongeza;

"Wenye akaunti mpya lazima benki ijidhihirishe hela waliyopokea inatoka wapi, lakini hata na walizonazo siku nyingi kama mtu hakuwahi kupokea kiasi kikubwa cha hela, lazima benki ijidhirishe imetokea wapi ndio maana mchakato umechukua muda mrefu."

Manyanga ameitaja sababu nyingine inatokana na wanufaika kuwa na akaunti katika benki tofauti na ile ambayo fedha za mradi zipo.

"Fedha zote za mradi zipo benki ya NMB, hivyo wananchi wengine utakuta wana akaunti tofauti na ya benki hiyo, hivyo mchakato wake lazima uwe mrefu kidogo kwa kuwa hapa ni mpaka NMB washirikiane na Benki Kuu ya Tanzania kujidhihirisha kuwa anatelipwa ndiye," amesema Manyanga.

Hata hivyo, mratibu huyo amesema malengo yao ni hadi kufika mwishoni mwa Novemba wawe wamemaliza kuwalipa watu wote 2,592 wanaopaswa kulipwa fidia hiyo.

Shabani Hamisi mkazi wa msimbazi Bondeni ambaye ameshaingiziwa hela yake amesema anashukuru hata kwa hicho kidogo alichopata kuliko angekosa kabisa.

Hamisi amesema awali katika matarajio yake ilikiwa walau alipwe Sh25 milioni, lakini matokeo yake amelipwa Sh7 milioni.

"Naishukuru Serikali, lakini ukweli ni kwamba hela ni ndogo ukizingatia nyumba yangu yenye vyumba viwili nilitumia gharama kubwa kujijenga ikiwemo kuweka vifusi, lakini nitafanyaje imebidi nikubali ikizingatia asilimia kubwa watu wamekubali kulipwa mimi nani,” amehojihoji na kuongeza;

"Unaweza kuigomea hiyo hela baadaye ukaja kupata usumbufu, hata hiyo kidogo wasikulipe, si unajua tena Serikali ikitaka jambo lake."

Katika hatua nyingine, wananchi zaidi ya 100 wanagomea fidia, wameomba kuonana na uongozi wa Tarura, Mkuu wa Mkoa au Waziri Mchengerwa kuweza kufikisha malalamiko yao ya kwa nini wamegomea fedha hizo.

Mwenyekiti wa wananchi wa mitaa 16 ambao wanaathirika na mradi huo, Charles Swai amesema waliambiwa milango ipo wazi ya mazungumzo ni vema wakayafanye kwa kuwa wanaamini majadiliano ni njia nzuri zaidi.

"Tumejipa wiki moja yaani hii ya leo kukutana na watu hao na baadhi tulishafika ofisini kwao kuomba ahadi ya kukutana na wengine kuwaandikia ujumbe mfupi baada ya simu zao kuzipiga bila kupokelewa," amesema mwenyekiti huyo.