Fidia wanaopisha Bonde la Mto Msimbazi yawagawa wakazi

Dar es Salaam. Hisia mchanganyiko za wakazi wa bonde la Mto Msimbazi kufuatia tamko la Serikali kuwa watalipwa fidia ya ardhi ya Sh4 milioni kwa kila mwenye eneo, imeibuka huku wengine wakiunga mkono uamuzi huo, na wengine wakiupinga.

Awali kulikuwa na malalamiko ya wakazi hao baada ya kuonekana kuwa watafidiwa nyumba zao na si vinginevyo.

Kassim Said amehoji iweje wananchi wa Loliondo wao walilipwa vizuri na kujengewa hadi nyumba lakini wao wanaokaa mjini wanapewa kiasi hicho kidogo cha fedha?

"Kwa mfano mimi nyumba yangu ya vyumba vitatu nimelipwa Sh11 milioni nikichanganya na hiyo Sh4 milioni ina maana nina Sh15 milioni, niambie naweza kujenga nyumba ya kiwango hicho hapa mjini? Ngoja tumwachie Mungu yeye ndio anajua," amesema Said.

Lakini hali ni tofauti kwa Siasa Mtambo, ambaye ameridhishwa na uamuzi huo, kwani kwa muda wa miaka 30 amekuwa akiishi kwa tabu katika eneo hilo kutokana na ukweli kuwa hakuwa na uwezo wa kwenda kujenga sehemu nyingine, pengine kwa hicho kidogo walichopewa ataweza hilo kulifanya.

Aisha Sharif mmoja wa wananchi waliokataa fidia kutokana na kutoridhishwa na tathimini, amesema kilichomfurahisha ni kitendo cha Waziri huyo kuahidi kuwasikiliza wote waliokataa pendekezo hilo.

"Hao waliokubali waachwe walipwe kwa kuwa kila mtu anajua thamani ya nyumba yake wengine kuliko tulipwe hiyo hela ni bora tuendelee kubaki hapa mjini," amesema Aisha.

Haya yote yanajiri baada Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa alipokutana na wananchi hao leo Jumatano Novemba 15, 2023 katika viwanja vya jangwani jijini humo, na kutangaza kuwa kesho (Alhamisi) Serikali itaanza kulipa fidia ya Sh4 milioni kwa kila mwenye ardhi itaanza kulipwa kesho.

Kimsingi, wananchi hao walikuwa na malalamiko wakitaka aina mbili za fidia kufanyika, ile ya nyumba pamoja na hiyo ya ardhi, jambo ambalo awali Serikali ilikubali kuwafidia nyumba pekee.

"Tulisikia malalamiko yenu kupitia nyie wenyewe, viongozi wenu akiwemo Mkuu wa Mkoa, Madiwani na Wabunge, nami nikalifikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kwa kuwapenda jana ameridhia kila mwananchi anayepisha mradi huu alipwe Sh4 milioni kama kifuta jasho kwa ardhi aliyoimiliki.

"Kwani kama mlivyosikia wataalam wetu hili walisema ni eneo la ardhi owevu hivyo kisheria halikupaswa kulipwa fidia kwa kuwa sio salama kwa makazi, lakini kwa huruma ya mama amemua mlipwe hiyo Sh4 mlioni,” amesema Mchengerwa.

Sambamba na hilo la ulipaji fidia hiyo ya ardhi ambayo kimsingi ni tofauti ile fidia ya jengo, Waziri huyo aliagiza pia Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), kuanza mara moja ujenzi wa mradi huo huku malipo ya fidia yakiendelea ili kupunguza adha ya mafuriko katika eneo hilo yanayoathiri shuguli za kila siku za wananchi.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alisema anachojua mkoa huo hauna mafuriko isipokuwa watu ndio wameziba njia zinazopitisha maji kwa kujenga na kuishi maeneo ambayo maji yanapaswa kupita.